Tafuta

Papa Leo XIV anasema, amesikitishwa na taarifa za ajali ya Helikopta ya kijeshi iliyoanguka nchini Ghana. Papa Leo XIV anasema, amesikitishwa na taarifa za ajali ya Helikopta ya kijeshi iliyoanguka nchini Ghana.   (ANSA)

Papa Leo XIV Asikitishwa na Ajali Nchini Ghana: Watu 8 Wamefariki Dunia

Papa Leo XIV anasema, amesikitishwa na taarifa za ajali ya Helikopta ya kijeshi iliyoanguka nchini Ghana. Anapenda kuchukua fursa hii, kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu wote na hivyo kuwakabidhi chini ya huruma ya Mungu. Anapenda kuwafariji wote walioondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwahakikishi watu wa Mungu nchini Ghana uwepo wake wa karibu katika kipindi hiki kigumu cha msiba na maombolezo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mawaziri wa Ulinzi na Mazingira wa Ghana wamefariki dunia katika ajali ya Helikopta ya Kijeshi iliyotokea Jumatano tarehe 6 Agosti 2025 katika eneo la kati la Ashanti, pamoja na watu wengine sita. Mkuu wa Majeshi Julius Debrah aliuambia mkutano na Waandishi wa habari kwamba Waziri wa Ulinzi Edward Omane Boamah na Waziri wa Mazingira, Sayansi na Teknolojia Ibrahim Murtala Muhammed (50), walifariki katika ajali hiyo, ambayo imetajwa kuwa ni janga la kitaifa. Helikopta hiyo ilikuwa imeondoka Accra, saa 09:12 kwa saa za huko Ghana na ilikuwa inaelekea katika machimbo ya dhahabu huko mjini Obuasi. Wengine waliofariki katika ajali hii mbaya ni: Naibu Mratibu wa Usalama wa Taifa wa Ghana na Waziri wa zamani wa Kilimo Alhaji Muniru Mohammed na Samuel Sarpong, Makamu Mwenyekiti wa Chama tawala cha “National Democratic Congress.” Serikali ya Ghana imeanza uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hii.

Mwanadanu hapa duniani ni mpita njia tu hana makazi ya kudumu
Mwanadanu hapa duniani ni mpita njia tu hana makazi ya kudumu   (ANSA)

Askofu Matthew Kwasi Gyamfi, wa Jimbo Katoliki Sunyani ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana, (Ghana Catholic Bishops’ Conference, GCBC), anasema, Ghana imepata pigo kubwa kutokana na ajali iliyo. Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana limetuma salam za rambirambi kwa Rais, familia, Bunge na Taifa katika ujumla wake. Maaskofu wametoa mwaliko kwa watu wa Mungu kuungana katika sala kuwakumbuka na kuwaombea, kwani kwa hakika, hawa walikuwa ni viongozi waliokuwa wamejisadaka katika huduma kama watumishi wa Serikali, Wanasiasa, Mafundi na Maafisa wa Jeshi. Kwa hakika haya ni maafa makubwa kwa Taifa la Ghana.

Salam za rambirambi kutoka kwa Maaskofu katoliki Ghana
Salam za rambirambi kutoka kwa Maaskofu katoliki Ghana

Katika nyakati za uchungu na majonzi kama hizi, mwanadamu anakumbushwa kwamba, hapa duniani ni msafiri na wala hana makazi ya kudumu; lakini watambukwa wale wote wanaosadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, huku wakikita maisha yao katika kanuni maadili, utu wema, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha wa ajali hii, Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, kwenda kwa Askofu Matthew Kwasi Gyamfi, wa Jimbo Katoliki Sunyani ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana, anasema, amesikitishwa na taarifa za ajali ya Helikopta ya kijeshi iliyoanguka nchini Ghana. Anapenda kuchukua fursa hii, kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu wote na hivyo kuwakabidhi chini ya huruma ya Mungu. Anapenda kuwafariji wote walioondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwahakikishi watu wa Mungu nchini Ghana uwepo wake wa karibu katika kipindi hiki kigumu cha msiba na maombolezo.

Papa Leo XIV Ajali Ghana
08 Agosti 2025, 14:15