Tafuta

Kardinali Parolin anasema, kuna haja ya kuimarisha haki, amani na utulivu ili kuwajengea matumaini vijana wa kizazi kipya Kardinali Parolin anasema, kuna haja ya kuimarisha haki, amani na utulivu ili kuwajengea matumaini vijana wa kizazi kipya  (AFP or licensors)

Kardinali Pietro Parolin: Jumuiya ya Kimataifa Isiyasahau Mateso ya Watu wa Msumbiji

Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii mjini Vatican anasema hija ya kitume nchini Msumbiji: Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 30 tangu Vatican ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Msumbiji tarehe 14 Desemba 1994, miaka 30 iliyopita sanjari na Jubilei ya Miaka 50 tangu Msumbiji ijipatie uhuru wake wa bendera pamoja na kuhitimisha Maadhimino ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Msumbiji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 5 Desemba hadi tarehe 10 Desemba 2025 katika mahojiano maalum na Vyombo vya Mawasiliano ya Jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican amesema, alifanya hija ya kitume nchini Msumbiji kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 30 tangu Vatican ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Msumbiji tarehe 14 Desemba 1994, miaka 30 iliyopita sanjari na Jubilei ya Miaka 50 tangu Msumbiji ijipatie uhuru wake wa bendera pamoja na kuhitimisha Maadhimino ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Msumbiji. Kardinali Parolin alikutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Msumbiji, wakiongozwa na Rais Margarida Adamugy Talapa. Dominika tarehe 7 Desemba 2025 alikutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji sanjari na kufunga Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa. Kardinali Parolin alisema kuna haja ya kuwa na maridhiano kati ya Kanisa la Serikali ya Msumbiji; ili kujenga na kuimarisha haki, amani na maridhiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Ni wakati wa kukazia, haki, amani, utulivu na usalama na zaidi sana kuendeleza majadiliano katika misingi ya ukweli na uwazi; majadiliano yanayowashirika watu wote wa Mungu nchini Msumbiji. Kardinali Parolin anasema, kuna haja ya kuimarisha haki, amani na utulivu ili kuwajengea matumaini vijana wa kizazi kipya. Jimboni Cabo Delgado, magaidi wanatumia umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, hali ya nyanyaso sanjari na ukwapuaji wa rasilimali za taifa kwa ajili ya mafao ya watu wachache ndani ya jamii. Kardinali Parolin anasema, ametumia siku mbili kutembelea Jimbo la Cabo Delgado, ili kuonesha upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV na Kanisa katika ujumla wake. Ulikuwa ni muda wa kutoa faraja kwa waathirika wa vitendo vya kigaidi; watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na wahamiaj. Takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kwamba, kulikuwa na watu 765, 000 wasiokuwa na makazi maalum.

Papa Francisko alipotembelea nchini Msumbiji 2019
Papa Francisko alipotembelea nchini Msumbiji 2019

Kambi ya Naminawe inahifadhi watu wasiokuwa na makazi 9, 200 na kati yao kuna watoto 3, 700 wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Hawa ni watoto wasiokuwa na fursa za kwenda shuleni na kwamba, vijana hawana ruksa ya kutoka kwenye kambi, ili kujitafutia maisha. Haya ni matokeo ya machafuko yaliyotokea kunako mwaka 2017 na hali kuwa ya hatari zaidi mwaka 2020. Haya ni machafuko ya kidini, kumbe kuna haja ya kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini kati ya Waislam na Wakristo, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Kimsingi watu wanaosababisha vurugu na machafuko ya kidini ni watu wachache wenye misimamo mikali ya kidini. Hii ni fursa kwa Wakristo kuendelea kuimarika katika imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kardinali Pietro Parolin anasema, inasikitisha sana kuona baadhi ya Mapadre na watawa wanazikimbia Parokia zao kutokana na changamoto ya ulinzi na usalama. Chama cha Misaada cha Kanisa Katoliki Caritas kimekuwa mstari wa mbele kutoa huduma kwa waathirika wa mashambulizi ya kigaidi huko Cabo Delgado na kwamba, wanashirikiana na Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma sanjari na kurejesha mahusiano mema kati ya wananchi wa Msumbiji. umuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika “Southern African Development Community kifupi: SADC.” iliundwa huko Lusaka, Zambia, tarehe 1 Aprili 1980 imekuwa ikisaidia kuimarisha ulinzi na usalama, lakini hiki ni kikundi kidogo. Kardinali Parolin anasema, kwa waamini “silaha” yako kubwa ni sala na upendo wa udugu wa kibanadamu; kuwasaidia na kuwahudumumia kama ndugu katika Kristo Yesu.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa Nchini Msumbiji 2025
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa Nchini Msumbiji 2025

