Tafuta

2025.10.31: Wajumbe wa Baraza la Kimataifa la Ushauri wa Vijana 2025.10.31: Wajumbe wa Baraza la Kimataifa la Ushauri wa Vijana  (@VATICAN MEDIA)

Papa kwa vijana:Katika Kanisa tunataka kusikiliza vijana na kukaribisha karama na vipaji vyao!

Papa Leo XIV akizungumza kwa Kiingereza na wajumbe wa Baraza la Kimataifa la Ushauri wa Vijana,Oktoba 31 aliwalezea vijana kuwa katika enzi ya mitandao ya kijamii,wasiishi imani yao kwa upweke na hivyo aliwahimiza kuzingatia mada tatu sinodi,utume na ushiriki ili kukabiliana na upweke na kusaidia Kanisa kuwafikia wale wanaohitaji."Lazima muwe na mioyo iliyo wazi kwa wito wa Mungu na isiyojishughulisha na mipango iliyo tayri tayari kuelewa na kuhurumia.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV siku ya Ijumaa tarehe 31 Oktoba 2025 alitoa hotuba yake kwa wajumbe wa Baraza la Kimataifa la Ushauri wa Vijana(IYAB), chombo kinachohusiana na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambacho kinalenga kuleta mtazamo wa vijana katika Kiti Kitakatifu kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa ajili ya utume wa Kanisa. Kikundi hiki cha vijana (IYAB), tangu Jumanne 27 Oktoba, kimekuwa na mkutano jijini Roma kutafakari mada zinazowaathiri vijana Wakatoliki, huku mada tatu za sinodi, utume, na ushiriki zikiwa ndio kiini cha majadiliano yao.

Papa na wajumbe washauri wa vijana
Papa na wajumbe washauri wa vijana   (@VATICAN MEDIA)

Papa alianza kusema kuwa "Wapendwa vijana, habari za asubuhi na karibu! Mmealikwa kuwa sehemu ya Baraza la Kimataifa la Ushauri kwa Vijana (IYAB). Ikiunganishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, Baraza hili linalenga kuwafahamisha Watakatifu "mtazamo wa vijana" kuhusu masuala mbalimbali ambayo yako katikati ya utume wa Kanisa. Papa aliwakushukuru kwa nia yao, na kwa juhudi zao za siku chache zilizopita za kushiriki katika mazungumzo na majadiliano kwa nia ya kutoa mchango wao kwa washirika wa Papa katika Baraza la Wawakilishi la Curia Romana. Kwa nnia hiyo Baba Mtakatifu alipendelea kushirikishana na tafakari tatu fupi kuhusu ushiriki, sinodi na utume."

Ushiriki

Ili kutekeleza kazi yao, wanaitwa, zaidi ya yote, kutambua kwamba wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Kama wanavyojua vyema, huu ni utume wa ulimwengu wote, ikimaanisha kwamba unaelekezwa kwa wanaume na wanawake wote, kutoka kila sehemu ya dunia na kutoka kila utamaduni na hali ya kijamii. Ushiriki halisi wa Kanisa unatoka wapi?" Papa aliuliza na kujibu kuwa: “Ningesema kwamba unatokana na kuwa karibu na Moyo wa Kristo. Asili yake, basi, ni ya kiroho, si ya kiitikadi au kisiasa.” Papa alibainisha tena kuwa “Muda mfupi kabla ya kifo chake, Yesu alimwomba Baba, kama ilivyosimuliwa katika Injili ya Yohane kwa maneno haya: “Siwaombei hawa tu, bali pia na wale watakaoniamini kwa neno lao, ili wote wawe na umoja” (Yh 17:20-21).

Yesu havutiwi na kundi dogo la wanafunzi walio mbele yake tu; anatazama mbali zaidi. Mawazo yake yanawageukia watu wote, wakiwemo wale walio mbali na wale watakaokuja baadaye. Angependa kila mtu awe wazi kwa ujumbe wa wokovu ambao wanafunzi wake wata upeleka, na kila mtu agundue ndani yake umoja wa imani na upendo wa pande zote. Kwa neno moja, Papa aliongeza “Bwana hubeba ulimwengu wote moyoni mwake kila wakati. Hii ndiyo chanzo cha ushiriki. Wale walio karibu na Yesu, ambao huwa marafiki zake kupitia sala, Sakramenti na maisha ya kila siku, wanaanza kuhisi kama anavyohisi.

