Papa:Ninaomba Mungu ili silaha Ukraine zinyamazishwe na njia ya mazungumzo ifunguliwe
Vatican News
Katika fursa ya siku ya Uhuru nchini Ukraine inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 24 agosti ambapo kwa mwaka huu imefikisha miaka 34 ya uhuru Baba Mtakatifu Leo XIV, Papa Leo XIV alituma ujumbe kwa Rais Volodymyr Zelenskyy, akimhakikishia "sala zake kwa watu wa Ukraine wanaoteseka kwa sababu ya vita, hasa kwa wale wote waliojeruhiwa kimwili, kwa wale ambao wamepoteza wapendwa wao, na kwa wale ambao wamepoteza nyumba zao." “Kwa moyo uliojeruhiwa na jeuri iliyoharibu nchi yako, ninawageukia wewe," Papa aliandika, akimwomba Mungu awafariji wale wanaoteseka kutokana na matokeo ya vita, kuwatia nguvu "waliojeruhiwa," na kutoa "pumziko la milele kwa marehemu."
Papa pia anamsihi Mwenyezi aguse mioyo ya watu wenye mapenzi mema na "kunyamazisha kelele za silaha," akitoa njia ya "mazungumzo" na kufungua "njia ya amani kwa manufaa ya wote." Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alisema: “Nalikabidhi taifa lako kwa Bikira Maria, Malkia wa Amani.” Ujumbe wa Papa ulichapishwa na Rais Zelenskyy katika chapisho kwenye akaunti yake ya X. "Ninashukuru kwa dhati Baba Mtakatifu kwa maneno yake mazito, sala zake, na umakini wake kwa watu wa Ukraine katikati ya vita vya uharibifu." Mkuu huyo wa nchi ya Ukraine aliongeza kwamba: “matumaini” na “juhudi” zote za taifa “zinaelekezwa katika kufikia amani iliyosubiriwa kwa muda mrefu,” “ili wema, ukweli, na haki viwepo,” na alioneesha shukrani zake kwa “uongozi wa kimaadili na uungwaji mkono wa kitume” wa Papa.
