Tafuta

Papa:Katika familia ni muhimu kusikiliza zaidi kuliko kuelewa!

“Kwa nini Familia ya Nazareti ni mfano?Kwa sababu ni familia inayozungumza,inayosikilizana na inayojadiliana.Mazungumzo ni jambo muhimu kwa familia! Familia ambayo haiwasiliani haiwezi kuwa familia yenye furaha.Ni katika tafakari ya Papa kabla ya sala ya Malaika wa Bwana,Dominika tarehe 29 Desemba,Mama Kanisa akiadhimisha Siku Kuu ya Familia Takatifu ya Nazareti.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mama Kanisa akiwa anaadhimisha Siku kuu ya Familia Takatifu ya Nazareti ya Yosefu Maria na Yosefu, Dominika tarehe 29 Desemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume ametoa tafakari yake kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Papa amesema: "Leo tunaadhimisha siku kuu ya Familia Takatifu ya Nazareti. Na Injili inasimulia wakati Yesu alikuwa mwenye umri wa miaka kumi na miwili, mwishoni mwa safari ya kila mwaka ya kwenda Yerusalemu, alipopotea na Maria na Yosefu, ambao baadaye walimkuta Hekaluni akijadiliana na madaktari ( Lk 2:41-52). Mwinjili Luka anafunua hali ya roho ya Maria anayemwuliza Yesu: “Mwanangu, kwa nini umetufanyia hivi? Baba yako na mimi tulikuwa tunakutafuta kwa shauku” (Lk 2, 48). Naye Yesu anamjibu: “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwa katika kazi ya Baba yangu?" (Lk 2, 49). Papa amesisitiza: “ Huu ni uzoefu, ningesema karibu kawaida, kwa kila familia ambayo hubadilishana  wakati wa utulivu na mgumu.

Papa Francisko wakati wa tafakari
Papa Francisko wakati wa tafakari

Inaonekana kama historia ya shida ya familia, shida ya nyakati zetu, ya kijana mgumu na wazazi wawili ambao hawawezi kumwelewa. Hebu tusimame tutazame hii familia. Je! mnajua kwa nini Familia ya Nazareti ni mfano? Kwa sababu ni familia inayozungumza, inayosikilizana, inayojadiliana. Mazungumzo ni jambo muhimu kwa familia! Familia ambayo haiwasiliani haiwezi kuwa familia yenye furaha. Ni vizuri wakati mama anapoanza bila ukali na aibu, lakini kwa swali. Maria hakumshtaki au kuhukumu, lakini alijaribu kutaka kuelewa ni jinsi gani ya kumkaribisha Mwanae huyu wa tofauti sana kwa njia ya kusikiliza. Licha ya jitihada hizo, Injili inasema kwamba Maria na Yosefu “hawakuelewa alichokuwa amewaambia” (Lk 2, 50), ikionesha kwamba katika familia ni muhimu zaidi kusikiliza kuliko kuelewa.

Katika familia ni muhimu zaidi kusikiliza kuliko kuelewa, Papa amekazia neno hilo

Kwa hiyo "Kusikiliza kunamaanisha kuwapa wengine umuhimu, kutambua haki yao ya kuwepo na kufikiri kwa kujitegemea. Watoto wanahitaji hilo." Papa ameongeza kusema “Fikirini kwa makini enyi wazazi. Msikilize watoto wenu kwa sababu  wanahitaji.” Na “wakati mzuri  wa mazungumzo na kusikiliza katika familia ni wakati wa chakula. Ni vizuri kuwa pamoja kwenye meza na kuzungumza. Hili linaweza kutatua matatizo mengi, na zaidi ya yote huunganisha vizazi: watoto wanaozungumza na wazazi wao, wajukuu wanaozungumza na babu na bibi zao...” Papa ametoa onyo kuwa “Kamwe msijifungie wenyewe yaani kukaa kimya au, mbaya zaidi, ni  kuinamisha vichwa kwenye simu ya mikononi. Hii kamwe haifanyi kazi ... hiyo isifanyike. Kinachotakiwa ni kuzungumza, kusikilizana kila mmoja, hayo ndiyo mazungumzo ambayo ni njia nzuri kwenu na kuwasaidia kukua!”

Mwonekano wa waamini na mahujaji katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Mwonekano wa waamini na mahujaji katika Uwanja wa Mtakatifu Petro

Papa alisema kuwa "Familia ya Yesu, Maria na Yosefu ni "Takatifu. Lakini tuliona kwamba hata wazazi wa Yesu hawakuelewa kila wakati. Tunaweza kutafakari juu ya hilo, na tusishangae ikiwa wakati fulani katika familia yetu hatuelewani. Haya yanapotupata tujiulize je tumesikilizana? Tunakumbana na shida kwa kusikilizana au tunajifunga kimya kimya?  wakati mwingine kwa chuki, kwa kiburi? Je, tunachukua muda wa kuongea? Kwa njia hiyo “Tunachoweza kujifunza kutoka katika Familia Takatifu leo ​​ni kusikilizana. Tujikabidhi kwa Bikira Maria na kuomba zawadi ya kusikiliza familia zetu?

Tafakari kabla ya sala 29 Desemba 2024

 

29 December 2024, 15:25