Nia ya maombi ya Papa kwa Novemba 2025:“kwa ajili ya kuzuia kujiua”
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Nia ya maombi ya Sala ya kila mwezi ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwa mwezi Novemba 2025 ni "kwa ajili ya kuzuia kujiua." Katika maelezo yake kwa njia ya Video, Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Kanisa kuombea nia hiyo ambayo imekabidhiwa kwa Kanisa Katoliki Ulimwenguni kote kupitia Mtandao wa Maombi wa Papa Kimataifa.
Katika video hiyo imetengenezwa na kusambazwa na Mtandao wa Kimataifa kwa usaidizi Jimbo Katoliki la Phoenix, Arizona, nchini Marekani kwa ushirikiano na vyombo vya habari vya Vatican. Katika ujumbe na nia ya Papa kupitia video inaanza na maneno ya Baba Mtakatifu akiwaalika waamini kuungana naye katika kuomba kwamba "wale wanaopambana na mawazo ya kujiua wapate msaada, utunzaji, na upendo wanaohitaji katika jumuiya yao, na wawe wazi kwa uzuri wa maisha."
Kupambana na mawazo ya kujiua
Papa Leo XIV kwa njia hiyo anaanza sala yake kwa kumwomba Bwana, ambaye anawaalika waliochoka na wenye mizigo kuja kwake na kupata pumziko moyoni Mwake, kusindikizana na watu wote wanaoishi gizani na kukata tamaa, hasa wale wanaopambana na mawazo ya kujiua, ili wa wapate daima, jumuiya inayowakaribisha, kuwasikiliza, na kuwasindikiza,” ameomba Baba Mtakatifu. Papa akiendelea anabainisha kuwa "Na tujue, jinsi ya kuwa karibu kwa heshima na upole, kusaidia kuponya majeraha, kujenga vifungo, na kufungua upeo."Katika muktadha huo Papa aliomba kuwa "kwa pamoja tugundue tena kwamba maisha ni zawadi, kwamba bado kuna uzuri na maana, hata katikati ya maumivu na mateso."
Tuhisi upendo na ukaribu wako
Baba Mtakatifu pia alikiri wazi kwamba kufika mahali penye giza kama hilo kunaweza kumgusa mtu yeyote, akionesha kwamba hata wale wanaomfuata Yesu wako hatarini kwa huzuni bila tumaini. Baba Mtakatifu alihimisha kwa kuomba, kwamba: “tunakuomba utufanye kila wakati tuhisi upendo Wako ili, kupitia ukaribu Wako kwetu, tuweze kutambua na kutangaza kwa wote upendo usio na kikomo wa Baba anayetuongoza kwa mkono ili kufufua imani yetu katika maisha Unayotupa. Amina."
Mtandao wa Kimataifa wa Maombi ya Papa ulianzishwa 2016
Video ya Baba Mtakatifu ni mpango rasmi wa Kimataifa wenye lengo la kusambaza nia za maombi sala ya kila mwezi ya Baba Mtakatifu inayoandaliwa na Mtandao wa Maombi wa Papa Ulimwenguni (Utume wa Maombi). Tangu 2016, Video ya Papa imetazamwa zaidi ya mara milioni 247 katika mitandao yote ya kijamii ya Vatican, na imetafsiriwa katika lugha zaidi ya 23, ikipata habari kwa vyombo vya habari katika nchi 114. Video hii, iliyotayarishwa na timu ya Mtandao wa Maombi ya Video ya Papa, iliyoratibiwa na Andrea Sarubbi, na kuundwa kwa msaada wa Coronation Media, inasambazwa kwa msaada wa shirika la 'Machi' na ushirikiano wa Vatican Media.
Mtandao wa Maombi ya Papa Ulimwenguni aidha ni Jumuiya ya Kipapa, yenye dhamira ya kuwahamasisha Wakatoliki kupitia sala na vitendo ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanadamu na dhamira ya Kanisa. Kulingana na Shirika la Afya Duniani, karibu watu elfu 720 hujiua kila mwaka. Zaidi ya nusu ya vifo vyote hutokea kabla ya umri wa miaka 50.
