Tafuta

Mwaka 2025, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka 160 tangu Kardinali Rafael Merry del Val alipozaliwa. Mwaka 2025, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka 160 tangu Kardinali Rafael Merry del Val alipozaliwa.  (ANSA)

Kardinali Rafael Merry Del Val: Mwanadiplomasia Mahiri wa Kanisa: Miaka 160 ya Kuzaliwa

Mwaka 2025, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka 160 tangu Kardinali Rafael Merry del Val alipozaliwa. Huyu ni Mwanadiplomasia mahiri wa Kanisa, aliyelihudumia Kanisa katika ulimwengu uliokuwa umesheheni changamoto mbalimbali; akaonesha: Ukomavu na umahiri; Uaminifu na busara. Akajisadaka kufundisha Katekesi kwa vijana wa Roma, miongoni mwao akatambulikana kuwa ni Padre aliyekuwa karibu sana na vijana wa kizazi kipya kama Baba na Rafiki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Kardinali Rafael Merry del Val alikuwa mtu maarufu sana katika uongozi wa Kanisa Katoliki, akihudumu kama Katibu Mkuu wa Vatican chini ya uongozi wa Papa Pio X na pia akishikilia cheo cha Kardinali- Padre. Aliteuliwa katika majukumu haya kunako mwaka wa 1903-1914, na kumfanya kuwa mmoja wa Makadinali wa kwanza wa uongozi wa Papa Pio X. Tarehe 21 Oktoba 1899 aliteuliwa kuwa Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa “Pontificia Accademia Ecclesiastica, PAE”, leo imetimia miaka 325 tangu kuanzishwa wake. Tarehe 19 Aprili 1900 aliteuliwa kuwa Askofu mkuu na tarehe 12 Novemba 1903 akateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Vatican, Utume alioutekeleza kwa ari na moyo mkuu; kwa uaminifu na ukarimu.

Kumbukizi ya Miaka 160 tangu azaliwe Kardinali Rafael Merry Del Val
Kumbukizi ya Miaka 160 tangu azaliwe Kardinali Rafael Merry Del Val   (@Vatican Media)

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Rafael Merry del Val alizaliwa tarehe 10 Oktoba 1865. Baada ya majiundo na masomo yake ya Kikasisi, tarehe 30 Desemba 1888 akapewa Daraja takatifu ya Kipadre. Akafariki dunia tarehe 26 Februari 1930 na mwaka 2025, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka 160 tangu Kardinali Rafael Merry del Val alipozaliwa. Huyu ni Mwanadiplomasia mahiri wa Kanisa, aliyelihudumia Kanisa katika ulimwengu uliokuwa umesheheni changamoto mbalimbali; akaonesha: Ukomavu na umahiri; Uaminifu na busara. Akajisadaka kufundisha Katekesi kwa vijana wa Roma, miongoni mwao akatambulikana kuwa ni Padre aliyekuwa karibu sana na vijana wa kizazi kipya kama Baba na Rafiki.

Kardinali Rafael Merry del Val alikuwa ni mwanadiplomasia mahiri
Kardinali Rafael Merry del Val alikuwa ni mwanadiplomasia mahiri   (@Vatican Media)

Akatangaza na kushuhudia kwamba kwa hakika alikuwa mwandiplomasia na mchungaji; akaunganisha huduma ya Kanisa na huduma ya walimwengu; akawa ni mfano bora wa “Litania ya Unyenyekevu; Uaminifu katika ukimya na kujiaminisha kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake, kiasi cha kuwa mshiriki wa karibu wa Papa Benedikto XV na Leo XIII na hivyo kuuachia ukweli useme; Alikuwa ni mtulivu katika maisha na utume wake, akawa ni mwaminifu wa Injili; mtu huru ambaye hakumezwa na malimwengu kwani alijishikamanisha na Kristo Yesu. Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 13 Oktoba 2025 kwa wajumbe waliokuwa wanashiriki katika mkutano kuhusu Hayati Kardinali Rafael Merry del Val. Kwa hakika alikuwa ni mtu huru na alijitahidi kutafuta na kuishi utakatifu kama kielelezo cha maisha; kwa kujikita katika umoja, huku wakitembea kumwendea Kristo Yesu mintarafu Neno la Mungu: Umoja na ushirika ni ngugo msingi katika diplomasia ya Kanisa. Kila mtu ameitwa kuwa ni Mtakatifu kadiri ya hali na mazingira yake.

Kardinali Rafael Merry Del Val alikuwa huru
Kardinali Rafael Merry Del Val alikuwa huru   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema; kumbukizi ya mwanadiplomasia wa kweli wa falsafa ya kukutana, iwe chanzo cha moyo wa shukrani kubwa na msukumo kwa wote, lakini haswa kwa wale wanaoshirikiana na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika ujenzi wa diplomasia ya Kanisa. Bikira Maria, ambaye Kardinali Rafael Merry del Val alimpenda kwa huruma ya kimwana, afundishe familia, wanadiplomasia wa Kiti kitakatifu, na wale wote wanaofanya huduma katika Kanisa, kuunganisha ukweli na upendo, busara na ujasiri, huduma na unyenyekevu, ili Kristo Yesu peke yake aangaze na kung’ara katika mambo yote.

Diplomasia ya Kanisa
13 Oktoba 2025, 15:32