Wajumbe washauri wa vijana
Wajumbe washauri wa vijana   (@VATICAN MEDIA)

Wanaanza kubeba ulimwengu wote mioyoni mwao: hakuna kitu kigeni kwao na hakuna mtu asiyejali kwao.” Wanajali, na kuguswa na mateso ya wengine, mahitaji na matarajio yao. Hii husababisha hamu ya kushiriki, kuwa sehemu ya utume wa Kanisa kwa wote, ambao unaelekezwa kwa kila mtu.” Kuhusika huku pia ni ishara ya ukomavu wa kibinadamu na kiroho. Ingawa watoto wanajali tu mahitaji yao wenyewe, watu wazima wanajua jinsi ya kushiriki matatizo ya wengine na kuyafanya yao wenyewe. Pia wameitwa katika ukomavu huu na wanaalikwa "kuzama" katika Kristo, ili wapate kuhisi kama anavyohisi na kuona kama wanavyoona. Kwa namna fulani, wanavutiwa na matumaini, ndoto na magumu ya vijana, ya vijana wote wa wakati wetu. Papa aliwasihi watazame  kwa huruma ile ile ya Kristo na kujaribu kufikiria jinsi ambavyo Kanisa, lililoongozwa na imani, linavyoweza kwenda kukutana nao.

Sinodi

Kipengele cha pili ni sinodi. Papa alisema kuwa “mnajua kwamba sinodi ni mojawapo ya njia za kutekeleza asili ya Kanisa kama ushirika. Katika mfano wa Utatu Mtakatifu, Kanisa pia ni ushirika wa watu, wa waamini wa kila kizazi, lugha na taifa, wanaosafiri pamoja, wakitajirishana na kushiriki vipawa vyao vya kiroho.” Kwa hivyo, “katika Kanisa la kisinodi, tunataka kusikiliza kile ambacho Roho Mtakatifu anawaambia vijana; tunataka kukaribisha karama zao, vipawa ambavyo ni maalum kwa umri wao na hisia zao.”

Vijana, katika Kanisa la Sinodi, pia wanaitwa kuzungumza kwa niaba ya wenzao. Kupitia ninyi, tunataka kusikia sauti za wanyonge, maskini na wapweke, wakimbizi na wale wanaojitahidi kujumuika katika jamii, au kupata fursa za kielimu. Mara nyingi, sauti hizi huzimwa na kelele za wenye nguvu, waliofanikiwa na wale wanaoishi katika hali halisi "pekee.” Wakati huo huo, kwa vijana, Kanisa la Sinodi pia ni changamoto, kichocheo tunaweza kusema, kwani linawatia moyo kutoishi imani yao peke yao.

Papa Leo alisema kwamba wao wanajua kwamba katika miaka ya hivi karibuni vijana wengi wamekaribia imani kupitia mitandao ya kijamii, programu zilizofanikiwa na mashahidi maarufu wa Kikristo mtandaoni. Hatari ni kwamba imani inayopatikana mtandaoni ina mipaka ya uzoefu wa mtu binafsi, ambao unaweza kuwa wa kutia moyo kiakili na kihisia, lakini kamwe "haujumuishwi." Uzoefu kama huo hubaki "usio na mwili," umetengwa na "mwili wa Kanisa." Wala hauishi pamoja na wengine katika hali halisi za maisha, mahusiano au kushiriki. Mara nyingi, mashine  za mitandao ya kijamii huunda ubao wa kusikilizwa tu kwa watu binafsi, ukizingatia mapendeleo na ladha za kibinafsi, na "kuzirudisha" zikiwa zimekuzwa na kutajirishwa na mapendekezo ya kuvutia.

