Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake kwa Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2025 anasema Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani, Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake kwa Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2025 anasema Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani,   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV: Noeli ya Bwana Ni Noeli ya Amani

Papa Leo XIV anasema Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani, na hasa katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine: kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Umwilisho ni kitovu na chemchemi ya furaha, amani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwana wa Mungu aliyezaliwa mjini Bethlehemu ili kuvunjilia mbali nguvu za dhambi na mauti na hatimaye, kumrudishia tena mwanadamu utu na heshima yake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kristo Yesu anakuja kuwaletea waja wake amani na furaha ya kweli. Fumbo la Umwilisho ni tukio muhimu sana katika imani, tamaduni na sanaa ya Kikristo, kwani Neno wa Mungu amefanyika mwili na kuja kukaa kati ya waja wake. Noeli ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia amani, umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na furaha ya ujio wa Mwana wa Baba wa milele. Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake kwa Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2025 anasema Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani, na hasa katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine: kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Papa Leo XIV Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani
Papa Leo XIV Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani

Katika Siri ya Noeli anasema Baba Mtakatifu Leo XIV: "Mungu haoni aibu kwa unyenyekevu wa mwanadamu; anaingia ndani yake. […] Mungu anapenda kile kilichopotea, kinachopuuzwa, kisicho na maana, kilichotengwa, kilicho dhaifu, na kilichovunjika.” Mwenyezi Mungu apende kuwakirimia unyenyekevu huohuo, huruma yake ile ile, upendo wake, ili waweze kuwa ni wanafunzi na mashuhuda wa Kristo Yesu, kila siku ya maisha yao. Noeli ni sherehe ya watakatifu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu; ni furaha ya wazima wanaowajibika kuwatunza na kuwahudumia wagonjwa; ni sherehe ya matajiri wanaopaswa kuonesha huruma, upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha! Ni Sherehe ya waamini wanaopaswa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa njia matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na utu wema, ili wale wasio amini waweze kuvutika kwa kuona ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotolewa na Wakristo katika maisha na utume wao!

Noeli ni sherehe inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani
Noeli ni sherehe inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani   (@Vatican Media)

Noeli ni Sherehe inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani, moyo mnyofu na utu wema katika maisha, kwani Neno wa Mungu, Kristo Yesu amejinyenyekeza na kuzaliwa katika hali ya umaskini, changamoto kwa waamini kumtambua katika imani na kumpokea ili aweze kupata nafasi katika sakafu ya mioyo ya waamini. Mwanadamu mamboleo anayo mambo mengi ambayo yanakwamisha fursa ya kumtambua Kristo Yesu katika maisha! Hii inatokana na changamoto mbalimbali zinazojionesha katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, kazi na jamii katika ujumla wake. Watu wengi wamekengeuka, kiasi cha kuzama na kutopea katika uchu wa mali na madaraka. Hawa ni watu wanaoogopa kupoteza nafasi na utambulisho wao katika jamii kama ilivyokuwa kwa Mfalme Herode, kiongozi katili aliyetaka kumfutilia mbali Mtoto Yesu kwa kudhani kwamba, alitaka kumpora Ufalme wake hapa duniani!

Kwa ajili yetu, Mtoto amezaliwa
Kwa ajili yetu, Mtoto amezaliwa   (Vatican Media)

Noeli kiwe ni kipindi cha kutoa nafasi ya kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mafano wa Mungu; utimilifu wa furaha na amani ya kweli. Ni wakati wa kujikita katika ukweli na uwazi; uaminifu na udumifu katika mambo msingi; kwa kusamehe na kusahau; kwa kujenga na kudumisha urafiki na udugu wa kibinadamu; kwa kujadiliana katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Huyu ndiye Immanueli. Kila mtu anayo thamani, utu na heshima yake, mbele za Mwenyezi Mungu. Ukarimu kwa maskini ni njia ya kumkaribisha Kristo Yesu katika maisha, ili aweze kuwatembelea, kuzungumza na kuonja maisha yao, ili kuwaonesha upendo wake usiokuwa na mipaka! Ni wakati wa kumtengenezea Mwenyezi Mungu nafasi katika maisha, kwa njia ya upendo na mshikamano kwa jirani. Baba Mtakatifu Leo XIV, katika Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2025, majira ya Saa 4:00 kwa Saa za Ulaya anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, sawa na Saa 6:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Itakapogota Saa 6: 00 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 8: 00 Kwa Saa za Afrika Mashariki, Baba Mtakatifu Leo XIV atatoa Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi.”

Mkesha wa Noeli 2025
24 Desemba 2025, 14:56