Tafuta

Viongozi wa Makanisa ya Kikristo wamewaandikia ujumbe washiriki wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP26 kuhusu umuhimu wa kutekeleza sera na mikakati utunzaji wa mazingira. Viongozi wa Makanisa ya Kikristo wamewaandikia ujumbe washiriki wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP26 kuhusu umuhimu wa kutekeleza sera na mikakati utunzaji wa mazingira. 

Ujumbe wa Viongozi wa Makanisa kwa Mkutano wa COP26 Glasgow

Viongozi wa Makanisa wanagusia kuhusu madhara ya UVIKO-19, umuhimu wa kushikamana, kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na njili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wanakazia zaidi kuhusu umuhimu wa utunzaji endelevu wa mazingira nyumba ya wote; madhara ya uchafuzi wa mazigira kwa maskini pamoja na dhamana na wajibu wa kulinda na kutunza mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican. 

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland, kuanzia tarehe Mosi Novemba hadi tarehe 12 Novemba 2021 unafanikiwa. Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC ambao unajumuisha michango na ahadi zilizowekwa kitaifa na nchi mbalimbali kama hatua madhubuti za kupunguza athari za ongezeko la kiwango cha joto duniani unapaswa kutekelezwa kama ilivyokubaliwa. Kiwango cha wastani wa nyuzi joto 1.5C ndicho kinachotakiwa vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inakabiliana na janga kubwa la uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe, changamoto ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 45% ifikapo mwaka 2030 ni muhimu sana. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kuna haja ya kutekeleza kwa vitendo upunguzaji wa nyuzi joto 1.5C kama ilivyobainishwa kwenye Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi.

Kila nchi itaamua kiwango cha mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kiwango hicho kitategemea uchumi wa nchi husika na pia kiasi cha uzalishaji wa gesijoto. Kuongeza uwekezaji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa angalau asilimia 50% ya fedha za jumla za ufadhili wa umma wa mabadiliko ya tabianchi. Makanisa kuanzia tarehe 1 Septemba hadi 4 Oktoba yanaadhimisha Kipindi cha Kazi ya Uumbaji Kiekumene. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuungana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli pamoja na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani kutoa ujumbe katika maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji. Ujumbe huu unaelekezwa zaidi kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa watakaoshiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland.

Viongozi wa Makanisa wanagusia kuhusu madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, umuhimu wa kushikamana, kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, kwa kuchagua mtindo bora zaidi wa maisha, ili kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Huu ni wakati muafaka wa kusikiliza na kujibu “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini.” Wanakazia zaidi kuhusu umuhimu wa utunzaji endelevu wa mazingira nyumba ya wote; madhara ya uchafuzi wa mazigira kwa maskini pamoja na dhamana na wajibu wa kushirikiana na kushikamana kwa pamoja. Viongozi wa Makanisa wanakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira ni jambo muhimu na mahali pa kuanzia hata katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kimazingira kama mbinu mkakati wa kumwangalia binadamu katika familia kubwa ya binadamu. Uchafuzi na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote ni matokeo ya; uchoyo na ubinafsi; uchu wa mali na faida kubwa kwa kipindi cha muda mfupi. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yamapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na matokeo yake yanaanza kuonekana.

Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa Kiikolojia kwa kuonesha ukarimu zaidi kutokana na mtindo wa maisha, jinsi ya kufanya kazi pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali fedha. Uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote umewatumbukiza watu wengi katika umaskini kutokana na: Uharibifu wa bayoanuai, madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa ni sehemu ya kazi ya mikono ya wanadamu. Waathirika wa majanga haya wengi wao ni maskini. Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini kinahitaji kusikilizwa kwa makini na kupewa majibu muafaka kwa wakati huu. Kuna madhara makubwa kutokana na mafuriko sehemu mbalimbali za dunia; ongezeko la kina cha bahari kinachotishia maisha ya watu na makazi yao; athari za vimbunga pamoja na ukame wa kutisha. Mambo yote haya yanachangia pia hata katika ukosefu wa usalama wa chakula duniani. Binadamu anapaswa kutambua kwamba, anashiriki katika kazi ya uumbaji.

Viongozi wa Makanisa wanakazia umuhimu wa ushirikiano na mshikamao wa udugu wa kibinadamu, ili kuweza kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali fedha, kwani kinyume chake, kimepelekea uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka; kuboromoka kwa afya, ulaji wa kupindukia sanjari na madhara mengine ya kiuchumi na kijamii; mambo ambayo yana mwingiliano wa pekee kabisa! Kumbe, kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa ndani wa ndani ili kuleta mabadiliko; kwa kujikita katika upendo, haki na huruma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watu wajenge utamaduni wa kuwajibika kama mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake na hivyo kuvunjilia mbali kuta zinazowatenganisha watu. Kwa mara ya kwanza katika historia, Viongozi wakuu wa Makanisa, wanaungana kwa pamoja ili kuragibisha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba wote sanjari na mapambano dhidi ya umaskini. Huu ni mwaliko wa kuchagua na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linauliza swali msingi, Je, Mazingira ni nyumba ya wote? Ni wakati wa kupyaisha Oikos “οἶκος” yaani nyumba ya Mungu kwa kujikita katika ikolojia endelevu. Kwa kusimamia uchumi shirikishi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Juhudi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto ya kiekumene na kidini inayofumbatwa katika upendo wa dhati. Changamoto na mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini duniani. Kipaumbele cha kwanza ni kwa ajili ya watu wa Mungu wanaoishi vijijini na kwenye mazingira magumu na hatarishi. Ili kuweza kufanikisha yote haya kunahitajika kipaji cha ubunifu na sera na mikakati ya siasa inayokita mizizi yake katika upendo!

Kanisa na Mazingira
04 October 2021, 15:30