Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watafakari kuhusu Fumbo la Kifo kama Kristo Yesu alipomlilia rafiki yake Lazaro, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Rej Yn 11:35. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watafakari kuhusu Fumbo la Kifo kama Kristo Yesu alipomlilia rafiki yake Lazaro, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Rej Yn 11:35.   (AFP or licensors)

Papa Leo XIV Kumbukizi ya Miaka 5 ya Mlipuko wa Bandari ya Beirut, Lebanon

Papa Leo XIV anawaalika watafakari kuhusu Fumbo la Kifo kama Kristo Yesu alipomlilia rafiki yake Lazaro, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Rej Yn 11:35. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon, kuunganisha machozi yao na yale ya Kristo Yesu, kama kielelezo cha majonzi makubwa. Kristo Yesu yuko karibu na kila mmoja wao anasema Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe uliondikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Miaka mitano imegota tangu mlipuko mkubwa ulipotokea kwenye Bandari ya Beirut nchini Lebanon na hivyo kusababisha watu zaidi ya 2,000 kupoteza maisha, watu 6, 500 kujeruhiwa vibaya sana pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na hii ilikuwa ni tarehe 4 Agosti 2020. Taarifa za awali zilionesha kwamba chanzo ni kulipuka kwa “Ammonium Nitrate” Tani 2750 iliyokuwa imehifadhiwa bandarini hapo. Watu wa Mungu nchini Lebanon wanataka kuona haki na ukweli vikitamalaki, ili kuwepo na uwajibikaji katika dhana ya ukweli na uwazi. Watu wa Mungu nchini Lebanon anaendelea kuombea amani nchini mwao na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Lebanon inapaswa kuendelea kuwa ni sehemu ya mradi wa amani, mahali ambapo jumuiya za watu mbalimbali zinaishi kwa pamoja katika amani na utulivu; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Kanisa nchini Lebanon liko bega kwa bega pamoja na wale wote wanaoteseka kwa kuondokewa na wapendwa wao. Kamwe watu wa Mungu nchini Lebanon wasijisikie wapweke kwani Kanisa litaendelea kuwaonesha mshikamano, kwa njia ya sala na Injili ya upendo katika uhalisia wa maisha yao. Wawe na imani, matumaini na ustawi kama Mwerezi wa Lebanon, utambulisho wa nchi ya Lebanon, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kuinua nyuso zao juu mbinguni kwa Mwenyezi Mungu ambaye kimsingi ni chemchemi ya matumaini ambayo kamwe hayamdanganyi mtu.

Kumbukizi ya Miaka 5 ya Mlipuko wa Bandari ya Beirut, Lebanon
Kumbukizi ya Miaka 5 ya Mlipuko wa Bandari ya Beirut, Lebanon

Bikira Maria wa Harissa, aendelee kuwaangalia wananchi wa Lebanon kwa macho yake yenye huruma. Ni katika muktadha wa Mkesha wa kumbukizi ya miaka mitano tangu mlipuko mkubwa utokee kwenye Bandari ya Beirut, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Lebanon uwepo wake wa karibu kiroho na kwamba, anaungana nao kwa njia ya sala, ili kuwakumbuka na kuwaombea wahanga wa mlipuko huo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watafakari kuhusu Fumbo la Kifo kama Kristo Yesu alipomlilia rafiki yake Lazaro, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Rej Yn 11:35. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon, kuunganisha machozi yao na yale ya Kristo Yesu, kama kielelezo cha majonzi makubwa. Kristo Yesu yuko karibu na kila mmoja wao anasema Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe uliondikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Kristo Yesu akamwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya maisha, akamfufua ili kuwapatia waja wake alama hai, chemchemi ya matumaini ya Kikristo katika maisha na uzima wa milele na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiini cha uhai wa mwanadamu na wala kifo hakina neno la mwisho. Martha alimlilia ndugu yake Lazaro, lakini Kristo Yesu alimfariji kwa kumkumbusha kwamba; “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? Yn 11:25-26.

Kanisa liko bega kwa bega na watu wa Mungu Lebanon
Kanisa liko bega kwa bega na watu wa Mungu Lebanon   (AFP or licensors)

Mbele ya Fumbo la kifo, mwanadamu anakuwa kama anatembea katika giza nene, na ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anawakirimia waja wake mwanga wa imani, chemchemi ya matumaini mbele ya Fumbo la kifo. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini amefunguliwa mlango wa kwenda nyumbani mwa Baba wa milele, anayewaongoja waja wake. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watu wa Mungu nchini Lebanon kuhisi uwepo wake na wa Kanisa zima zima. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwapokea wale wote waliopoteza maisha kutokana na mlipuko wa Bandari ya Lebanon. Baba Mtakatifu Leo XVI anapenda kuwa ni faraja, kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo na kwamba, Lebanon itaendelea kuchukua nafasi ya pekee katika maisha na sala zake. Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa ambao wameendelea kuwa karibu na waathirika wa janga hili. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mtakatifu Charbel pamoja na watakatifu wote wa Lebanon na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Mlipuko wa Bandari ya Beirut: Ukweli, Uwazi na Uwajibikaji
Mlipuko wa Bandari ya Beirut: Ukweli, Uwazi na Uwajibikaji

