Tafuta

Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. 

Sakramenti ya Upatanisho: Chemchemi ya Huruma, Upendo na Msamaha

Kitovu cha maungamo ni upendo. Ni Yesu mwenyewe ambaye anawasubiri, anayewasikiliza na kuwasamehe waamini dhambi zao. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba: Kwenye moyo wa Mungu, binadamu anatangulia kuliko dhambi zake. Toba na wongofu wa ndani unafumbatwa katika: kufunga, sala na sadaka. Toba huleta msamaha na upatanisho kati ya: Mungu, Kanisa na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyezi Mungu, ambaye peke yake ndiye Mtakatifu na mwenye kutakatifuza, alitaka kujitwalia wanadamu wawe washiriki na wasaidizi wake, ili watumikie kwa unyenyekevu katika kazi ya kutakatifuza. Ndiyo maana mapadre huwekwa wakfu na Mungu, kwa njia ya Askofu, hivi kwamba washirikishwe kwa namna ya pekee ukuhani wa Kristo, na katika maadhimisho matakatifu watende kazi kama wahudumu wa Yule anayetekeleza bila kukoma wadhifa wake wa kikuhani kwa ajili yetu katika liturujia, kwa njia ya Roho wake. Maana wao kwa njia ya Ubatizo huwaingiza wanadamu katika taifa la Mungu; kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio huwapatanisha wakosefu na Mungu na Kanisa; kwa Mafuta ya wagonjwa huwatuliza wagonjwa; na hasa kwa adhimisho la Misa hutolea, kwa namna ya Sakramenti, dhabihu ya Kristo Yesu. Lakini wanapotoa Sakramenti zote, mapadre, kama alivyokwisha kushuhudia Mtakatifu Inyasi shahidi wakati wa Kanisa la mwanzo wameunganika kihierarkia na Askofu mahalia kwa namna mbalimbali; na hivyo wanamwakilisha katika kila kusanyiko (Congregationibus) la waamini. Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho sanjari na mang’amuzi ya miito miongoni mwa vijana Wakristo. Rej. Presbyterorum ordinis, 4.

Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Hii ni Sakramenti inayopania kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya ndani kabisa na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na ni njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Umefika wakati kwa waamini kujenga utamaaduni wa kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na utu wema sanjari na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Kitovu cha maungamo ni upendo wa Mungu ambao mwamini anaupokea na ambao anauhitaji daima. Ni Kristo Yesu mwenyewe ambaye anawasubiri, anayewasikiliza na kuwasamehe waamini dhambi zao. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba: Kwenye moyo wa Mungu, binadamu anatangulia kuliko dhambi na makosa yake. Toba na wongofu wa ndani unafumbatwa katika: kufunga, sala na sadaka. Toba huleta msamaha na upatanisho na Kanisa. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Kristo Yesu alitaka Kanisa lake lote kabisa, katika sala, maisha na utendaji wake, liwe ni ishara na chombo cha msamaha na upatanisho ambao amewastahilisha wanadamu kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Kanisa ni mhudumu wa Upatanisho. Muundo wa Sakramenti ya Upatanisho unasimikwa katika maisha ya mwamini anayeongoka kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa: kujuta dhambi, kuziungama, kutimiza malipizi na kukusudia kuacha dhambi n anafasi zake.

Ni katika muktadha huu, Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume katika barua yake kwa Mapadre waungamishaji wa Makanisa makuu ya Jimbo kuu la Roma pamoja na waungamishaji sehemu mbalimbali za dunia wakati huu wa Kipindi cha Majilio na hatimaye Sherehe ya Noeli kwa mwaka 2021, anawataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Sakramenti ya Upatanisho kwa kukazia dhana ya uponyaji wa ndani unaoletwa na Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu. Huyu ni Kristo Yesu ambaye yuko pamoja na waja wake kama chemchemi ya huruma, upendo, haki, ukweli na neema na faraja na Mkombozi wa pekee wa walimwengu. Kadiri ya Maandiko Matakatifu, Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Maandiko Matakatifu na katika Kazi ya Uumbaji na kuingia katika historia na hatimaye, kushiriki kikamilifu katika maisha ya mwanadamu. Uwapo angavu na endelevu wa Kristo Yesu katika nyakati unajionesha kwa namna ya pekee kabisa katika Neno, Sakramenti na katika Kanisa lake.

Wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho wanahimizwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kuwa ni Mkombozi pekee wa walimwengu, ili kuendelea kujikita katika: ukweli na haki; uhuru na ukombozi wa kweli kutoka kwa Kristo Yesu. Licha ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu na ambaye ana nguvu na uweza wa kusamehe na kumwokoa mtu kutoka dhambini. Rej. Mk 2: 1- 12. Mwinjili Marko anakumbusha kwamba, utume wa Kristo Yesu hapa duniani ni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njiia ya Sakramenti ya Upatanisho. Mapadre waungamishaji watambue dhamana na wajibu wao mkubwa unaowashirikisha katika ufunuo wa huruma ya Mungu, ukweli na haki. Haya na mapinduzi ya upendo wa Mungu ambaye kimsingi ndiye upendo wenyewe. Kumbe, mapinduzi ya upendo na wongofu wa upendo unafumbatwa katika Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni wongofu unaowaelekeza waamini kujielekeza zaidi katika wongofu wa kichungaji, kikanisa na kijamii. Daima Kristo Yesu anapaswa kuwa ni kiini cha wongofu huu, unaolijenga Kanisa na kuutegemeza Ulimwengu katika ujumla wake.

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume, anawahimiza Mapadre waungamishaji, kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kwa uvumilivu. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa faraja na huruma kwa watu wa Mungu wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Uwepo wao ni muhimu sana. Mama Kanisa anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Mapadre waungamishaji kwa huduma yao makini kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Mwishoni, Kardinali Mauro Piacenza anawakabidhi Mapadre waungamishaji wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Huruma ya Mungu. Anawatakia heri na baraka kwa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2021.

Sakramenti ya Upatanisho
14 December 2021, 15:35