Mahubiri Kwaresima 2025: Matumaini, Kupaa na Wajibu wa Kushuhudia!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika Kanuni ya Imani anasadiki na kufundisha kwamba, “Akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Ubinadamu ukiachwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye “nyumba ya Baba,” kwenye uzima na kwenye furaha ya Mungu. Kristo Yesu peke yake ameweza kumfungulia mtu njia hii “ili tukae tukiamini kwamba, sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu. Mbinguni Kristo Yesu anatekeleza ukuhani wake daima kwa kumwokoa na kumkomboa mwanadamu. Kupaa kwa Kristo Yesu mbinguni ni alama dhahiri ya kuingia ubinadamu wa Yesu ndani ya makao ya mbingu ya Mwenyezi Mungu, ambako toka huko atarudi. Rej. Mdo 1: 11, lakini ubinadamu huu kwa sasa unafichika mbele ya macho ya watu. Rej. Kol 3: 3. Kristo Yesu ni kichwa cha Kanisa, anawatangulia waja wake katika ufalme mtukufu wa Baba wa milele, ili waamini ambao ni viungo vya huo Mwili waendelee kuishi katika tumaini la kuishi naye milele yote. Kristo Yesu, akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya Hekalu la mbingu, anasali kwa ajili ya waja wake kama mshenga anayewahakikishia kumiminwa kwa Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Roho wa Kristo Mfufuka awasaidie waamini kung’amua na hatimaye, kusoma alama za nyakati, ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili kwa uaminifu na kwa furaha katika medani mbalimbali za maisha, daima wakijitahidi kuwa ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni wakati muafaka wa kuangalia matukio muhimu kabla ya Kristo Yesu kupaa mbinguni, kwani, anawaachia wafuasi wake wosia akisema “Basi, enendeni, mkawafanye Mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28:19-20. Huu ni ujumbe makini kwa vijana kujizatiti katika utume wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa. Wazee na wagonjwa hata katika mahangaiko yao, watambue kwamba, wanayo nafasi muhimu sana katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu ulimwenguni. Na kwa wanandoa wapya watengeneze mazingira katika familia zao, ili ziwe ni mahali pa kujifunza kumpenda Mwenyezi Mungu, daima wakijitahidi kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili. Waamini wapokee na kujitahidi kumwilisha wito wa umisionari unaofumbatwa katika ushuhuda, kwa kuendelea kuungana na Kristo Yesu katika maisha ya: Sala, Sakramenti na Huduma ya huruma na upendo kwa Mungu na jirani.
Ni katika muktadha huu, Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa na kuongozwa na kauli mbiu “Kutia nanga katika Kristo” Kukita mizizi na kusimikwa katika tumaini la maisha mapya.” Mahubiri haya ni kwa ajili ya waamini wote wanaojisikia kutaka kuboresha maisha yao ya kiroho na yanaanza saa 3:00 kwa Saa za Ulaya. Ni katika muktadha wa mahubiri ya nne ya Kipindi cha Kwaresima tarehe 11 Aprili 2025 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Kueneza matumaini: Kupaa na wajibu.” "Tumesimikwa katika Kristo Yesu: Wenye Mizizi Katika Tumaini la Maisha Mapya." Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa amekazia umuhimu wa kujikita katika wongofu wa ndani: ushuhuda wa Maria Magdalena; Kupaa Bwana mbinguni na kutazama juu; Ushuhuda wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; sanjari na nguvu ya Roho Mtakatifu katika ushuhuda. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelekea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho wao na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku. Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani tayari kuambata utakatifu wa maisha. Kumbe, maadhimisho ya Jubilei, yanapata chimbuko lake katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ambaye ndiye chimbuko la lengo halisi la imani ya Kikristo. Rej. Yn 10: 7-9. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ushiriki na utume. Kwa kujikita katika hekima na busara, chemchemi ya unyenyekevu, upendo, imani, furaha ya kweli na msamaha kutoka katika undani wa mwamini. Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, Kristo Yesu ni Mlango unaojenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, tayari kumpokea Kristo Yesu kama zawadi, ili kumtangaza na kumshuhudia kwa watu wa Mataifa. Kwa muda wa siku arobaini Kristo Yesu aliwatokea na kujidhihirisha kwa wafuasi wake kama ilivyotokea kwa Maria Madgalena. Rej. Yn 20: 11-15. Alionja huruma na upendo wake wa ndani, akamtafuta kule Bustanini, huku akirejesha ile kumbukumbu ya upendo na faraja baada ya mateso na kifo cha Msalaba; akamtambua Kristo kwa kuitwa jina na huo ukawa ni mwanzo wa furaha mpya ya ufufuko wa Kristo kwa wafu, tayari kumtangaza na kumshuhudia miongoni mwa watu wa Mataifa. Rej. Yn 20:17-18.