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1991, Mtakatifu Yohane Paulo II aliitisha Siku Maalum ya Sala kwa ajili ya Lebanon na baadaye mwaka 1995 yakafuatia maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Viongozi hawa kwa mwaka 2021 wakasali na kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie watoto wake wa Lebanon amani ya kudumu. Viongozi hawa wakawasha Mshumaa wa matumaini kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Baadaye Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wageni wake wakashiriki kwenye vipindi vitatu vya majadiliano ya faragha. Baadaye, majira ya jioni, kwa pamoja wakaadhimisha Liturujia ya Kiekumene iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Watu wa Mungu nchini Lebanon alioutoa wakati wa Liturujia ya Kiekumene tarehe 2 Julai 2021 kwa ajili ya kuombea amani; aliomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kwa niaba ya viongozi wa Makanisa walioshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Mlipuko wa Bandari ya Beirut: Mshikamano wa udugu wa kibinadamu
Mlipuko wa Bandari ya Beirut: Mshikamano wa udugu wa kibinadamu   (ANSA)

Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani. Ni wito wa Lebanon kuwa ni nchi inayokita mizizi yake katika uzoefu wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kuzamisha mizizi yao katika ndoto ya amani, tayari kung’arisha mwanga wa matumaini. Anasema, kamwe wasichoke kumlilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ili aweze kuwakirimia waja wake amani ya kudumu. Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ujumbe unaosikika kwa wakati huu kutoka Mashariki ya Kati ni amani na udugu wa kibinadamu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon na huu ni mradi unaopaswa kudumu katika amani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kumezwa na malimwengu. Wito wa Lebanon unapaswa kuwa ni nchi ya maridhiano na ya watu wengi, chemchemi ya udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi wa kisiasa walioko madarakani, wanapaswa kujizatiti zaidi kutafuta na kudumisha amani ya kweli na kamwe wasitafute masilahi yao binafsi. Na kamwe watu wachache wasiendelee kufaidika kwa mateso na mahangaiko ya wananchi wa Lebanon na kwamba, watu wanataka kusikia ukweli wote kuhusu hatima ya maisha yao. Lebanon na Mashariki ya Kati katika ujumla wake, “lisiwe ni pango la wevi” kwa ajili ya masilahi ya watu wachache, wanaotaka faida na utajiri wa haraka haraka.

Mlipuko wa Bandari ya Beirut: Ulisababisha maafa makubwa kwa watu
Mlipuko wa Bandari ya Beirut: Ulisababisha maafa makubwa kwa watu   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha watu wa Mungu nchini Lebanon kwamba, Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon. Umoja na tofauti zao msingi ziliwawezesha wahenga wa Lebanon kuishi kwa pamoja. Huu ni wakati wa kuzamisha mizizi kwa ajili ya ndoto ya amani, kwa kushirikiana na wengine. Wananchi wasikate tamaa bali waendelee kuwa na matumaini. Viongozi wa kisiasa kadiri ya wajibu wao watafute majibu ya matatizo na changamoto za kiuchumi kwa kujikita katika haki kama msingi wa amani. Wananchi wa diaspora kutoka Lebanon, wajifunge kibwewe kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao huko Lebanon. Jumuiya ya Kimataifa isaidie juhudi za kufufua uchumi nchini Lebanon; yote haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, ikiwa kama Lebanon inataka kujenga na kudumisha amani; wote wanapaswa kuungana na kushikamana ili kutenda katika umoja, upendo na huruma. Wakristo wanaitwa na kuchangamotishwa kuwa ni wapanzi wa amani na wajenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwajibika kikamilifu sanjari na kuendelea kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi na inayosimikwa katika njia ya amani. Majadiliano ya kidini na kiekumene yaimarishe mchakato wa umoja na mshikamano, tayari kufanya kazi kwa pamoja kama ndugu! Katika amani hakuna mshindi wala anayeshindwa. Ni wakati wa kunogesha majadiliano, kukuza na kudumisha elimu na mshikamano wa kweli. Katika pazia la usiku wa giza nene, kuna mapambazuko ya matumaini kama walivyoonesha vijana waliowakabidhi viongozi wa kidini mishumaa inayowaka, kielelezo cha matumaini kwa sasa na kwa siku zijazo.

Watu wa Mungu Lebanon wawe na imani, matumaini na mapendo
Watu wa Mungu Lebanon wawe na imani, matumaini na mapendo   (AFP or licensors)

Katika mchakato wa kufanya maamuzi, viongozi watambue na kukumbuka kwamba, watu wanataka kuona mwanga wa matumaini ukiwashwa katika safari ya maisha yao. Viongozi waongozwe na mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika dhamiri nyofu, ili kuwashirikisha watu wa Mungu matumaini mapya. Wanawake wathaminiwe na kushirikishwa katika vikao vyote vinavyotoa maamuzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Lebanon. Katika kipindi hiki cha kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, changamoto kubwa ni wote kushikamana na kuungana ili kuwa ni kitu kimoja. Kwa njia hii wataweza kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; ili kuendeleza nia njema, ili hatimaye, kuwasha mwanga wa matumaini pale penye giza. Mwisho mwa ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Lebanon, Baba Mtakatifu aliwaaminisha wote chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu, Mfalme wa amani, ili awakirimie huruma na matumaini! Usiku wa kinzani na migogoro utoweke; mapambazuko ya matumaini yaangaze, chuki na uhasama vikome, Lebanon irejee tena kuangaza nuru ya amani.

Maafa Beirut
05 Agosti 2025, 14:57