Tafuta

Papa Leo XIV Jumatatu tarehe 22 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Vatican kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana heri na baraka katika Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Papa Leo XIV Jumatatu tarehe 22 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Vatican kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana heri na baraka katika Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Salam za Noeli Kwa Wafanyakazi wa Vatican 2025: Pango la Noeli

Baba Mtakatifu Leo XIV kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumatatu tarehe 22 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, Wafanyakazi wa Vatican pamoja na wale wa Jimbo kuu la Roma, wakiwa wameambatana na familia zao, ndugu na jamaa zao. Ametumia fursa hii, kuwashukuru wote kwa kazi kubwa wanayoitekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumatatu tarehe 22 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, Wafanyakazi wa Vatican pamoja na wale wa Jimbo kuu la Roma, wakiwa wameambatana na familia zao, ndugu na jamaa zao. Ametumia fursa hii, kuwashukuru wote kwa kazi kubwa wanayoitekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Mama Kanisa. Pole pole anasema, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu anatarajia kukutana na kila mmoja wao katika maeneo yao ya kazi. Pango la Noeli kwa Mwaka 2025 limetolewa na watu wa Mungu kutoka Costa Rica. Kwa mara ya kwanza, Pango la Noeli halikuwa limepambwa kwa sanamu mbalimbali kama zinavyonekana wakati huu. Pole pole, Pango la Noeli likapambwa kwa Sanamu ya Mtoto Yesu aliyelazwa kwenye hori la kulishia wanyama. Na wote walioshuhudia tukio hili wakarejea makwao wakiwa wamesheheni furaha kubwa nyoyoni mwao.

Papa Leo XIV Salam za Noeli kwa wafanyakazi wa Vatican: Pango la Noeli
Papa Leo XIV Salam za Noeli kwa wafanyakazi wa Vatican: Pango la Noeli   (@VATICAN MEDIA)

Haya ni matunda ya uinjilishaji uliofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi, kiasi kwamba, mafundisho yake, hadi leo hii yanaendelea kugusa sakafu ya maisha ya waamini kwa njia ya imani. Pango la Noeli ni kielelezo cha: huruma na upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru! Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Malaika wa Bwana na nyota angavu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenda kumwabudu Mwana wa Mungu.

Papa Leo XIV: Injili ya Pango la Noeli: Unyenyekevu
Papa Leo XIV: Injili ya Pango la Noeli: Unyenyekevu   (@Vatican Media)

Wachungaji wakawa ni watu wa kwanza kuona zawadi ya ukombozi. Maskini na wanyenyekevu wa moyo wakashuhudia Fumbo la Umwilisho. Kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu akapata tena nafasi ya kukutana na watoto wake katika mazingira ya Pango la Noeli. Mazingira ya Pango la Noeli kwa kawaida yanapaswa kuonesha uwepo wa maskini wanaothamini zaidi ufukara wa maisha ya kiroho. Hawa pia wanayo haki ya kuwa karibu na Mtoto Yesu na wala asiwepo mtu anayetaka kuwafukuzia mbali! Katika muktadha huu, nyumba inakuwa ni mahali pa ukarimu kwa maskini, kwa sababu hawa ndio watu wa kwanza kabisa kutambua uwepo wa Mungu kati ya waja wake na hawa kimsingi ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu. Pango la Noeli ni ukumbusho kwamba, utajiri na raha za dunia ni mambo mpito.

Noeli yenye furaha, amani na utulivu kutoka kwa Kristo Yesu
Noeli yenye furaha, amani na utulivu kutoka kwa Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwenye Pango la Noeli kwa kweli kuna fani za zamani: nyingine zimepotea au zimebadilishwa kabisa. Lakini zinaendelea kuhifadhi maana yao ya ndani ya tukio la kuzaliwa kwa Kristo Yesu. Zinawakumbusha waamini kwamba: shughuli zao zote, kazi zao za kila siku, zinapata maana yake kamili katika mpango wa Mungu, ambao una kiini chake katika Kristo Yesu, chemchemi ya neema na baraka zote; kielelezo cha unyenyekevu, huruma na upendo wa Mungu. Mtoto Yesu anaabudiwa na kutukuzwa na Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu pamoja na wachungaji. Kila mtu anatekeleza dhamana na wajibu wake wa kila siku, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa; waamini walei wajenge upendo kwa familia zao kwani kwa kufanya hivyo, wanamtukuza Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutokana na kuzaliwa kwa Mtoto Yesu mtindo wa usahili na unyenyekevu, ili kuhakikisha kwamba, huu ndio unakuwa ni mtindo wa maisha na utume wa Kanisa. Mwishoni, amewataka wafanyakazi wote hawa kuwafikishia salam na matashi mema, wapendwa wao waliosalia nyumbani, hasa wagonjwa na wazee, wawaambie kuwa Baba Mtakatifu anawaombea. Mwishoni, amewatakia Noeli Njema na Takatifu, yenye furaha, amani na utulivu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Papa Leo XIV Wafanyakazi wa Vatican
22 Desemba 2025, 14:59