Papa Francisko katika sala kwenye Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu
Vatican News
"Mapema alasiri ya leo, Papa Francisko alikwenda kwenye Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu katika kesha la Dominika ya Matawi, na mwanzo wa Juma Kuu Takatifu, alikaa kitambo na kusali mbele ya picha ya Bikira, Salus Populi Romani, yaani Bikira Afya ya Watu wa Roma." Hayo ndiyo yaliyoelezwa na Ofisi ya Vyombo vya Habari Vatican, alasiri Jumamois tarehe 12 Aprili 2025.
Uhusiano wa Papa na Picha ya Bikira Salus Populi Romani
Uhusiano kati ya Papa Francisko na Picha ya Bikira Afya ya Watu wa Roma (Salus Populi Romani) umekuwa wa kimwana. Mwisho mwa kulazwa kwake hospitalini Gemelli, Roma majuma matatu yaliyopita, Papa alikuwa amesimama kwenye uwanja mbele ya Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu bila kuingia ndani, kabla ya kurejea makao yake, katika Nyumba ya Mtakatifu Marta, ili kusali na kupeleka shada la maua liwekwe mbele ya Picha ya Bikira, alilokabidhi kwa Kardinali Rolandas Makrickas, Mkuu mwenza wa Basilika hiyo. Hilo ndilo lilikuwa ni shada la maua ya njano ambalo Bi. Carmela Mancuso alikuwa amempelekea Papa na baada ya Papa Francisko kutoa shukrani kwa umma kwa kumtambua katika umati wa watu alipokuwa juu ya ghorofa katika hospitali ya Gemelli.
Desturi ya Papa tangu 2013
Heshima kwa picha ya Maria Salus Populi Romani ni desturi ya Baba Mtakatifu Francisko iliyoanza tarehe 14 Machi 2013, siku moja baada ya kuchaguliwa kwake, na imedumishwa kabla na baada ya kila akifanya ziara za kitume na kichungaji. Na hatimaye, kwenda kwake mnamo Machi 23, ilikuwa kama kuashiria mwisho wa safari ya hospitali na mwanzo wa safari mpya ya kupata nafuu akiwa makazi yake katika nyumba ya Mtakatifu Marta mjini Vatican.
Ziara ya Mwisho ya Kitume ya 47 huko Ajaccio, Corsica
Ziara ya mwisho katika Kanisa Kuu la Kirumi zaidi ya mia moja iliyofanyika, ilikuwa ni tarehe 14 Desemba 2024 wakati Papa alipokwenda kusali kwa kuzingatia ziara yake ya kitume ya 47 ya kwenda huko Ajaccio, kisiwani Corsica, kwa ajili ya hitimisho la Kongamano la "La Religiosité Populaire en Mediterranée", yaani "Udini Maarufu wa watu wa Mediterranea."