Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa: Mashuhuda wa Upendo wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amejifunua kwa njia ya Sheria, kielelezo cha utambulisho, dira na mwongozo wa watu wa Mungu. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Manabii wake watakatifu, waliotumwa kutangaza na kushuhudia uwepo wake endelevu katika hija ya maisha ya waja wake. Hatimaye, Mwenyezi Mungu katika nyakati hizi amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma na upendo wa Baba wa milele. Huyu ndiye Neno aliyekuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huu ni muhtasari wa Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, kama tunavyousoma katika Dibaji au Utangulizi wa Injili yake. Hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu inayowaambata na kuwakumbatia watu wa nyakati zote. Ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Huyu ndiye Nuru halisi inayomtia nuru kila mtu na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kuikwepa nuru hii. Ndiye Kristo Yesu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Neno wa Mungu ni nuru inayong’aa gizani, wala giza halikuiweza. Rej Yn 1:5. Kristo Yesu ni ufunuo wa upendo wa Mungu, unaovunjilia mbali vikwazo na vizingiti; hali ya kukataliwa na hivyo kuendelea kuangaza mapito ya waja wake. Huyu ndiye Neno wa Mungu aliyezaliwa kwake Bikira Maria anayepita na kuvuka kuta za utengano. Neno wa Mungu amezaliwa wakati “wakuu wa Mataifa” wakiwa bado wamezama katika kulinda himaya zao badala ya kujibidiisha kumtafuta Mwana wa Mungu aliyezaliwa mjini Bethlehemu. Rej. Mt 2:3-8.
Neno wa Mungu aliishi katika Familia Takatifu; akapokelewa, akaoneshwa na kukuzwa katika upendo kutoka kwa Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Yosefu kadiri ya hali na mazingira yao. Neno wa Mungu alijifunua katika hali ya unyonge pasi na ulinzi; akakutana na wachungaji kutoka kondeni, watu waliokuwa wanathamini uhai wa binadamu, lakini hawakuwa na thamani kubwa mbele ya jamii. Rej Lk 2:8-18. Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, wakiongozwa na nyota, wakajibidiisha kumtafuta “Yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi.” Mt 2:1. Mamajusi wakabahatika kumwona Mtoto Yesu katika hali ya kawaida na mazingira ya umaskini mkubwa. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Dominika ya Pili ya Kipindi cha Noeli, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 5 Januari 2025. Licha ya changamoto zote hizi, Mwenyezi Mungu anaendelea kujibidiisha kuwatafuta waja wake, ili wale wanaokwenda katika giza nene waweze kuona nuru kuu na wale wanaokaa katika uvuli wa mauti waweze kuangaziwa na nuru kuu. Rej Isa 9: 1-6. Baba Mtakatifu anasema, huu ni ukweli unaofariji na kuwatia watu shime katika ulimwengu mamboleo unaohitaji kwa kiasi kikubwa mwanga, matumaini na amani, pale ambapo watu watakatifu wa Mungu wanatengeneza mazingira na wanataka kuondokana na hali zinazokinzana na Nuru ya uzima.
Huu ni mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu anaotaka watu wa Mungu kumwiga Mwenyezi Mungu ambaye kimsingi ni upendo, kwa kuwafungulia wengine mwanga wa matumaini wale wote wanaokutana nao katika mazingira ya kifamilia, kijamii na Kimataifa. Mwenyezi Mungu anawaalika watu wake waanze kupiga hatua ya kwanza, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, hususan kwa watu wanaoteseka; kwa kujitahidi kuwasaheme wale waliowakosea; huruma na msamaha, ili kuhakikisha kwamba, njia inakuwa ni nyeupe kwa watu wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini. Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini; kwa kuambata na kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwani hii kimsingi ndiyo njia ya wokovu. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake kwa kusema, mwanzoni kabisa mwa Mwaka mpya wa 2025, waamini watumie fursa hii, kutathimini hali yao ya maisha, ikiwa kama wameonesha uthubutu wa kuwafunguliwa jirani zao dirisha la matumaini; chombo cha upendo wa Mungu. Bikira Maria, Nyota angavu inayowaongoza watu kumwendea Kristo Yesu, awasaidie watu wote wa Mungu kuwa ni vyombo na mashuhuda angavu wa upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.