Tafuta

Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.  (Vatican Media)

Mbiu ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana Kwa Mwaka 2025

Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo Yesu kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo Yesu kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 20 Aprili 2025.

Pasaka ya Bwana itaadhimishwa tarehe 20 Aprili 2025
Pasaka ya Bwana itaadhimishwa tarehe 20 Aprili 2025

Kila Dominika, Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili kuu katika maisha na imani yao; kwani Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Sherehe ya Pasaka ni chemchemi ya Sikukuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 5 Machi 2025 kwa waamini kupakwa majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni hapo tarehe 1 Juni 2025 na Pentekoste, Sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya Waamini Walei itaadhimishwa hapo tarehe 8 Juni 2025.

Sherehe ya Pentekoste itaadhimishwa tarehe 8 Juni 2025
Sherehe ya Pentekoste itaadhimishwa tarehe 8 Juni 2025

Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio ambayo kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa, na maandalizi ya ujio wa Kristo Yesu itaadhimishwa hapo tarehe 30 Novemba 2025. Mama Kanisa anayeendelea kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Sherehe na Sikukuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; Sikukuu za Mitume na Watakatifu mbalimbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu. Sifa na utukufu kwa Kristo Yesu aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia na nyakati zote ni zake, ni Alfa na Omega. Amina.

Mbiu ya sherehe ya Pasaka 2025
06 January 2025, 14:44