Tafuta

Ibada kwa Jina Takatifu la Yesu inapata chimbuko na asili yake kwenye Maandiko Matakatifu Ibada kwa Jina Takatifu la Yesu inapata chimbuko na asili yake kwenye Maandiko Matakatifu 

Ibada kwa Jina Takatifu la Yesu: Mkombozi wa Ulimwengu

Jina Takatifu la Yesu lilifafanua ndani mwake: Fumbo la Umwilisho linalopata hatima yake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu. Hili ni jina linalofumbata na kuambata tunu msingi za maisha ya Kikristo: Ufukara, maisha, utume na kazi alizotenda Kristo Yesu kwa ajili ya kufunua na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu.."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Ibada kwa Jina Takatifu la Yesu inapata chimbuko na asili yake kwenye Maandiko Matakatifu. Lakini hizi hasa zilikuwa ni juhudi za Mtakatifu Bernardino wa Siena (8 Septemba 1380 - 20 Mei 1444), na Yohane wa Capistrano) Watawa wa Shirika la Ndugu Wadogo kuineza sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Bernardino wa Siena ndiye anayesadikiwa kutunga herufi IHS, yaani “Iesus Hominum Salvator.” Na kwa lugha ya Kigiriki “ΙΗΣΟΥΣ, Iesûs” “Yesu” na maana yake “Yesu Mkombozi wa Binadamu.” Kwa kuwa Jina Takatifu la Yesu ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo, Papa Innocent XIII akaieneza Ibada hii ulimwenguni kote. Na Mtakatifu Yohane Paulo II akatamka iandikwe kwenye Kalenda ya Liturujia ya Kiroma na kuadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Januari. Baba Mtakatifu Francisko katika ufunguzi wa Lango la Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo anasema, Kristo Yesu ni tumaini la waja wake, ndiye Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi! Huyu ndiye Mungu aliyejinyenyekesha na kuwa mdogo, Mwanga wa Kimungu unaong’aa katika giza nene la ulimwengu; Ndiye utukufu wa Mungu ulionekana ulimwenguni katika umbo la Mtoto mchanga, katika hori la kulishia wanyama, leo hii anazaliwa katika nyoyo za waja wake, tumaini hai linaloyazunguka maisha ya watu wake.

Mateso, kifo na Ufufuko Uletao maisha na uzima wa milele
Mateso, kifo na Ufufuko Uletao maisha na uzima wa milele

Kwa kufungua Mlango wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, huo ni mwanzo wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hili ni Lango la matumaini, chemchemi ya watu wote wa Mungu. Ili kuweza kuukumbatia mshangao wa zawadi hii kubwa, waamini wanaalikwa kujiunga na wachungaji kule kondeni, kuelekea mjini Bethlehemu kwa haraka, tayari kuonja tena matumaini yaliyopotea, ndani ya kila mwamini, tayari kuyapandikiza katika nyakati na katika ulimwengu, kwa haraka huku wakivutwa na Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko wa kwenda kwa haraka, ili kumwona Mtoto Yesu aliyezaliwa, kwa ajili yao kwa moyo wa shukrani, tayari kukutana naye, ili kuwaonjesha Injili ya matumani katika medani mbalimbali za maisha. Hii ni kwa sababu matumaini ya Kikristo ni ahadi ya Mungu inayopaswa kupokelewa kwa utulivu mkubwa; bila ya kuwa wavivu, bali wakiwa na ari na moyo wa toba na wongofu wa ndani; mahujaji wanaotafuta ukweli, waota ndoto wajasiri; ndoto ya Ulimwengu mpya ambamo haki na amani vinatawala. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujifunza kutoka kwa wachungaji wa kondeni, waliokuwa na ujasiri na watu wenye uthubutu wa kuhatarisha hata maisha yao; tayari kufichua ukosefu wa haki msingi, unaohatarisha maisha ya jirani zao; kwa kuwajibika na kuonesha huruma.

Kristo Yesu ni Lango la maisha na uzima wa milele
Kristo Yesu ni Lango la maisha na uzima wa milele

Itakumbukwa kwamba Mwezi Januari umetangwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada na heshima kwa Jina Takatifu la Yesu na Sikukuu ya Jina Takatifu la Yesu inaadhimishwa kwa namna ya pekee na Wayesuit. Lengo la Sikukuu ya Jina Takatifu la Yesu ni kukuza na kudumisha fadhila za Kikristo, kupyaisha na kuboresha maisha ya Kikristo mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Kwa namna ya pekee kabisa Mtakatifu Bernardino wa Siena, alitaka kulipyaisha Jina Takatifu la Yesu kama lilivyojulikana kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Jina Takatifu la Yesu lilifafanua ndani mwake: Fumbo la Umwilisho linalopata hatima yake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hili ni jina linalofumbata na kuambata tunu msingi za maisha ya Kikristo: Ufukara, maisha, utume na kazi alizotenda Kristo Yesu kwa ajili ya kufunua na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Mt 1:21.

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliyezaliwa na Bikira Maria
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliyezaliwa na Bikira Maria

Kumbe, hili ni jina kadiri ya Maandiko Matakatifu linalofafanua utume wa Yesu, yaani “Mungu anaokoa." Katika maisha na utume wao, Mitume pamoja na wafuasi mbalimbali wameendelea kutenda miujiza na maajabu mengi kwa jina la Yesu kama Maandiko Matakatifu yanavyofafanua “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” Yn 14:13-14. Mwinjili Luka katika Kitabu chake cha Matendo ya Mitume anakaza kusema, “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Mdo 4:12. Jina la Kristo Yesu ni chemchemi ya: Ushirika, umoja na unyenyekevu: “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Flp 2: 5-11.

Jina Takatifu la Yesu
02 January 2025, 14:15