Madhara ya Vita ya Wenyewe Kwa Wenyewe Nchini Sudan
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Kimataifa kwa huzuni na masikitiko makuu, tarehe 15 Aprili 2025 inafanya kumbukizi ya Miaka miwili tangu kuibuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan na hivyo kusababisha vifo vya maelfu ya watu wasiokuwa na hatia na mamilioni ya watu kulazimika kuyakimbia makazi yao. Vita hii imepelekea mateso makubwa kwa watoto na wanawake na watu wengine wengi kuendelea kuishi katika mazingira magumu na hatarishi. Huu ni ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari yake kwenye Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Matawi, tarehe 13 Aprili 2025.
Baba Mtakatifu anawaalika wahusika wakuu katika mgogoro huu wa kivita, kukomesha ghasia hizi na kuanza kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Sudan. Jumuiya ya Kimataifa ihakikishe kwamba, watu wa Mungu Sudan wanapata misaada ya kiutu, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Mgogoro wa Sudan unatajwa kama "mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu kuwahi kurekodiwa" na sasa vita vinavyoendelea kati ya vikosi vya serikali na waasi wenye silaha nchini Sudan vimehamia kwenye mji wa El Fasher, mji mkuu wa Kaskazini mwa Darfur, magharibi mwa nchi ya Sudan.
Wanamgambo wa Kikosi cha “Rapid Support Forces (RSF)” na makundi washirika ya kisiasa na yenye silaha, hivi karibuni wametia saini mkataba wa kuanzisha serikali katika maeneo wanayoyadhibiti. Kundi hilo, ambalo sasa linajiita “Sudan Founding Alliance”, linadai linataka taifa hilo jipya liwe la kisekula, kidemokrasia, na la ugatuzi, linalosimikwa juu ya misingi ya "uhuru, usawa na haki." Hatua hii inazua wasiwasi na hofu kuhusu madhara yanayoweza kutokea kwa nchi ambayo tayari imehathiriwa na migogoro pamoja na vita.
Sudan iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Mwezi Aprili mwaka 2023, kati ya Jeshi la Sudan na “Rapid Support Forces.” RSF iliundwa kutoka kwa wanamgambo wa Janjaweed ambao hapo awali walipigana kwa niaba ya serikali ya Sudan na wanaongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti. RSF inadhibiti sehemu muhimu za Sudan, ikiwa ni pamoja na Darfur, sehemu za Khartoum, Kordofan, na Blue Nile. Mgogoro huu umekwisha kupelekea watu zaidi 60, 000 kupoteza maisha. Zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Huu ni ukatili unaotekelezwa na RSF pamoja na Jeshi.