Papa amteua Balozi mpya wa Iraq,Monsinyo Wachowski
Vatican News
Baba Mtakatifu Leo XIV alimteua tarehe 18 Septemba 2025, Monsinyo Mirosław Stanisław Wachowski, ambaye hadi uteuzi wake alikuwa ni Katibu Msaidizi wa Mahusiano na Mataifa, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Iraq, na wakati huo huo akimpandisha hadi kwenye kiti cha heshima cha Villamagna di Proconsolare, akiwa na hadhi ya Askofu Mkuu. Tangazo la uteuzi huo limetolewa asubuhi ya Alhamisi na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa, na Mashirikia ya Kimataifa mbele ya wahusika wa kitengo cha tatu cha Sekretarieti ya Vatican.
Alizaliwa wa Pisz, Poland, tarehe 8 Mei 1970. Monsinyo Wachowski alipewa Daraja Takatifu la Upadre mnamo 15 Juni 1996, kwa ajili ya Jimbo la Ełk. Ana shahada ya Sheria ya Kanoni.
Aliingia katika huduma ya kidiplomasia ya Kiti Kitakatifu, tarehe 1 Julai 2004 na kuhudumu katika Uwakilishi wa Kipapa nchini Senegal, Utume wa Kudumu kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya(OSCE); Ofisi ya Umoja wa Mataifa na Mashirika Maalum huko Vienna, Ofisi ya Ubalozi wa Vatican huko Poland, na hivi karibuni katika Kitengo cha Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa ya Sekretarieti ya Vatican. Aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Mahusiano na Mataifa mnamo tarehe 24 Oktoba 24. Anajua kuzungumza Kiitaliano, Kiingereza, Kifaransa, Kihispania na Kirusi kwa ufasaha.
