Tafuta

Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu,   (Vatican Media)

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Mtoto Yesu Nyota ya Matumaini Kwa Wote

Baba Mtakatifu Francisko katika Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2025, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Jubilei ya matumaini katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu: Nyota angavu, kielelezo cha furaha na upendo wa Mungu; hii ni nyota inayoonekana na wote, alama ya matumaini kwa wale wanaojibidiisha kumtafuta Mungu na kwamba, nyota hii angavu ni kielelezo cha hija ya mapendo hapa duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Sherehe ya Tokeo la Bwana, Epifania ni ufunuo wa Kristo Yesu kama Masiha wa Israeli, Mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu. Mamajusi wanawakilisha dini za mazingira ya kipagani. Injili inaonesha matunda ya kwanza ya watu wa Mataifa wanaopokea Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Mamajusi wanaonesha ile kiu ya watu wa Mataifa kutafuta kwa Israeli mwanga wa Masiha kwa nyota ya Daudi atakayekuwa Mfalme wa Mataifa. Hiki ni kielelezo cha watu wa Mataifa wanaotaka kumwabudu, kumsujudia na kumwamini kama Mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu. Rej. KKK 528. Mamajusi, kimapokeo, wanatajwa kuwa walikuwa watatu na majina yao yakiwa Gaspari, Melkiori na Baltazari. Hawa walikuwa ni wataalam wa nyota, watu wenye hekima na busara na matajiri waliongozwa kutoka mashariki kuja kumsujudu mfalme aliyezaliwa. Mamajusi hawa wanawakilisha mataifa yote yasiyo Wayahudi na kitendo chao cha kutoka mbali katika nchi zao kuja kumsujudia Mtoto Yesu kinamtambulisha Kristo Yesu kama Masiha wa Mataifa yote. Yeye ni Masiha wa ulimwengu mzima na ndiye anayewaalika watu wote waupate wokovu kwa njia yake.

Waamini wakiongozwa na nyota angavu ni mahujaji wa matumaini
Waamini wakiongozwa na nyota angavu ni mahujaji wa matumaini

Mamajusi walimtolea Mtoto Yesu zawadi ya Dhahabu, kielelezo cha Ufalme wake; Uvumba kielelezo cha Umungu na Ukuhani wake mkuu na hatimaye, Manemane ni kielelezo cha mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Hii ni sherehe ya sala na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo. Ni Siku ya kutangaza pamoja Injili ya upendo; Kusali kwa pamoja kama ndugu; kucheza pamoja, kielelezo makini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kutembea pamoja kama mahujaji wa matumaini, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia.

Epifania pia ni sikukuu ya Utoto Mtakatifu
Epifania pia ni sikukuu ya Utoto Mtakatifu

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Jubilei ya matumaini katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu: Nyota angavu, kielelezo cha furaha na upendo wa Mungu; hii ni nyota inayoonekana na wote, alama ya matumaini kwa wale wanaojibidiisha kumtafuta Mungu na kwamba, nyota hii angavu ni kielelezo cha hija ya mapendo inayosimikwa katika unyenyekevu, ili kukutana na Kristo Yesu, kwa kukiri na kutangaza imani, ili hatimaye kupokea upendo na huruma yake kuu. Mamajusi walishuhudia na kusema: “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2.

Mamajusi walikuwa ni wataalam wa nyota.
Mamajusi walikuwa ni wataalam wa nyota.

Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali ndio waliowafunulia watu wa Yerusalemu siri ya nyota angavu ya Noeli, upya wa maisha na matumaini kwa watu wanaojibidiisha kumtafuta Mungu katika maisha yao. Hii ni nyota angavu inayowaonesha watu wote wokovu na furaha inayofumbatwa katika upendo wa Mungu. Huu ni upendo uliofanyika mwili na hivyo kujisadaka kwa ajili ya binadamu wote, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni alama na vyombo vya matumaini kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo. Hii ni nyota iliyowaongoza Mamajusi kwenda mjini Bethlehemu, mwaliko kwa waamini kwa njia ya upendo wao, waweze kumpeleka Kristo Yesu kwa watu wanaokutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kumtambua Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, ufunuo wa uzuri wa Uso wa Mungu aliyefanyika mtu. Rej Isa 60: 2; jinsi anavyopenda, anavyoonesha: ukaribu, huruma na upendo kwa kuhakikisha kwamba, nyoyo zao zinaangazwa na mwanga angavu wa upendo na matendo ya ukarimu. Mamajusi wakiwa wanaangalia angani, wanatoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mwanga kwa wengine, ili waweze kuumwona na hatimaye, wamwone Mwenyezi Mungu.

Mahujaji wa matumaini
Mahujaji wa matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Nyota angavu inayonekana na wote ni alama ya matumaini, kwa wale wanaomtafuta kwa imani na matumaini, lakini Mungu ndiye anayeonesha hatua ya kwanza ya kumtafuta binadamu na kwamba, Mamajusi ni mfano wa mahujaji wa kila rika na kwa makundi mbalimbali ya watu, ili kuwakumbusha wanadamu kwamba, Mwenyezi daima anawatafuta waja wake. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, lakini bado kuna changamoto kubwa ya watu kutofahamiana na wala kukutana katika tofauti zao msingi. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu anapenda kukutana na watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa, ili aweze kuwakabidhi utume wake wa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu, kwa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini, ili watu wote katika umoja wao, waweze kupata furaha ya kweli nyumbani mwake.

Mtoto Yesu ni nyota ya imani, matumaini na mapendo
Mtoto Yesu ni nyota ya imani, matumaini na mapendo

Nyota angavu inaelezea pia ndoto ya Mwenyezi Mungu, ili binadamu wote katika amana, utajiri na tofauti zao msingi waweze kujenga familia moja ya binadamu, kwa kuishi katika maelewano, ustawi na amani. Rej Isa 2:2-5 na kwamba, nyota hii inawaelekeza waamini katika hija ya matumaini, ili hatimaye, kuweza kukua katika pendo la Mungu hadi mwisho wa maisha ya mwanadamu, kwani hakuna mtu awaye yote anayeweza kujigamba kwamba, amefika ukomo, bali waamini wote waendelee kufanya hija ya maisha inayosimikwa katika unyenyekevu, siku kwa siku, huku wakiendelea kuzifuata nyayo za Kristo Yesu. Waamini wajizatiti katika kumwilisha upendo kati yao, ili kuweza kukutana na Kristo Yesu, kwa kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na hivyo kuonesha ukuu wa huruma na upendo wake kwa watu wote. Ni kwa njia ya toba, wongofu wa ndani pamoja na msamaha wa dhambi, waamini wanaweza kutangaza na kushuhudia kwa ari na moyo mkuu wa kimisionari kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia. Waamini wafanye hija ya pamoja kama watu wanaotafuta maana ya maisha.

Hii pia ni sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Malezi ni muhimu
Hii pia ni sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Malezi ni muhimu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama “wanafunzi wa njia” Rej. Mdo 9:2. Mwamini ni msafiri ambaye anatambua kwamba, kamwe hajafikia lengo na hatima ya safari yake hapa duniani. Kumbe, anapaswa kujifunza kila siku, akijitahidi kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni: njia, kweli, na uzima unawaowapeleka kwa Baba wa milele. Huu ni wito na mwaliko wa kutafuta kila wakati fursa ya kupanua nyoyo zao sanjari na kuimarisha mshikamano wa upendo. Na kwa njia hii waamini wanaweza kuwa ni mwanga unaowaonesha watu kwa Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama mwema na mkarimu, ili hatimaye, kuweza kukutana naye, kumfahamu na kumwabudu na kwa njia yake waamini waweze kupyaishwa kwa kupeleka mwanga wa upendo wake ulimwenguni kote.

Papa Epifania 2025
06 January 2025, 15:41