“Noli me tangere” yaani “Usiniguse.” Maria Madgalena alitaka kuonja upendo wa Kristo Mfufuka na kwamba, Kristo Yesu anampatia fursa ya kusonga mbele mintarafu Heri za Mlimani, tayari kutangaza na kushuhudia Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka. “Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote.” Efe 4:10. Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kumtafuta kati ya ndugu zake na kutambua uwepo wake katika uhalisia wa maisha ya waamini, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungano ya udugu wa kibinadamu.Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, Kristo Yesu alipopaa mbinguni, wanafunzi wake walisimama wakitazama juu mbinguni, kwani walikuwa wanafuta Sura ya Kristo Mfufuka, mwaliko kwa waamini kwanza kabisa ni kuutafuta Uso wa Kristo Mfufuka katika Neno, Sakramenti, Huduma na katika uhalisia wa maisha ya waamini kwa sababu Mwenyezi Mungu “awe yote katika wote.”1Kor 15:28. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kubeba vyema Misalaba ya maisha yao, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia huduma ya ukweli katika upendo; kwa kutoka katika undani wao, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa waliobatizwa: Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa ujengwe katika umoja: “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.” Ushuhuda huu ujengwe katika upendo na ukweli.
Kupaa Bwana Mbinguni ni mwanzo wa mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kama walivyofanya watakatifu na mashuhuda wa imani; kwa kutambua na kuheshimu uzuri unaofumbatwa katika: Kazi ya Uumbaji, kwa kuheshimu, kulinda na kudumisha Injili ya uhai; kwa kusimama kidete katika mchakato wa uinjilishaji wa kina kwa nguvu za Roho Mtakatifu; Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; katika toba na wongofu wa ndani; kwa kumwilisha huduma ya upendo na hekima ya kichungaji; kwa njia ya unyenyekevu, usikivu, ukarimu pamoja na mang’amuzi; kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa tunu msingi za Kiinjili; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: utu, heshima na haki msingi za binadamu kama njia muafaka ya kuuona Uso wa Mungu, tayari kujenga ushirika na mafungamano ya watu wa Mungu. Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi, changamoto kwa Wakristo ni kwenda ulimwenguni kote kutangaza na kushuhudia Injili. “Nao wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.” (Mk. 16:20.) Maisha ya Kristo aliyezaliwa, akateswa, akafa, akafufuka na kupaa mbinguni yanakuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili; alama ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo na hivyo kuwapatia wanadamu maisha mapya kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa amehitimisha mahubiri yake ya nne ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 kwa kusema kwamba, Kupaa Bwana Mbinguni ni amana, utajiri na urithi wa Kanisa kutoka kwa Kristo Yesu anayewakirimia waja wake fursa ya kujenga ushirika wa kweli na wa kina, tayari kujiaminisha mbele ya Mungu kama mahujaji wa matumaini, tayari kuwajibika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya huduma ya Injili; kwa kumpenda Mungu na jirani; kwa kuupokea na kuubeba vyema Msalaba wa wokovu wa mwanadamu. Kristo Yesu atarudi tena kuwahukumu wazima na wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwilisha, kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili, kwa kuendelea kuboresha matumaini wakati huu wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Kristo Yesu, lango la imani, matumaini na mapendo. SALA: “Kanisa lako, ee Baba, lifurahie kwa furaha takatifu fumbo linaloadhimisha katika liturujia hii ya sifa, kwa sababu katika Mwanao kupaa kwenda zake mbinguni, ubinadamu wetu umeinuliwa kando yako, na sisi, viungo vya mwili wake, tunaishi katika tumaini la kumfikia Kristo, kichwa chetu, katika utukufu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.