Papa Leo XIV akutana na rais wa Timor Mashariki
Vatican News
Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 21 Novemba 2025 alikuta na Bwana José Manuel Ramos-Horta, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Timor-Leste,nchi ndogo ya Kusini-mashariki mwa Asia iliyotembelewa na Papa Francisko mnamo Septemba 2024 na ambayo makaribisho yake ya kuvutia kwa Papa huyo, yalikumbushwa wakati wa kukutana na Papa katika Jumba la Kitume mjini Vatican.
Mazungumzo ya Sekretarieti ya Vatican
Baada ya mkutano na Papa, Horta baadaye alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa. Katika taarifa kutoka Ofisi ya Habari ya Vatican ilisema, "Wakati wa majadiliano ya kirafiki katika Sekretarieti ya Vatican, uhusiano mzuri kati ya Vatican na Timor-Leste na mchango wa Kanisa Katoliki kwa jamii ya Timor ulisisitizwa. Kisha mkutano huo ulilenga vipengele fulani vya hali ya kiuchumi na kijamii ya nchi."
Katika kuendelea na mazungumzo, pia kulikuwa na kubadilishana maoni kuhusu hali ya kikanda, na kujiunga hivi karibuni kwa Timor- Mashariki na Chama cha Mataifa ya Kusini-mashariki mwa Asia (ASEAN) kulijadiliwa.
