Papa Leo XIV:Kukuza Elimu Bora ya Kikatoliki barani Afrika
Vatican News
Baba Mtakatifu Leo XIV akikutana na Wanachama wa Mfuko wa Kimataifa wa Dini na Vyama mjini Vatican tarehe 7 Novemba 2025 aliwatia moyo, siku chache tu baada ya sherehe ya Jubilei ya Elimu Ulimwenguni. Shirika hilo, Papa Leo XIV alisisitiza katika salamu yake kwa lugha ya Kifaransa, kuwa limejitolea "kukuza elimu bora ya Kikatoliki barani Afrika na kukuza ushirikiano bora wa kimisionari kati ya Kusini na Kaskazini." Pia liko wazi kwa changamoto mpya, kama vile Kongamano la pili litakalofanyika Nairobi, Kenya, katika majuma mawili yajayo, likizingatia mada: "Elimu ya Kikatoliki na Kukuza Ishara za Matumaini katika Muktadha wa Kiafrika."
Ushirikiano wa Kimisionari kati ya Kaskazini na Kusini
Papa Leo anathamini juhudi "za kutoa elimu bora, iliyojaa utambulisho wa Kiafrika, kama ilivyopendekezwa na Mkataba wa Elimu wa Kiafrika," ambao ni sehemu ya Mkataba wa Elimu wa Kimataifa, uliozinduliwa na Papa Francisko mnamo 2019 ili kufufua kujitolea kwa elimu iliyo wazi na jumuishi zaidi. Kisha akakumbuka mkutano na waelimishaji Oktoba 31 iliyopita. Leo hii katika mazingira yetu ya kielimu, inatia wasiwasi kuona dalili za udhaifu wa ndani ulioenea zikikua katika rika zote. Hatuwezi kufumbia macho vilio hivi vya kimya kimya vya kuomba msaada. Sio elimu tu, bali pia utume, na hasa, Papa alisisitiza, katika suala la Mfuko wa Kimataifa wa Dini na Jamii, ni "ushirikiano wa kimisionari kati ya Kaskazini na Kusini." Hakika, ni muhimu kutembea pamoja kutangaza Injili na muhimu vile vile kukuza ujumuishaji katika majimbo mahalia.
Utume inahitaji kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuepuka kutengwa
Utume unahitaji kufanya kazi kwa ushirikiano, kuepuka kutengwa, na kukubaliana kujenga mshikamano imara wa kichungaji, ambao hauzuiliwi na njia za kifedha tu bali pia unajumuisha ubadilishanaji wa wafanyakazi wa kichungaji kati ya Makanisa. Ushirikiano wa kimisionari, Papa anakumbuka, ulijadiliwa Mei iliyopita katika mkutano kwenye Monasteri ya Maredsous nchini Ubelgiji, tukio lililosababisha kuundwa kwa Kituo cha Kimataifa cha Umisionari na Uchungaji wa Kaskazini-Kusini. Ni matumaini ya Papa Leo XIV ni kwamba bidii ya kimisionari itagunduliwa tena, ikipendekeza Injili ya Yesu kwa ujasiri na upendo.
Papa alisema “Asanteni, ndugu wapendwa, kwa yote mnayofanya: kuwakumbusha kila mtu uzuri wa uinjilishaji. Tumwombe Bwana neema ya kuwa wanafunzi wa kimisionari na wachungaji kulingana na mapenzi yake. Awapatie msukumo wa mipango yenu na Roho Mtakatifu awasaidie katika kujitolea kwenu kuitumikia Injili.”
Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa unataka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida:cliccando qui
