Tafuta

Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu iliyonzishwa kunako mwaka 2019. Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu iliyonzishwa kunako mwaka 2019.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan Kwa Mwaka 2026

Papa Leo XIV amekutana na waandaaji wa Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan kwa mwaka 2026 na ametumia fursa hii kuwapongeza wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa kutoa karama na mapaji yao, maono, kanuni maadili na utu wema kwa ajili ya ujenzi na huduma kwa udugu wa kibinadamu. Tuzo hii inaendelea kupyaisha amana na utajiri wa Sheikh Zayed na kwamba, watu wote wanachangamotishwa kujenga udugu wa kibinadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji wa Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Katika kipindi cha Mwaka 2019 Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kitume nchini Morocco na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu ambako kuna idadi kubwa ya waaamini wa dini ya Kiislam. Lengo lilikuwa ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili waamini wa dini hizi mbili waweze kufahamiana, kama sehemu ya kumbukumbu endelevu na angavu ya miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultan Al Malik al- Kamil kunako mwaka 1219.

Tuzo ya Sheik Zayed Bin Sultan kwa Mwaka 2026
Tuzo ya Sheik Zayed Bin Sultan kwa Mwaka 2026   (@Vatican Media)

Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ilianzishwa kunako mwaka 2019. Haya ni matunda ya ushirikiano na majadiliano ya kidini kati ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ulioanzishwa tarehe 2 Desemba 1971 ilitolewa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Viongozi hawa ndio waasisi pia wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu. Tuzo hii pamoja na mambo mengine, inapania: Kunogesha jitihada za watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali zinazojipambanua katika kutafuta, kujenga na kukuza mahusiano na mafungamano ya kibinadamu. Inalenga kujenga madaraja ya majadiliano ya kidini sehemu mbalimbali za dunia; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi Tuzo hii ni alama ya ushirikiano na mshikamano kati ya waamini wa dini mbalimbali wanaojipambanua katika huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Tuzo ya Sheik Zayed ilianzishwa mwaka 20219
Tuzo ya Sheik Zayed ilianzishwa mwaka 20219   (Vatican Media)

Ni katika muktadha huu wa Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu iliyonzishwa kunako mwaka 2019, Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 11 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na waandaaji wa Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan kwa mwaka 2026 na ametumia fursa hii kuwapongeza watu wa Mungu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa kutoa karama na mapaji yao, maono, kanuni maadili na utu wema kwa ajili ya ujenzi na huduma kwa udugu wa kibinadamu. Tuzo hii inaendelea kupyaisha amana na utajiri wa Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan na kwamba, watu wote wanachangamotishwa kujenga udugu wa kibinadamu, kwa kuchangia amana na urithi wao wa maisha ya kiroho, kwa ajili ya huduma kwa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Katika kinzani, migogoro na vita anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, walimwengu wanahitaji mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo; wanaomwilisha Injili ya upendo katika uhalisia wa maisha ya jirani zao ili kukuza na kudumisha matumaini. Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan inawakumbatia, kuwaambata na kuwaheshimu watu binafasi pamoja na taasisi zinazojipambanua katika kumwilisha fadhila ya huruma na mshikamano, kwa kuonesha mfano halisi jinsi ya kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu, katika Ulimwengu mamboleo. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewahakikishia waandaaji hawa sala zake na kuwatia shime kuendelea na kazi hii, ili nguvu zao ziweze kuzaa matunda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu.

Tuzo 2025
11 Desemba 2025, 15:12