Hata hivyo, kila mtu hubaki peke yake na yeye mwenyewe, wafungwa wa mielekeo na makadirio yake mwenyewe. Kwa maana hiyo, uzoefu wa sinodi iliyo hai hushinda vikwazo vya nafsi na kuwatia moyo vijana kuwa wanachama wenye ufanisi wa familia ya Yesu Kristo. Zinaturuhusu "kuishi imani pamoja na kuonesha upendo wetu kwa kuishi katika jumuiya na kushiriki na vijana wengine upendo wetu, muda wetu, imani yetu na matatizo yetu.” Papa alisisitiza kwamba “Kanisa linatoa uwezekano mwingi tofauti wa kuishi imani yetu katika jumuiya, kwani kila kitu ni rahisi zaidi tunapofanya pamoja" (Wosia wa Kitume Baada ya Sinodi Christus Vivit, 164).

Utume

Kipengele cha mwisho ni utume.  Ambapo Papa alisema kuwa “Sinodi halisi husababisha utume. Hakika, kitendo cha Roho Mtakatifu ndicho kiini cha sinodi. Sio suala la sheria zinazoongoza mikutano. Badala yake, ni kuhusu kutoa nafasi kwa kitendo cha Mungu kwa kumsikiliza Roho.” Roho Mtakatifu hutafuta kutuongoza katika kweli yote (taz. Yh 16:13), ili tuweze kumkaribisha Yesu kwa undani zaidi, ambaye ni Kweli. Roho anatukumbusha kila kitu ambacho Yesu ametuambia (taz. Yh14:26), na hufanya maneno yake yawe muhimu leo. Kwa hivyo, Roho anatuongoza kuelekea utume. Papa alsisitiza kwamba pia wao watapata fursa ya kupata uzoefu wa jinsi maombi ya kawaida, kusikiliza na majadiliano yanavyoweza kuwasaidia kuelewa jinsi ya kuifanya Injili ionekane katika ulimwengu wa leo.

Papa na washauri wa vijana
Papa na washauri wa vijana   (@VATICAN MEDIA)

Hakika, utambuzi wa kikanisa kwa ajili ya utume unamaanisha kuelewa, katika kila kizazi, jinsi ya kupeleka Injili kwa kila mtu. “Yote haya yanahitaji kwamba ninyi, vijana, muwe na mioyo iliyo wazi, tayari kusikiliza "miongozo" ya Roho na "matamanio" ya kina ya kila mtu. Lazima mtazame zaidi ya mwonekano ili kutafuta majibu ya kweli yanayotoa maana kwa maisha.” “Lazima muwe na mioyo iliyo wazi kwa wito wa Mungu”, Papa alisisitiza  na “isiyojishughulisha na mipango yenu wenyewe, na ambayo iko tayari kuelewa na kuhurumia kabla ya kutoa hukumu. Dhana ya utume pia inahusisha uhuru dhidi ya  hofu, kwa sababu Bwana anapenda kutuita katika kutubu na kufuata njia mpya. Kwa maana hii, kama vijana, mnaweza kuwa viongozi wa ubunifu na ujasiri.”

Kwa kuhitimisha Papa aliwashukuru kwa  mchango watakaoutoa kwa utume, ambao watatoa nguvu mpya na kasi kwa moyo wa kimisionari wa Kanisa. Kiukweli, shirika lao ni sehemu ya harakati hiyo pana ya kiroho ambayo inajumuisha Siku ya Vijana Duniani, huduma ya kawaida ya vijana na harakati mpya za vijana, na ambayo huweka Kanisa kuwa changa milele.Wapendwa vijana, mnawakilisha wengi wa wenzenu, na kupitia kwenu, wanaweza pia "kuzungumza" na Kanisa.” Na kwa hiyo “hakikisheni kwamba sauti yenu inasikika na inachukuliwa kwa uzito. Uwepo wenu na mchango wenu  ni muhimu sana. Roho Mtakatifu awaongoze, awaangazie na awaimarishe katika furaha ya ushuhuda wa Kikristo.” Papa alimalizia kwa baraza zake za kipapa kwao.

31 Oktoba 2025, 19:24