Papa Leo XIV Ateta na Rais wa Ukraine Kuhusu Mustakabali wa Nchi ya Ukraine
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumanne tarehe 9 Desemba 2025 akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amekutana na kuzungumza na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine. Katika mazungumzo yao ya faragha, viongozi hawa wawili wamegusia kuhusu umuhimu wa kuendeleza majadiliano kati ya Urusi na Ukraine na ni matumaini yao kwamba, mbinu mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa utasaidia kusitisha vita nchini Ukraine, ili hatimaye amani ya kudumu iweze kupatikana. Wafungwa wa kivita pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto kutoka Ukraine waliopelekwa nchini Urusi wanarejeshwa na hatimaye kuunganishwa na wazazi pamoja na familia zao na jinsi ambavyo Kanisa linaweza kusaidia kutekeleza mkakati huu.
Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na waandishi wa habari amesema, Vatican iko tayari kutoa nafasi na fursa ya mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine, ingawa, tangu sasa fursa hii bado haijapata nafasi kwa wahusika. Vatican iko tayari kuhakikisha kwamba, amani ya kudumu inayosimikwa katika haki inapatikana. Rais Volodymyr Zelenskyy, mara kwa mara amekuwa akimwalika Baba Mtakatifu kutembelea nchini Ukraine na kwamba, anayo nia ya dhati kabisa kuitembelea lakini, wanapaswa kuwa wa kweli kuhusu hali hali halisi, lakini iko siku hija hii ya kitume inaweza kufanyika. Vatican inaendelea kufuatilia kwa karibu mchakato wa kuwarejesha watoto kutoka Ukraine waliotekwa nyara, mchakato ambao unakwenda polepole na katika siri kubwa.
Mwishoni mwa mwezi Novemba 2025, utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump ulipendekeza mpango wa amani uliokosolewa vikali na Ukraine pamoja na washirika wake wa Ulaya kwa kuwa uliitaka Ukraine kuachia baadhi ya sehemu ya ardhi yake kwa Urusi. Aidha Rais Volodymyr Zelenskyy ameongeza kuwa yuko tayari kuandaa uchaguzi mpya nchini Ukraine ikiwa watahakikishiwa usalama huku akisisitiza kuwa Urusi haioneshi nia ya kuendelea na mchakato wa amani, kwani inaendeleza mashambulizi makali dhidi ya miundombinu yake ya nishati. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, kwa sasa hana maoni rasmi, kwani ni hajausoma kikamilifu mpango huo wa amani uliowasilishwa na Rais Trump na kwamba, Bara la Ulaya linayo nafasi muhimu katika kukuza na kudumisha amani nchini Ukraine.
Baba Mtakatifu anasema, akiwa kwenye Msikiti wa Blue nchini Uturuki alisali katika ukimya, kwa kuheshimu imani na tamaduni za waamini wa dini ya Kiislam waliokuwa wamekusanyika mahali hapa kwa sala. Lakini amekaza kusema, anapendelea kusali katika Kanisa Katoliki mbele ya Sakrameti kuu ya Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV, tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki bado anaendelea kuishi katika makazi yake ya awali na kwamba, bado hajahamia kwenye Jengo la Kipapa na kwamba, Makatibu wake, wanaishi pamoja naye kwa furaha na amani.
