Papa Francisko kwa vijana wa Opus Dei wa Vyuo vikuu tembeeni na shauku ya imani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu aliwatumia ujumbe uliochapishwa kwenye Tovuti ya Shirika la Opus Dei, kwa washiriki vijana wa Mkutano wa Kimataifa wa Vyuo vikuu (UNIV 25) ambao unaendelea jijini Roma kuanzia tarehe 12 hadi 20 Aprili 2025 kwa kuongoza na mada: "Raia wa Ulimwengu wetu."
"Vijana wapendwa, Mkutano wa kimataifa wa UNIV ambao umeandaliwa Roma unawaunganisha katika siku hizi katika maadhimisho mara mbili ya matukio ya kijubilei; kwanza Mwaka Mtakatifu 2025 na maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 100 tangu kupewa daraja la Upadre. Mtakatifu Josemaría Escrivá," anaandika Papa.
Papa ameongeza kuwa: “ni sababu ngapi za kuweza kumshukuru Mungu na kuendelea kutembea kwa shauku katika imani, bidii katika upendo na kudumu katika tumaini (rej 1 Ts 1,3)!” Kwa njia hiyo baba Mtakatifu anaunganisha “furaha yake na kuwasindikiza kwa sala zake, huku akimuomba Bwana kwamba wakati huu wa kipindi cha hija na cha kukutana kidugu, kiwasukume kuwapelekea wote Injili ya Yesu Kristo, aliyekufa na kufufuka, kama tangazo la tumaini ambalo ahadi zake, zinaleta furaha na iliyosimikwa juu ya upendo usiokatisha tamaa( rej. Bolla Spes non confundit, 2).
Kwa kuhitimisha ujumbe huo, Papa amesema kuwa Bwana awabariki na Bikira Maria awalinde. Na ameomba tafadhali, wasisahau kusali kwa ajili yake. Ni ujumbe uliotiwa saini kidugu na Papa Francisko tarehe 8 Aprili 2025.