Tafuta

Tajiriba ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki na Lebanoni inawafundisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, amani ni jambo linalowezekana.  Tajiriba ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki na Lebanoni inawafundisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, amani ni jambo linalowezekana.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Asema: Amani Duniani Ni Jambo Linalowezekana Kabisa

Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya amani, kwa kuendelea kujizatiti katika kutafuta na kudumisha amani kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni amani yao. Amani ya kweli inasimikwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili, changamoto kwa watu wote ni kujenga jamii inayopenda amani. Baba Mtakatifu Leo wa XIV anasema, amani duniani ni jambo linalowezekana, ikiwa kama watu wa Mungu watatia nia ya dhati kabisa na kuitekeleza kwa vitendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Majilio ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuweza kuinua utu na heshima yao, iliyokuwa imechakaa kutokana na dhambi, ili hatimaye, kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ni hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ile ya mwisho, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu; kama Kanisa linavyokiri na kufundisha kwenye Kanuni ya Imani. Kwa njia ya Kipindi cha Majilio, Mama Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake Kristo Yesu na hivyo waamini huweza kuchota na kujazwa na neema ya wokovu. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake wa daima anapenda kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Mafundisho, Sala pamoja na Matendo ya toba na huruma. Rej. Sacrosanctum concilium, 102-111. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika hija hii ya kitume amekazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija ya maisha ya kiroho kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, yaani miaka 2033 ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, huko mjini Yerusalemu.

Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA
Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA   (ANSA)

Yerusalemu ni mahali ambapo Kristo Yesu aliadhimisha Karamu ya Mwisho, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, Siku ile ya Pentekoste, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo huku akirejea kwenye kauli mbiu yake: "In illo Uno Unum" yaani "Ingawa Sisi Wakristo ni Wengi, Katika Kristo Mmoja Sisi ni Wamoja.” Hili ni tukio la kihistoria, ambalo litawakusanya Wakristo kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hadi sasa hakuna tarehe maalum ambayo imekwisha kupangwa. Lakini Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru viongozi wote walioshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325. Huu ulikuwa ni Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene kufanyika katika historia ya Kanisa na hivyo ukaibua imani ambayo ilikamilishwa na Mtaguso wa Kwanza wa Costantinopol ulioadhimishwa Mwaka 381 na hivyo kutoa dira na mwongozo wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wsa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 7 Desemba 2025 amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Anathegora wa Costantinopol na huo ukawa ni mwanzo mpya wa majadiliano ya kiekumene kwa kuondoa hati za utengano baina ya Makanisa haya mawili. Hija ya kitume iliyofanywa na Papa Paulo wa Sita, ilikuwa ni nyepesi, iliyojikita katika: moyo wa Sala na Ibada; toba na upendo. Lengo lilikuwa ni kufanya hija ya maisha ya kiroho ili kutoa heshima ya pekee kwa maeneo ambayo Mtakatifu Petro aliishi na kutekeleza utume wake. Ilikuwa ni tarehe 4 Desemba 1963, mara baada ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Papa Paulo wa sita alipotangaza kwamba, alikuwa na wazo la kutembelea Nchi Takatifu. Huu ulikuwa ni mwanzo mpya katika historia ya Kanisa katika mchakato wa kukabiliana na changamoto za Majadiliano ya Kidini na Kiekumene, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vianasa vya utume wa Kanisa
Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vianasa vya utume wa Kanisa   (ANSA)

Baba Mtakatifu Paulo wa sita, alibahatika kukutana na kuzungumza na Patriaki Athenagoras I (1886-1972), baada ya miaka mingi ya kinzani, chuki na migawanyiko ya Kikanisa kuanzia mwaka 1054 hadi mwaka 1965. Viongozi wakuu wa Makanisa wakakutana kwa pamoja mjini Yerusalem, kwenye chemchemi ya Injili na kufungua ukurasa mpya wa Majadiliano ya Kiekumene, unaoendelea kufanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka 60 kwa sasa, ili wote waweze kuwa ni wamoja chini ya Kristo Yesu mchungaji mkuu. Hii ni changamoto ya kupyaisha majadiliano ya kiekumene, ili kushuhudia umoja wa Kanisa unaoonekana, kama ushuhuda wa Injili ya upendo na mantiki ya Mwenyezi Mungu anayejifunua miongoni mwa wadogo. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt. 5:9. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon kujikita kikamilifu katika kutafuta na kudumisha haki na amani hata katikati ya mtutu wa bunduki na kwamba, hii ni changamoto endelevu dhidi ya: chuki, kiburi, utawala wa mabavu, utengano na uhasama!

Papa Leo XIV: Amani Duniani ni Jambo linalowezekana kabisa
Papa Leo XIV: Amani Duniani ni Jambo linalowezekana kabisa   (AFP or licensors)

Amewataka wawe wajenzi, watangazaji na mashuhuda wa amani! Huu ni wakati wa kuasha ile ndoto ya Lebanon inayosimikwa katika umoja, ili haki na amani iweze kutamalaki. Ikumbukwe kwamba, amani ni tunda la haki Rej Yak 3:18; kazi ya haki ni kuleta amani Rej. Isa 32:17 na kwamba, pasipo haki hakuna amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema amekutana na kuzungumza na watu wa Mungu wanatangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kwa njia ya ukarimu na upendo. Amekutana na kuzungumza na waathirika wa mlipuko wa Bandari ya Beirut, nchini Lebanon na ametumia fursa hii kuwafariji. Tajiriba ya hija hii ya kitume inawafundisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, amani ni jambo linalowezekana. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu walioathirika kwa mafuriko huko Barani Asia. Anawaombea wale wanaowaombolezea ndugu, jamaa na marafiki zao; wale wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika na kwamba, anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa waathirika hawa.

Papa Leo XIV Amani
08 Desemba 2025, 15:27