Papa Leo XIV: Noeli Ni Sherehe ya Imani, Upendo na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kadiri ya Mapokeo ya tangu zamani za kale Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, yaani Noeli ya Bwana yanafanyika Usiku wa manane, ili kuwakumbusha waamini usiku ule mtakatifu utukufu wa Mungu ulipowang’aria wachungaji waliokuwa kondeni: “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Lk 2: 8-11. Kama sehemu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Waamini wamehimizwa kujiandaa kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa kwao kwa: Njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa katika Mkesha wa Sherehe ya Noeli, waamini kwa namna ya pekee wanampokea Kristo Yesu kama Kiini cha Injili ya Matumaini yasiyodanganya kamwe. Hii ni fursa ya kusikiliza, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu mintarafu uhalisia wa maisha na utume wa kila mwamini. Kitabu cha Orodha ya Majina ya Wafiadini wa Roma “Roman Martyrology” kinaonesha kwamba, Siku Nane Kabla ya Maadhimisho ya Mwaka Mpya Kadiri ya “Kalenda ya Januari” yaani tarehe 25 Desemba, Kristo Yesu anazaliwa na Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa hakika Kristo Yesu ni kitovu cha historia na Ulimwengu.
Baba Mtakatifu Leo XIV, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, katika tafakari yake amejikita katika: Hekima ya Noeli inayofumbatwa katika amani "isiyo na silaha na inayopokonya silaha. Noeli ni chemchemi ya Injili ya matumaini na furaha ya kweli; ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu na utume unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo. Tafakari ya Fumbo la Umwilisho, Neno aliyefanyika mwili inatia moyo neno jipya na la kweli katika Kanisa lote kwa kuwataka waamini kutangaza na kushuhudia furaha ya Noeli, ambayo ni adhimisho la fumbo la imani, mapendo na matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu. Ni sherehe ya matumaini, kwa sababu Mtoto Yesu anawasha tena matumaini ndani ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa ni vyombo na wajumbe wa amani. Wakiwa wamesheheni fadhila hizi nyoyoni mwao, kamwe hawawezi kuogopa usiku na kwamba, wanaweza kukabiliana kikamilifu na changamoto ya mapambazuko ya siku mpya. Nabii Isaya alitabiri na kusema; “Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.” Isa 9:2. Na Malaika wakawatangazia wachungaji kondeni kwamba: “maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Lk 2:11.
Huyu ndiye Kristo Bwana anayekuja kusadaka maisha yake na kuangazia usiku wa giza la maisha ya mwanadamu. Huyu ndiye yule Mtoto aliyelazwa kwenye Hori ya kulia ngombe. Hii ni Sherehe ya Kuzaliwa Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini kuutafakari ukuu wa Mungu unaofumbatwa katika udhaifu wa Mtoto mchanga; Utakatifu wa Roho Mtakatifu unang’ara katika uso wa Mtoto Yesu anayeshiriki kikamilifu maisha ya ndugu zake na kwamba, Mwanga Mtakatifu kutoka kwa Mtoto Yesu, unawawezesha waamini kuona maisha ya kila mtoto anayezaliwa.Katika Sherehe ya Noeli, Mwenyezi Mungu ameufunua mpango wake wa upendo aliokuwa nao tangu kuumbwa kwa Ulimwengu, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kutoa nafasi kwa watoto, maskini na wageni. Inasikitisha kuona kwamba, hapa duniani hakuna nafasi kwa Mungu na wala kwa mwanadamu, lakini kinyume chake ni ukweli usiopingika kiasi kwamba, Hori la kulishia wanyama linaweza kuwa kielelezo cha Utakatifu na tumbo la Bikira Maria likawa ni Sanduku la Agano Jipya. Unyenyekevu wa Kimungu ndiyo fadhila iliyo mnyanyua mwanadamu. Inasikitisha kuona kwamba, mwanadamu anataka kujifanya kuwa Mungu ili awatawale jirani zake na kwamba, upendo wa Mungu ungetosha kubadili historia ya walimwengu, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, na Yosefu, wakikesha usiku ule Mtakatifu, kwani katika Moyo Mtakatifu wa Yesu unaunganisha upendo wa kimbingu na upendo wa kidunia; Mungu Muumbaji na Kiumbe chake.
Kabla ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kesha la Noeli kwa Mwaka 2025, Baba Mtakatifu alielekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kusalimiliana na waamini zaidi ya 5,000 waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakifuatilia kwa karibu maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ni kubwa, lakini haliwezi kuwaingiza waamini wote, anawaheshimu na kuwashuruku kwa ujasiri pamoja na hamu ya kuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro katika Mkesha wa Sherehe ya Noeli, ili kuweza kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu aliyezaliwa anawaletea amani na upendo wa Mungu. Takwimu zinaonesha kwamba, ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kulikuwemo waamini zaidi ya 6, 000.
