Kutabarukiwa Kwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano: Mama ya Makanisa Yote
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 9 Novemba 2022 anasema, kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano lililoko Jimbo kuu la Roma. Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ni Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum.” Kanisa hili liliwekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324, na kuwekwa chini ya ulinzi wa Kristo Mkombozi wa Ulimwengu, baadaye, liliwekwa pia chini ya ulinzi wa Yohane Mbatizaji na Mwinjili Yohane. Haya ni matunda ya uhuru wa kidini na kiimani uliotolewa kwa Wakristo kuabudu kadiri ya dini yao na Mfalme Costantino kunako mwaka 313. Baba Mtakatifu anayakumbuka Makanisa mahalia ambamo Jumuiya za waamini zinakusanyika kuadhimisha mafumbo ya Kimungu. Uhusiano wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na Makanisa mahalia usaidie kunogesha furaha kwa kila mwamini ili kutembea pamoja katika huduma ya Injili, sala, ushirika na kama mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo. Hili lilikuwa ni Kanisa la kwanza kujengwa mjini Roma na baadaye, kuanzia mwaka 1565 Makanisa yakaanza kujengwa sehemu mbalimbali.
Kanisa hili ndilo Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, ambalo, Baba Mtakatifu ndiye Askofu wake mkuu. Kumbe, hii pia ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi! Hii ni changamoto na mwaliko wa kujenga Kanisa hai, yaani Jumuiya ya Kikristo katika msingi ambao ni Kristo Yesu mwenyewe. Kanisa ni mahali ambapo waamini wanakusanyika kusikiliza, kutafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Baba Mtakatifu Francisko anawashauri waamini: kusoma Neno la Mungu, kulisikiliza na hatimaye, kujitahidi kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza, kwa kuandaa mahubiri kuhusiana na Maandiko Matakatifu. Kanisa ni moja: lina bwana mmoja, laungama imani moja tu, lazaliwa kwa Ubatizo mmoja, lafanywa mwili mmoja, lahuishwa na Roho mmoja, kwa ajili ya tumaini moja. Rej. Efe 4: 3-5, na katika utimilifu wote migawanyiko yote itashindwa. Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Mungu aliye Mtakatifu sana. Kanisa ni Katoliki latangaza utimilifu imani. Kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya misingi imara ya Mitume kumi na wawili. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la Kitume. Rej. KKK 866-870.
Wasomaji wa Neno la Mungu wanapaswa kuandaliwa vyema, ili waweze kulitangaza kwa ukamilifu, kama ilivyo kwa wahudumu wa Ekaristi Takatifu kwa wagonjwa na wazee parokiani. Kanisa ni mahali ambapo waamini wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na upendo kati ya watu wanaoishi nao, kwa kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaotengeneza sadaka safi na yenye kumpendeza Mungu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anawahimiza Waamini kuyalinda na kuyatunza Makanisa yao, kwani huu ni urithi na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kitamaduni na kihistoria pamoja na kutambua kwamba, hata wao wenyewe, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu wanapaswa kuwa watakatifu.