Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 10 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Kikundi cha Wahafidhina wa Ulaya na Wanamageuzi wa Bunge la Ulaya. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 10 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Kikundi cha Wahafidhina wa Ulaya na Wanamageuzi wa Bunge la Ulaya.  (@Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Wabunge wa Bunge la Ulaya: Demokrasia & Utu

Papa Leo XIV, Jumatano tarehe 10 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Kikundi cha Wahafidhina wa Ulaya na Wanamageuzi wa Bunge la Ulaya Katika hotuba yake amewataka wajumbe hawa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; wakuze demokrasia; watambue na kuthamini mchango wa dini katika kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Ulaya: Urithi wa dini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri!

Bunge lijitahidi kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli
Bunge lijitahidi kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 10 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Kikundi cha Wahafidhina wa Ulaya na Wanamageuzi wa Bunge la Ulaya (European Conservatories and Reformists Group of the European Parliament.) Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka wajumbe hawa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; wakuze na kudumisha demokrasia; kutambua na kuthamini mchango wa dini katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Ulaya sanjari na urithi wa kanuni maadili na utu wema, unaopata chimbuko lake katika msingi wa dini ya Kiyahudi na Kikristo! Amewashukuru kwa kuchaguliwa kuwa ni wawakilishi wa wananchi katika Bunge la Ulaya, jukumu ambalo linapaswa kuendelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii, watu ambao Kristo Yesu aliwaita: “wadogo zaidi” kati yetu. Rej. Lk 9:48.

Wabunge wakuze utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana kwa adabu
Wabunge wakuze utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana kwa adabu   (@Vatican Media)

Bunge liwe tayari kupokea maoni mbalimbali na kuyajadili, kwa kuheshimu tofauti zake msingi; kwa kuyajadili kwa heshima na adabu; kwa uwezo wa kutokubaliana, na kwa kusikilizana kwa makini, na hata kuingia kwenye mazungumzo na wale ambao wanaweza kuwaona kama wapinzani kwa kuzingatia heshima na utu wao kama watoto wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe hawa kumtazama Mtakatifu Thomas More, mwombezi na mlinzi wa wanasiasa, ambaye hekima, ujasiri na ulinzi wa dhamiri ni kati ya mambo ambayo aliyapatia msukumo wa pekee, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ustawi wa jamii. Amewataka wajumbe hawa kukuza na kulinda urithi wa kidini unaopata chimbuko lake katika dini ya Kiyahudi na Kikristo, kwa kusimama kidete kulinda: haki msingi za binadamu; kutambua ukweli na kuusimamia na kwamba, mchango wa Jumuiya ya Kikristo umewanufaisha watu wote wa Bara la Ulaya; kwa kutambua na kuthamini hazina kubwa ya: Kitamaduni kwa Makanisa yake makuu, Sanaa ya hali ya juu na muziki, na maendeleo ya sayansi, bila kusahau kukua na kuenea kwa vyuo vikuu.  Maendeleo haya yanaunda kiunganishi cha ndani kati ya Ukristo na historia ya Ulaya, historia ambayo inapaswa kuthaminiwa na kuadhimishwa.

Kipaumbele kiwe ni kwa maskini na wanaosukumizwa pembezoni
Kipaumbele kiwe ni kwa maskini na wanaosukumizwa pembezoni   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia pia kanuni maadili na utu wema; Kulinda na kudumisha Injili yua uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na kwamba, wasimame kidete kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoletwa na umaskini, kutengwa na jamii, kunyimwa haki za kiuchumi, na pia kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ghasia na vita. Mama Kanisa kupitia Mafundisho Jamii ya Kanisa anaendelea kukazia ili rasilimali muhimu za umoja, ushirikiano na mshikamano zinadumishwa kwa sasa na kwa siku zijazo. Baba Mtakatifu Leo XIV amesisitizia kuhusu majadiliano kati ya “ulimwengu wa akili na ulimwengu wa imani – ulimwengu wa busara za kilimwengu na ulimwengu wa imani ya kidini” mchango uliotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI (Hotuba kwa Jumuiya ya Kiraia, Westminster Hall, London, 17 Septemba 2010). Wanasiasa wanalo jukumu muhimu sana kwa ajili ya kuheshimu uwezo maalum wa kila mmoja, na pia kwa ajili ya kupeana yale ambayo wengine wanahitaji, yaani jukumu la "kusafisha" kwa pande zote mbili kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hakuna mawindo ya upotoshaji (taz. ibid.) Amewaomba Wabunge hawa kujihusisha vyema katika mazungumzo haya muhimu, sio tu kwa ajili ya watu wa Ulaya, lakini kwa ajili ya familia yote ya kibinadamu.

Papa Leo XIV Wabunge
10 Desemba 2025, 15:33