Kardinali Parolin, akiwa nchini Msumbiji, ametembelea Kituo cha Huduma Kwa Maskini, “Casa Mateus25. Tarehe 8 Desemba 2025, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ametembelea Jimbo Katoliki la Pemba na hatimaye, kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na wa kidini na baadaye, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, tarehe 9 Desemba 2025 amekutana na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Msumbiji na baadaye, amefanya majadiliano ya kiekumene na kidini na viongozi mbalimbali nchini Msumbiji. Kardinali Parolin katika hotuba yake kama sehemu ya kumbukumbu ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Vatican na Msumbiji na Jubilei ya Miaka 50 tangu Msumbiji ijipatie uhuru wake, alikazia kuhusu: umoja na ushirikiano kati ya Vatican na Msumbiji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji, hali inayodhihirishwa na uwepo wa Balozi mkazi kutoka Msumbiji mjini Vatican. Haya ni mahusiano yanayosimikwa katika utu, heshima, uhuru wao wa kidini, utetezi pamoja na haki zao msingi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Katika diplomasia Kanisa daima linamtazama Kristo Yesu, ambaye mbele ya Pilato alijitangaza kuwa Mfalme, lakini wa Ufalme ambao si wa ulimwengu huu. Rej. Yn 18:36-37. Na kisha, alipoulizwa kuhusu sababu ya Ufalme wake kati ya wanadamu, Yesu alieleza akisema: “Kwa ajili ya hili nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie ile Kweli.” Yn 18:37.

Kardinali Parolin, Jumuiya ya Kimataifa isiyasahau mateso ya watu wa Msumbiji
Kardinali Parolin, Jumuiya ya Kimataifa isiyasahau mateso ya watu wa Msumbiji   (AFP or licensors)

Kardinali Parolin anasema, Kanisa Katoliki, kama jumuiya ya kiulimwengu inayowaleta pamoja waamini kutoka mabara yote, watu, lugha na tamaduni zote, lina wito mzito wa kujenga na kudumisha umoja na ushirika. Kanisa linaungana na kukusanya; haigawanyi wala kupinga. Linatafuta njia za uelewano na ushirikiano wa amani, likijitahidi, pamoja na njia zinazoweza kupatikana, kuepusha migogoro, migawanyiko, vita na uharibifu katika familia kubwa ya binadamu. Miaka 30 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Msumbiji na Vatican ni ushuhuda kwamba: Msumbiji inatambua na kuthamini: mwelekeo wa kidini na kimaadili wa matatizo ya binadamu, ambamo Kanisa linapania pamoja na mambo mengine kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika: ukweli, upendo na imani; Uadilifu na utu wema. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1988 alitembelea Msumbiji kama alivyofanya Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Hija yake kitume nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 ikiongozwa na kauli mbiu “Matumaini, amani na upatanisho." Papa Francisko alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji. Alikazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, viongozi wa wakuu wa Serikali ya Msumbiji kwa nyakati tofauti wametembelea Vatican. Papa Leo XIV anakazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa kutafuta, kulinda na kudumisha Injili ya Amani na kwamba, Msumbiji ina kiu kubwa ya amani.

