Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
Allegro giocoso
Ratiba Podcast
Mababa wa Kanisa wanasema, kila Injili ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa. Mababa wa Kanisa wanasema, kila Injili ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa.   (Vatican Media)

Amana na Utajiri wa Simulizi la Mateso ya Yesu Kadiri ya Mwinjili Luka: Mwaka C

Papa Francisko kama sehemu ya tafakari wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Matawi, amekazia maneno ya Kristo Yesu kwa Baba yake wa mbinguni, kwa kujikabidhi ili kutenda mapenzi ya Baba yake wa mbiguni; kuwasamehe kwani hawajui watendalo na kwamba, mikononi mwa Baba yake wa mbinguni aliiweka roho yake. Kristo Yesu hakusimama kujitetea, bali alikubali kufedheheshwa, akajitwika Msalaba wake akaendelea na Njia ya Msalaba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Simulizi la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu kadiri ya Mwinjili Luka, Mwaka C wa kanisa: Lk 22: 14-23-56 linabeba uzito wa juu sana kama kielelezo cha unyenyekevu wa Kristo Yesu kwa Baba yake wa mbinguni, anayewasamehe watu dhambi zao kama inavyojidhihirisha katika maneno matatu ya Kristo Yesu pale Msalabani: "Baba, uwasamehe, kwa maana hawajui watendalo" Lk 23:34). Haya ni maneno yanayoelekezwa kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma, upendo, msamaha na faraja kwa wale wote wanaomkimbilia. Huduma ya upendo ni chemchemi ya furaha ya Injili na kwamba, sadaka ya Kristo Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Lk 22: 19. Mtakatifu Petro anachukua nafasi ya pekee kabisa katika sala ya Kristo Yesu kwani Petro ni mwamba na anamkabidhi dhamana na jukumu la kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Luka anasimika Injili yake kwa mashuhuda kama akina Simoni Mkirene, Yusufu wa Arimathaya Lk 23: 50-56; Wahalifu wawili waliosubiwa pamoja na Kristo Yesu 23: 39-43; Akida aliyemkiri Kristo Yesu kuwa kweli ni mtu mwenye haki Lk 23: 47 pamoja na wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. Lk 23: 49.

Injili ni amana na utajiri wa Kanisa
Injili ni amana na utajiri wa Kanisa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mwinjili Luka amezingatia Mapokeo na ni mwaminifu kadiri ya Injili ya Marko, ambayo anaitumia kama rejea, ili kuboresha ufahamu wake kuhusu "Yesu wa Nazareti, ambaye alizunguka huko na huko akitenda mema [...], kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye" Mdo 10:38. Mababa wa Kanisa wanasema, kila Injili ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa. Simulizi la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu mintarafu Mwinjili Luka, linafafanua ubinadamu wa Kristo Yesu, mwingi wa huruma na mapendo; Kristo Yesu ni chemchemi ya wema na daima yuko karibu sana na waja wake. Yesu ni mwalimu na kielelezo cha utakatifu wa maisha, mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na mwombezi wa wote! Simulizi hili linafumbatwa katika jicho la imani! Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya tafakari wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Matawi tarehe 13 Aprili 2025 amekazia maneno ya Kristo Yesu kwa Baba yake wa mbinguni, kwa kujikabidhi ili kutenda mapenzi ya Baba yake wa mbiguni; kuwasamehe kwani hawajui watendalo na kwamba, mikononi mwa Baba yake wa mbinguni aliiweka roho yake. Kristo Yesu hakusimama kujitetea, bali alikubali kufedheheshwa, akajitwika Msalaba wake akaendelea na Njia ya Msalaba.

Mwinjili Luka anatajirisha Injili yake kwa shuhuda za watu mbalimbali
Mwinjili Luka anatajirisha Injili yake kwa shuhuda za watu mbalimbali   (Vatican Media)

Kristo Yesu alikuwa dhaifu kimwili, bali mwenye nguvu kwani alishikamana na kuambatana na Baba yake wa mbinguni, na hivyo kustahimili mateso, kifo na ufufuko wake. Hisia hizi za Kiliturujia anasema Baba Mtakatifu Francisko ni mwaliko kwa waamini kuzifanyia tafakari ya kina, ili hatimaye, kuweza kuzimwilisha na kuwa ni sehemu ya utambulisho wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watu wote wanayo maumivu mbalimbali: kiroho, kimwili, kiutu na kimaadili. Kumbe, imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu iwasaidie waja wake wasikate tamaa, kamwe wasijifungie kwenye uchungu na upweke hasi, lakini wajizatiti kukabiliana na changamto, matatizo na fursa mbalimbali, wakitambua kwamba, Kristo Yesu anawafunika na hivyo wanakumbatiwa na rehema pamoja na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kumkumbuka na kumwombea, wakati huu anapokabiliana na changamoto ya udhaifu wa kimwili, anaendelea kuhisi: upendo, huruma na ukaribu wa Mungu katika maisha yake.

Papa Francisko amesalimiana na waamini baada ya Misa ya Matawi
Papa Francisko amesalimiana na waamini baada ya Misa ya Matawi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu anasema anawaombea na kuwakabidhi watu wote wenye shida; watu wanaoteseka na kuathirika kwa vita, umaskini, njaa na magonjwa pamoja na majanga asilia kwa Bikira Maria, ili aweze kuwaombea. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea watu waliofariki na kujeruhiwa huko Santo Domingo na anapenda kuwafariji wale wote walioguswa na kutikiswa na ajali ya kuporomoka kwa paa la Klabu. Amewakumbuka watu wa Mungu nchini Lebanon wanapofanya kumbukizi ya miaka 50 tangu kuibuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na kwamba, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu waweze sasa kuishi kwa amani. Baba Mtakatifu anaendelea kuombea amani na utulivu nchini Ukraine, Palestina, Israeli, DRC, Myanmar na Sudan ya Kusini. Bikira Maria Mama wa mateso, awaombee rehema kwa Mungu, ili awasaidie kuishi vyema Juma kuu, kwa kujikita katika imani.

Mateso ya Kristo
13 Aprili 2025, 14:28
Prev
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930   
Next
May 2025
SuMoTuWeThFrSa
    123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031