Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Bethlehemu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024 amefungua Lango Kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka 2025 Wakristo wote wanaadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Mkesha huu umehudhuriwa pia na wajumbe kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia kuhusu Habari Njema ya Wokovu, yaani kuzaliwa kwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Wachungaji wanashangazwa na kundi kubwa la Malaika wanaoimba utukufu kwa Mungu juu, kwa kuifungua mbingu na kumtoa Kristo Yesu, ili aweze kumwinua binadamu aliyeanguka na kumpeleka mikononi mwa Mungu Baba Mwenyezi.
Kwa kufungua Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ni mwanzo wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hili ni Lango la: Imani na matumaini, chemchemi ya watu wote wa Mungu. Ili kuweza kuukumbatia mshangao wa zawadi hii kubwa, waamini wanaalikwa kujiunga na wachungaji kule kondeni, kuelekea mjini Bethlehemu kwa haraka, tayari kuonja tena matumaini yaliyopotea, ndani ya kila mwamini, na hivyo kuwa tayari kuyapandikiza katika nyakati na katika ulimwengu, kwa haraka huku wakivutwa na Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko wa kwenda kwa haraka, ili kumwona Mtoto Yesu aliyezaliwa, kwa ajili yao kwa moyo wa shukrani, tayari kukutana naye, ili aweze kuwaonjesha Injili ya matumani katika medani mbalimbali za maisha. Hii ni kwa sababu matumaini ya Kikristo ni ahadi ya Mungu inayopaswa kupokelewa kwa utulivu mkubwa; bila ya kuwa wavivu, bali wakiwa na ari na moyo wa toba na wongofu wa ndani; mahujaji wanaotafuta ukweli, waota ndoto wajasiri; ndoto ya Ulimwengu mpya ambamo haki na amani vinatawala. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujifunza kutoka kwa wachungaji wa kondeni, waliokuwa na ujasiri na watu wenye uthubutu wa kuhatarisha hata maisha yao; tayari kufichua ukosefu wa haki msingi, unaohatarisha maisha ya jirani zao; kwa kuwajibika na kuonesha huruma.
Maadhimisho ya Jubilei ni muda wa matumaini, ni wakati wa kutambua tena furaha ya kukutana na Kristo Yesu; mwaliko wa kupyaisha undani wao, tayari kuzama katika wongofu wa walimwengu, ili kuhakikisha kwamba, huu unakuwa ni muda kweli wa Maadhimisho ya Jubilei, kwa ajili ya dunia hii ambayo imezama katika kutafuta faida, kwa kuelemewa na umaskini; madeni makubwa yasiokuwa na haki, kiasi hata cha kuwageuza walimwengu kuwa wafungwa na watumwa wa utumwa mkongwe na utumwa mamboleo. Waamini wamepewa zawadi ili wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini pale yalipotoweka; mahali pale ambako kuwa vita; mahali ambapo watu wamepoteza matumaini; pale ambapo ndoto zimepotea; pale ambapo watu wamechoka na hawawezi tena kusimama; pale ambapo watu wamevunjika na kupondeka moyo; mahali ambapo watu wanajisikia kushindwa kusonga mbele; mateso yanayotesa nyoyo za watu; mahangaiko ya wafungwa; kwa maskini wanaoteseka kwa baridi bila kusahau maeneo ambayo yamenajisiwa kwa vita. Maadhimisho ya Jubilei ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaonjesha tena matumaini ya Injili, matumaini ya mapendo na matumaini ya msamaha wa kweli.
Ni katika mukadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Francisko ameiandikia waraka, Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Bethlehemu, kuhusu maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, mwanzo wa maisha mapya, matumaini na upatanisho. Maadhimisho ya Jubilei ni muda wa kupyaisha maisha ya kiroho kwa waamini kujikita katika udumifu wa miito yao, ili waweze kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo Yesu wenye furaha. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa anapenda kuwahimiza vijana wa kizazi kipya kujizatiti kikamilifu katika zawadi ya imani, amana na utajiri wa kushirikishana na wengine. Vijana licha ya matatizo na changamoto za maisha, wanahimizwa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, kwani Yeye ndiye chemchemi ya matumaini ya kudumu na kwamba, Kristo Yesu atawasaidia katika kuchangia katika maisha. Huu ni wakati wa kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya urafiki wa kijamii, amana kubwa kwa wanafunzi vyuoni na kwamba, maisha ya pamoja, yawe ni changamoto ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa watu wengine. Ulimwengi una kiu ya watu wenye matumaini yanayosimikwa katika mshikamano dhidi ya vita, vurugu na ghasia; mambo yanayoathiri sana watu wa familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kutoka Chuo Kikuu cha Bethlehemu kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za kiinjili, kama mfano bora wa kuigwa na viongozi wa dini na wanasiasa kutoka katika imani na mapokeo tofauti tofauti; na hivyo kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; uelewano, udugu wa utulivu na haki kwa wote. Mwishoni mwa salam zake Baba Mtakatifu Francisko ameiweka Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Bethlehemu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa na hatimaye, akawapatia baraka zake za Kitume, furaha na amani tele kwa kuzaliwa na Bikira Maria.