Kuna watu wanaoteseka kwenye kambi za watu wasiokuwa na makazi maalum
Kuna watu wanaoteseka kwenye kambi za watu wasiokuwa na makazi maalum   (AFP or licensors)

Kardinali Parolin amekumbushia kwamba, mwaka mmoja uliopita, kufuatia uchaguzi mkuu, Msumbiji ilitumbukia katika mzozo mkubwa ulioandamana na ghasia na vifo. Katika nyakati hizo ngumu na zenye msukosuko, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, lilitoa wito kwa kila mtu kutokubali kushindwa na kishawishi cha vurugu na vita, na hivyo, kuwaalika Wakatoliki na wananchi wote wa Msumbiji wenye mapenzi mema kujitolea kila siku kusali kwa ajili ya amani. Baada ya miezi hiyo, Msumbiji ilifunguka kwa matumaini na dhamira ya sasa ya kisiasa ya "Mazungumzo Jumuishi ya Kitaifa," yenye lengo la kufikia makubaliano ya mapitio ya Katiba na marekebisho ya vipengele mbalimbali vya mfumo wa serikali, ambayo inapaswa kukuza uwazi wa kitaasisi na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Hii ni fursa nzuri ambayo haiwezi kupotezwa. Historia inawakumbusha kwamba: ufunguo wa utulivu wa kisiasa na kijamii ni kujua jinsi ya kutarajia na kujibu mahitaji ya jamii kupitia utekelezaji wa mageuzi ya taratibu ambayo yanaboresha maisha ya watu. Hivi ndivyo msemo wa zamani unavyofundisha: "Ili kuepuka mapinduzi, mageuzi ni muhimu." Ili yote haya yaweze kutokea ni muhimu kusikiliza na kujibu kwa umakini sauti za wananchi wote wa Msumbiji, hasa sauti za vijana, wanawake, na maskini zaidi na wasio na uwezo. Kanisa Takatifu daima linaunga mkono mazungumzo kama njia muhimu ya kufikia upatanisho, umoja na amani. Kwa nia ya mazungumzo jumuishi, Maaskofu wa Msumbiji wamechapisha kitabu kilichoelekezwa kwa jumuiya za Kikristo na watu wote wenye mapenzi mema: ili kuwatayarisha kushiriki kikamilifu, kwa uangalifu, na kuwajibika katika mchakato huu. Kama Maaskofu wanavyoonyesha, lengo ni kukuza ujenzi wa jamii yenye uadilifu zaidi, uaminifu, shirikishi na utu.

Kardinali Parolin akiwa Mjini Maputo, Msumbiji
Kardinali Parolin akiwa Mjini Maputo, Msumbiji   (AFP or licensors)

Inafaa kutaja kwa namna ya pekee kabisa Jimbo la Cabo Delgado, mwathirika wa ukosefu wa usalama, ghasia pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kugumisha mahusiano, watu kukimbia makazi yao pamoja na vifo vya maelfu ya watu, changamoto na wito kama ulivyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV ni kurejesha usalama na amani katika eneo hilo. Jimbo la Capo Delgado ni eneo ambalo limeharibiwa sana na chuki za kidini kati ya Waislam na Wakristo. Ukristo na Uislamu ni dini ambazo zimeishi Msumbiji kwa amani, maelewano na kuheshimiana. Misimamo mikali ya kidini na ugaidi si sehemu ya nafsi ya waamini wa dini za Msumbiji; wao ni aina za dini potovu na ngeni kwa utambulisho wa ndani kabisa wa watu wa Msumbiji, ambao ni watu wenye amani, furaha, na wakarimu. Katika hali hii ngumu, Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, wanaokaribiwa na hatari. Kardinali Parolin amesema, Kanisa Katoliki halitafuti upendeleo, bali linatamani kuweza kutekeleza utume wake wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ushirikiano na Serikali ya Msumbiji. Ili kuthamini utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa tarehe 7 Desemba 2011, Serikali ya Msumbiji na Baraza la Kitaifa ilitia saini “Makubaliano ya Kanuni na Masharti ya Kisheria” ambayo yanapaswa kudhibiti uhusiano wao na “kukuza ushirikiano wenye afya kati ya Msumbiji na Kanisa Katoliki, kwa kuheshimu uhuru wa kila upande katika nyanja yake.” Katika kipindi chote cha miaka kumi na minne ya uhalali, Mkataba huu umethibitisha manufaa na thamani yake. Sasa, wote wanataka kusonga mbele zaidi katika utekelezaji kamili wa Mkataba huo, kwa lengo la kuwezesha huduma ambayo majimbo, taasisi za kidini na wamisionari kwa ukarimu na kwa upendo wa Kikristo hutoa kwa watu wa Msumbiji, hasa maskini zaidi, watoto, wazee, wagonjwa na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Parolin Msumbiji
30 Desemba 2025, 14:42