Tafuta

2025.09.17:Washiriki wa Kongamano la VIII la Viongozi wa Dini za Ulimwengu na Jadi huko Astana 2025.09.17:Washiriki wa Kongamano la VIII la Viongozi wa Dini za Ulimwengu na Jadi huko Astana 

Papa Leo XIV kwa viongozi wa kidini:tupaze sauti moja kwa ajili ya hadhi ya binadamu!

Katika ujumbe wake kwa washiriki katika Kongamano la VIII huko Astana,Kazakhstan,kuanzia Septemba 17 hadi 18,Papa Leo XIV anakumbusha kwamba wakati viongozi wa imani tofauti wanaposimama pamoja katika kutetea walio hatarini zaidi,makao yetu ya kawaida ya pamoja na hadhi ya watu wote,wanashuhudia ukweli kwamba imani inaunganisha zaidi kuliko inavyogawanya.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alituma ujumbe wake, Jumatano tarehe 17 Septemba 2025 kwa lugha ya Kiingereza, kwa viongozi wa dini za Ulimwengu na za kijadi waliokusanyika kuanzia Jumatatano tarehe 17, hadi 18 Septemba 2025 huko Astana, Kazakhstan kwa ajili ya Kongamano la VIII. Katika ujumbe huo anasisitizia kutengenza mshikamano wa kweli kwa ajili ya amani, bila silaha na kupokonya silaha, kuwa wanyenyekevu na wavumilivu, ambao wako tayari daima kutoa upendo na karibu na wale wanaoteseka. Hili ni tukio ambalo lilimuona hata ushiriki wa Papa Francisko kunako mwaka 2022. Ujumbe wa Baba Mtakatifu anaanza: “Ninatuma salamu za dhati kwa wale wote wanaoshiriki katika Kongamano la 8 la Viongozi wa Dini za Ulimwengu na Kijani,” lililoitishwa huko Astana kwa kauli mbiu: “Mazungumzo ya Dini: Harambee kwa Wakati Ujao.” Na zaidi Papa alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Kassym-Jomart Tokayev, Rais wa Jamhuri ya Kazakhstan.

Kufanya urafiki na kuupyaisha

Papa Leo XIV, katatika ujumbe huo  alisema kwamba wamekusanyika “kutoka kila kona ya dunia ili kupyaisha urafiki na kutengeneza urafiki mpya, kiwa tumeungana katika nia yetu ya pamoja ya kuleta uponyaji katika ulimwengu wetu uliovunjika na kujeruhiwa. Mandhari haya yanafaa hasa, yakisisitiza jukumu muhimu la mazungumzo baina ya dini katika enzi iliyoangaziwa na migogoro mikali.” Papa alisema kKatika moyo  wa “kimkakati, ” una maana ya kufanya kazi pamoja wote kwa ajili ya mtu mwingine na pamoja na Mungu. Kila msukumo halisi wa kidini hustawisha mazungumzo na ushirikiano, unaokitwa katika ufahamu wetu wa ndani wa kutegemeana ambao huunganisha watu binafsi na mataifa.

Kwa mtazamo huo, kufanya kazi pamoja kwa maelewano si chaguo la kimatendo tu, bali ni onesho la mpangilio wa kina wa ukweli.  Shughuli hiyo inapatana na muundo wa maisha yetu ya pamoja kama washiriki wa familia moja ya kibinadamu. “Katika kina cha dhamiri yetu, ufahamu huu unaleta hisia ya kina ya mshikamano, imani kwamba tunawajibika kwa kila mmoja(taz.Yohane Paulo II, Sollicitudo Rei Socialis, 30 Desemba 1987, 38). Mshikamano, basi, ni harambee katika vitendo: usemi hai wa kumpenda jirani zetu kama sisi kwa kiwango cha kimataifa. Ushirikiano kama huo si mwito wa kufuta tofauti, bali ni mwaliko wa kukumbatia utofauti kama chanzo cha utajiri wa pande zote. Kanisa Katoliki, kwa upande wake, linakubali na kuthamini yote ambayo ni "kweli na takatifu" katika dini nyingine(Nostra Aetate, 28 Oktoba 1965, 2).

