Papa Leo:Mwombeni Yesu nia ya Papa na tuombe watoto wote waishi kwa amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya nne ya Majilio, tarehe 21 Desemba 2025, akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican alisema: “kaka na dada, ninawasalimu kwa upendo nyote, Warumi na mahujaji kutoka Italia na sehemu zingine za dunia, hasa wale kutoka Jumilla, Hispania, na kundi la walimu kutoka Chuo cha Mama Yetu huko Hong Kong."
Papa Leo XIV akiendelea pia aliwasalimu waamini kutoka Chieti Scalo na Voghera, walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Sayansi ya "Banzi Bazoli" ya Lecce, na wanachama wa Mfuko wa "Agostiniani katika Ulimwengu " katika hafla ya maadhimisho ya kuanzishwa kwake.
"Kubariki sanamu za Mtoto Yesu"
Baba Mtakatifu kadhalika aliendelea kutoa salamu zake maalum kwa watoto wa kike na kiume wa Roma: "Wapendwa marafiki, mmekuja pamoja na familia zenu na makatekista kwa ajili ya kubariki sanamu za Yesu Mtoto, ili ziwekwe katika mapango ya kuzaliwa kwake nyumbani kwenu, shuleni, na katika vyumba vya ibada.” Papa alitoa shukurani kwa Kituo cha kuwapokea watoto cha Roma kwa ajili ya maandalizi ya tukio hili, na aliwabariki kwa moyo wote pamoja sanamu zote za Yesu Mtoto.
"Tuombe pamoja ili watoto wa dunia waishi kwa amani"
Papa leo aliendeea kusisitiza kuwa “Watoto wapendwa, mbele ya pango la kuzaliwa kwa Yesu, mwombeni Yesu pia kwa nia ya Papa. Hasa, tuombe pamoja ili watoto wote wa dunia waishi kwa amani. Asante kutoka moyoni mwangu! Na kwa Yesu Mtoto na maonesho yote ya imani yetu kwa Mtoto Yesu, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu awabariki kila wakati. Ninawatakia kila mtu Dominika njema na Noeli takatifu na yenye amani!
