Tafuta

Mtakatifu Stefano Shemasi ni shuhuda wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kati ya Mashemasi saba waliochaguliwa na Mitume wa Yesu kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Wakristo wa kwanza. Mtakatifu Stefano Shemasi ni shuhuda wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kati ya Mashemasi saba waliochaguliwa na Mitume wa Yesu kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Wakristo wa kwanza.  (ANSA)

Sikukuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi: Toba na Msamaha Wa Dhambi!

Mtakatifu Stefano Shemasi na Shuhuda wa kwanza ni mfano bora wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; msamaha, unyenyekevu na utii mfano wa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Ni ushuhuda wa kwanza wa Kristo Yesu na Kanisa lake kati ya umati mkubwa wa waamini wanaoendelea kushuhudia mwanga katika giza la maisha ya mwanadamu hadi katika nyakati hizi. Hawa ni watu wanaojibu ubaya kwa kutenda wema! Muhimu: toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi tarehe 26 Desemba 2024 anasema mara tu baada ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Desemba, anaadhimisha Sikukuu ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shuhuda wa kwanza mbinguni, Sikukuu ambayo ina uhusiano wa pekee kabisa na Sherehe ya Noeli kwani Fumbo la Umwilisho linapata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Mtakatifu Stefano Shemasi ni shuhuda wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kati ya Mashemasi saba waliochaguliwa na Mitume wa Yesu kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Wakristo wa kwanza. Utume ambao aliutekeleza kwa muda mfupi sana, ikilinganishwa na matumaini ya Mitume wa Yesu. Mtakatifu Stefano alikuwa ni mtu mwema, mwenye kujawa na Roho, na hekima. Alitenda maajabu na ishara, kisha akafungwa. Akabahatika kuwa ni shuhuda wa Yesu pamoja na kupewa neema ya kutafakari utukufu wa Kristo Mfufuka, kiasi hata cha kutangaza Umungu wake. Kabla ya kifo chake, akajiaminisha kwa huruma na upendo wa Kristo Yesu. Rej. Mdo 6:8-12; 7: 54-60. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata katika mateso makali Stefano akathubutu kuwasamehe watesi wake, mbele ya Kristo Yesu ili asiwahesabie dhambi hii, akiisha kusema haya akalala usingizi wa amani baada ya kupigwa mawe hadi kufa!

Sikukuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shuhuda wa Imani na Matumaini
Sikukuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shuhuda wa Imani na Matumaini

Kwa ufupi sana, Mtakatifu Stefano ni mfano bora wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; msamaha, unyenyekevu na utii mfano wa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Ni ushuhuda wa kwanza wa Kristo Yesu na Kanisa lake kati ya umati mkubwa wa waamini wanaoendelea kushuhudia mwanga katika giza la maisha ya mwanadamu hadi katika nyakati hizi. Hawa ni watu wanaojibu ubaya kwa kutenda wema; watu wasiojiruhusu kutumbukia katika vita wala uwongo, lakini wanajitahidi kuvunjilia mbali mnyororo wa chuki na uhasama kwa upole wa upendo. Mashuhuda hawa wanachomoza alfariji ya Mungu katika giza la ulimwengu. Kila Mkristo anahimizwa kuwa ni shuhuda amini wa Kristo Yesu, kwa kumfuasa Kristo kama alivyofanya Mtakatifu Stefano, mfano bora wa kuigwa, kwani ni hamu ya Mwenyezi Mungu ili watu wote waweze kuokoka na kupata maisha na uzima wa milele. Rej. Yn 10:17-18; Lk 23:34. Katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya Kanisa kuendelea kuwa na mashuhuda wanaothubutu: kusali na kusamahe, kama mfano bora wa kuigwa. Kati ya watu walioombewa na Stefano alikuwepo pia kijana Sauli aliyeona na kushuhudia vyema kuuawa kwake. Lakini baadaye kwa njia ya neema ya Mungu, Sauli akatubu na kumwongokea Mungu, akageuka kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa; Mmisionari aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Paulo amezaliwa upya kwa neema ya Mungu na kwa njia ya ushuhuda wa msamaha wa Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi, kiasi kwamba, amekuwa ni mbegu ya toba na wongofu wake mwenyewe! Huu ni ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaowasindikiza na kuwaambata watu wote na kamwe hachoki kuwatafuta, kuwapokea wanapotubu na kumwongokea Mungu. Rej. Lk 15:11-32. 

Sikukuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shuhuda wa Matumaini.
Sikukuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shuhuda wa Matumaini.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema hata katika ulimwengu mamboleo, kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa kizazi hiki. Ushuhuda wao, umwilishwe katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Wajitahidi kuwa ni mwanga angavu wa Kristo Yesu katika maisha yao. Wawe na ujasiri wa kuwakumbuka na kuwaombea wakosefu na wadhambi; watu “wanao ogelea katika shida na magumu ya maisha.” Msamaha uwe ni dira na mwongozo wa maisha ya kifamilia na kijamii, kwa kuruhusu mwanga wa Kristo Yesu, uweze kuingia katika maisha yao. Msamaha wa Mtakatifu Stefano Shahidi, umeleta mageuzi makubwa katika historia ya Kanisa, umegeuza ubaya kwa kutenda wema. Hata leo hii kuna watu wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu pamoja na Injili; hawa kwa hakika ni watu wanaoshiriki katika zawadi ya wokovu kutoka kwa Kristo Yesu; kielelezo na mfano bora wa wema kwa watesi wao, mahitaji ya msamaha na wokovu kwa watu wengine. Mwenyeheri Christian de Chegè, katika wosia wake wa maisha ya kiroho anasema kwamba, mtesi wake ni rafiki wa dakika yake ya mwisho, kama ilivyokuwa kwa yule mhalifu aliyemwomba Kristo Yesu amkumbuke atakapoingia katika Ufalme wake. Rej. Lk 23:43. Kwa hakika kuna haja ya kutafuta na kuambata upendo wa Mungu unaowaokoa walimwengu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwauliza waamini ikiwa kama wanamfahamu Mwenyezi Mungi anayetaka kuwaokoa watu wote? Kwa mtakia mema hata yule anayedhani kuwa ni adui yake. Bikira Maria Malkia wa Waungama dini awasaidie waamini kuwa ni mashuhuda wenye ujasiri wa Kiinjili kwa ajili ya wokovu wa walimwengu.

Mt. Stefano Shemasi
26 December 2024, 14:44