Kanisa linatafuta kukuza umoja na kuleta karama za kila tamaduni katika meza ya kukutana

Kwa hakika, linatafuta kukuza umoja wa kweli kwa kuleta karama tofauti za kila mila na tamaduni  kwenye meza ya kukutana, ambapo kila imani inachangia hekima yake ya kipekee na huruma katika huduma ya manufaa ya wote. Katika jitihada hii, "harambee kwa ajili ya siku zijazo" si kauli mbiu ya kufikirika bali ni ukweli hai ambao tayari umezaa matunda. Mkutano wa kihistoria wa viongozi wa kidini kwa ajili ya maombi huko Assisi mwaka 1986, ulioitishwa na Papa Yohane Paul II, ulionesha kwamba hakuwezi kuwa na amani kati ya mataifa bila amani kati ya dini. Hivi karibu zaidi, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Amani ya Ulimwengu na Kuishi Pamoja, iliyotiwa saini huko Abu Dhabi mnamo 2019 na mtangulizi wake, mtukufu Papa Francisko na Imamu Mkuu wa Al-Azhar, Ahmad Al-Tayyeb, Papa Leo XIV alisisitiza kwamba ilitoa mwongozo wazi wa jinsi harambee ya kidini inaweza kuendeleza amani na kuishi pamoja duniani. “Tulishuhudia roho hiyohiyo katika mkutano wa mwisho wa Kongamano hili mwaka wa 2022, ambapo viongozi wa imani mbalimbali, akiwemo Papa Francisko walikutana pamoja kulaani ghasia na itikadi kali, kutetea utunzaji wa wakimbizi, na kutoa wito kwa viongozi wote kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya amani.

Kardinali Koovacad alishiriki Mkutano wa Dini huko Astana
Kardinali Koovacad alishiriki Mkutano wa Dini huko Astana

Mustakabali wa amani, udugu na mshikamano unahitaji kujitolea

Papa alikazia  kusema kuwa ahadi hizi za hali ya juu zinaakisiwa katika hatua madhubuti: wakati majanga ya asili yanapotokea, wakati wakimbizi wanalazimika kukimbia, au wakati familia zinateseka kutokana na umaskini uliokithiri na njaa, jumuiya za imani mara nyingi huungana, zikifanya kazi bega kwa bega kuleta unafuu na matumaini kwa wale wanaohitaji zaidi. Wakati ujao tunaotazamia,  mustakabali wa amani, udugu na mshikamano,  unahitaji kujitolea kwa mikono yote na mioyo yote. Viongozi wa kidini wanaposimama pamoja kutetea watu walio hatarini zaidi katika jamii, kujiunga katika kupanda miti ili kutunza makao yetu ya kawaida ya pamoja, au kupaza sauti ya umoja kuunga mkono hadhi ya kibinadamu, wanashuhudia ukweli kwamba “imani huunganisha zaidi kuliko inavyogawanya.” Kwa njia hii, Papa alisisitiza kwamba “harambee inakuwa ishara yenye nguvu ya matumaini kwa wanadamu wote, ikidhihirisha kwamba dini, katika kiini chake, si chanzo cha migogoro bali ni kisima cha uponyaji na upatanisho.

Tusali bega kwa bega na tuseme kwa sauti moja popote ambapo hadhi ya mwanadamu iko hatarini

Kwa hisia hizi, Papa anaamini kwamba “kazi ya Kongamano hilo litatutia moyo kufanya kazi bila kuchoka kwa maelewano, kuunda harambee kwa ajili ya amani, ambayo, kama nilivyosema hapo awali,  kuwa haina silaha na inapokonya silaha, nyenyekevu na vumilivu," daima kutafuta upendo na kuwa karibu na wale wanaoteseka (Urbi et Orbi, 8 Mei 2025).” Kwa kuhitimisha Papa alisema “Tusali bega kwa bega, tutumikie bega kwa bega, na tuseme kwa sauti moja popote pale ambapo hadhi ya mwanadamu iko hatarini. Mwenyezi abariki juhudi zetu na alete matunda tele kwa manufaa ya watu wote.”

17 Septemba 2025, 09:53