Tafuta

Ibada ya Ufunguzi wa Lango Kuu la Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024 Ibada ya Ufunguzi wa Lango Kuu la Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024  (Vatican Media)

Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo: Ufunguzi wa Lango Kuu

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia kuhusu Habari Njema ya Wokovu, yaani kuzaliwa kwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Wachungaji wanashangazwa na kundi kubwa la Malaika wanaoimba utukufu kwa Mungu juu, kwa kuifungua mbingu na kumtoa Kristo Yesu, ili aweze kumwinua binadamu aliyeanguka na kumpeleka mikononi mwa Mungu Baba. Kristo Yesu ni tumaini la waja wake, ndiye Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi. Hili ni tukio la kiekumene!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Kanisa Katoliki kuhusu Fumbo la Umwilisho linasadiki na kufundisha kwamba: “Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu. Akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu.” Kristo Yesu alizaliwa katika utawala wa Kaisari Augusto aliyetaka iandikwe orodha ya majina ya watu wote ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024 amefungua Lango Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka 2025 Wakristo wote wanaadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Mkesha huu umehudhuriwa pia na wajumbe kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikkristo. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia kuhusu Habari Njema ya Wokovu, yaani kuzaliwa kwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Wachungaji wanashangazwa na kundi kubwa la Malaika wanaoimba utukufu kwa Mungu juu, kwa kuifungua mbingu na kumtoa Kristo Yesu, ili aweze kumwinua binadamu aliyeanguka na kumpeleka mikononi mwa Mungu Baba.

Mkesha wa Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2024: Jubilei kuu ya miaka 2025
Mkesha wa Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2024: Jubilei kuu ya miaka 2025

Kristo Yesu ni tumaini la waja wake, ndiye Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi! Huyu ndiye Mungu aliyejinyenyekesha na kuwa mdogo, Mwanga wa Kimungu unaong’aa katika giza nene la ulimwengu; Ndiye utukufu wa Mungu ulionekana ulimwenguni katika umbo la Mtoto mchanga, katika hori la kulishia wanyama, leo hii anazaliwa katika nyoyo za waja wake, tumaini hai linaloyazunguka maisha ya watu wake. Kwa kufungua Mlango wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, huo ni mwanzo wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hili ni Lango la matumaini, chemchemi ya watu wote wa Mungu. Ili kuweza kuukumbatia mshangao wa zawadi hii kubwa, waamini wanaalikwa kujiunga na wachungaji kule kondeni, kuelekea mjini Bethlehemu kwa haraka, tayari kuonja tena matumaini yaliyopotea, ndani ya kila mwamini, tayari kuyapandikiza katika nyakati na katika ulimwengu, kwa haraka huku wakivutwa na Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko wa kwenda kwa haraka, ili kumwona Mtoto Yesu aliyezaliwa, kwa ajili yao kwa moyo wa shukrani, tayari kukutana naye, ili kuwaonjesha Injili ya matumani katika medani mbalimbali za maisha. Hii ni kwa sababu matumaini ya Kikristo ni ahadi ya Mungu inayopaswa kupokelewa kwa utulivu mkubwa; bila ya kuwa wavivu, bali wakiwa na ari na moyo wa toba na wongofu wa ndani; mahujaji wanaotafuta ukweli, waota ndoto wajasiri; ndoto ya Ulimwengu mpya ambamo haki na amani vinatawala. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujifunza kutoka kwa wachungaji wa kondeni, waliokuwa na ujasiri na watu wenye uthubutu wa kuhatarisha hata maisha yao; tayari kufichua ukosefu wa haki msingi, unaohatarisha maisha ya jirani zao; kwa kuwajibika na kuonesha huruma.

Kristo Yesu ni Lango la Imani, Matumaini na Mapendo
Kristo Yesu ni Lango la Imani, Matumaini na Mapendo

Waamini wawe na ujasiri wa kuomba kupata mateso fulani katika maisha; furaha na hali ya kutoridhika. “Furaha kwa unachofanya, kutoridhishwa na ukosefu wangu wa majibu. Tafadhali ondoa amani zetu za uwongo na uweke rundo la miiba ndani ya "hori" yetu ambayo daima imejaa sana. Weka ndani ya mioyo yetu tamaa ya kitu kingine.” Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumaini ya Kikristo yanawataka kuondoka kwa haraka na kwa waamini wapate matumaini yao makubwa bila kuchelewa, kama mahujaji wa mwanga kwenye Ulimwengu unaofunikwa na giza. Maadhimisho ya Jubilei ni muda wa matumaini, ni wakati wa kutambua tena furaha ya kukutana na Kristo Yesu; mwaliko wa kupyaisha undani wao, tayari kuzama katika wongofu wa walimwengu, ili kuhakikisha kwamba, huu unakuwa ni muda kweli wa Maadhimisho ya Jubilei, kwa ajili ya dunia hii ambayo imezama katika kutafuta faida, kwa kuelemewa na umaskini; madeni makubwa yasiokuwa na haki, kiasi hata cha kuwageuza walimwengu kuwa wafungwa na watumwa wa utumwa mkongwe na utumwa mamboleo. Waamini wamepewa zawadi ili wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini pale yalipotoweka; mahali pale ambako kuwa vita; mahali ambapo watu wamepoteza matumaini; pale ambapo ndoto zimepotea; pale ambapo watu wamechoka na hawawezi tena kusimama; pale ambapo watu wamevunjika na kupondeka moyo; mahali ambapo watu wanajisikia kushindwa kusonga mbele; mateso yanayotesa nyoyo za watu; mahangaiko ya wafungwa; kwa maskini wanaoteseka kwa baridi bila kusahau maeneo ambayo yamenajisiwa kwa vita. Maadhimisho ya Jubilei ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaonjesha tena matumaini ya Injili, matumaini ya mapendo na matumaini ya msamaha wa kweli.

Kristo Yesu ni Tumaini la Waja wake.
Kristo Yesu ni Tumaini la Waja wake.

Injili na Pango la Noeli ni msaada katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, na hivyo kuwazamisha watu katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili hatimaye, kufuata ile Njia ya Msalaba kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari. Pango la Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; chemchemi ya matumaini; upendo wa Mungu unaovunjilia mbali ukaidi wa mwanadamu pamoja na hofu yake, tayari kutafakari ukuu wa matumaini yaliyo mbele ya mwanadamu. Mwelekeo huu, uwe ni mwangaza wa mapito ya kila siku ya mwanadamu. Ni katika muktadha wa usiku huu ambapo “Lango Takatifu” la Moyo wa Mungu linafunguliwa. Kristo Yesu, Mungu pamoja nasi, anazaliwa kwa ajili ya binadamu wote. Kumbe, pamoja naye, furaha ya dunia inachanua kama “maua ya kondeni.” Pamoja na Kristo Yesu, maisha yanabadilika na pamoja na Kristo Yesu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5.

Kesha la Noeli 2024

 

25 December 2024, 11:39