Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wafanyabiashara Wakristo kujikita katika ubunifu kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza kazi ya uumbaji na ukombozi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wafanyabiashara Wakristo kujikita katika ubunifu kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza kazi ya uumbaji na ukombozi. 

Papa Francisko Ujumbe Kwa Wafanyabiashara Wakatoliki: Ubunifu!

Papa: Kama Wafanyabiashara Wakristo wanapaswa kujiaminisha chini ya ulinzi na maongozi ya Mungu, wajizatiti katika kipaji cha ubunifu, ili kuweza kuongeza thamani ya shughuli wanazozitekeleza. Mungu amemfundisha mwanadamu kujikita katika mchakato wa uumbaji kwa kuhakikisha kwamba, anatumia kikamilifu kipaji cha ubunifu ili kushiriki katika kazi ya uumbaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Wafanyabiashara Wakatoliki (Conferenza Internazionale delle Associazioni di Imprenditori Cattolici) ulioanzishwa kunako Mwaka 1931 ni matunda ya Maadhimisho ya Miaka 40 tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika ulimwengu mambaoleo. Huu ulikuwa ni mwanzo wa Kanisa kuangalia changamoto zilizokokuwa zinajitokeza katika medani mbalimbali za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni; ukinzani uliojitokeza kati ya mtaji na nguvu kazi na itikadi mbalimbali zilizoibuka katika kipindi cha Karne ya kumi na tisa. Kanisa lilipenda kupenyeza tunu msingi za Kiinjili ili kuitajirisha jamii, kwa kuinjilisha na kuenzi utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kubainisha haki na dhamana ya Kanisa katika masuala kijamii. Huu ni ufahamu unaopata chimbuko lake kutoka katika mwanga wa imani, ili kufundisha na hatimaye kukuza na kudumisha haki na upendo katika jamii, daima kwa kusoma alama za nyakati na kuendelea kupyaisha ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Kunako mwaka 1949, Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Wafanyabiashara Wakatoliki, ulipata sura mpya na kuwa na mwelekeo wa kiekumene na kupewa jina jipya “International Christian Union of Business Executives”, na nchi nyingi zilijiunga katika Mkutano huu, ambao kwa kifupi unajulikana kama “Unione Christiana Imprenditori Dirigenti” “UCID”. Zote hizi ni jitihada za Mama Kanisa katika kukuza na kudumisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kujikita katika kanuni maadili na utume katika masuala ya kiuchumi! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni aliwatumia wanachama wa “UCID” ujumbe wa matashi mema, akiwataka kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo katika shughuli zao. Kama Wafanyabiashara Wakristo wanapaswa kujizatiti zaidi katika kipaji cha ubunifu, ili kuweza kuongeza thamani ya shughuli wanazozitekeleza, vinginevyo, shughuli zote hizi zitahifadhiwa kwenye majumba ya makumbusho. Mwenyezi Mungu amemfundisha mwanadamu kujikita katika mchakato wa uumbaji kwa kuhakikisha kwamba, anatumia kikamilifu kipaji cha ubunifu ili kushiriki katika kazi ya uumbaji. Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuonesha ukaribu wake katika historia na maisha ya mwanadamu na kwamba, kazi ya ukombozi bado inasonga mbele.

Huu ni mwaliko kwa wafanyabiashara Wakristo kuwa wabunifu kwa kuunganisha ubunifu wao na kazi ya uumbaji iliyotendwa na Mwenyezi Mungu, ili kupata ulinzi, kinga na maongozi yake katika hatua mbalimbali za maisha na hasa wakati wa shida na changamoto za maisha! Hakuna sababu msingi za  kuogopa kukua na kuendelea kukomaa katika katika kipaji cha ubunifu, kinachopaswa kuendelezwa. Athari za maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni changamoto na mwaliko wa kushirikiana na kushikamana katika udugu wa kibinadamu, ili kwa pamoja kuweza kukivuka kipindi hiki kigumu katika historia na maisha ya mwanadamu. Uzoefu unaonesha kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa binafsi, kumbe, kuna haja ya kushikamana kwa dhati. Watu wa Mungu wanaweza kutoka katika janga hili wakiwa wamepyaishwa zaidi au wanaweza kuelemewa na ubinafsi wao na kujikita wakiwa “wanaogolea katika mawimbi mazito ya maisha.” Ni kutoka na hali na mazingira kama haya, wafanyabiashara wanayo kazi na mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Yote haya anasema Baba Mtakatifu Francisko yanahitaji ujasiri na ubunifu!

Wafanyabiashara
15 November 2021, 14:13