Maadhimisho ya Juma la 49 La Wakatoliki wa Italia Kijamii: Yaliyojiri
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mwenyeheri Professa Giuseppe Toniolo, Baba wa Familia, Jaalimu wa siasa za kiuchumi toka Chuo kikuu cha Pisa, mwamini makini aliyeacha harufu ya utakatifu katika maisha ya kijamii nchini Italia ndiye Muasisi wa Maadhimisho ya Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii, ambalo kwa Mwaka 2021 limeingia katika awamu yake ya 49 tangu kuanzishwa kwake: Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii kuanzia tarehe 21-24 Oktoba 2021 limenogeshwa na kauli mbiu:"Sayari tunayotarajia. Mazingira, Kazi, Siku zijazo. Kila Kitu Kimeunganishwa." Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa maadhimisho haya ambayo yamefanyika baada ya wimbi kubwa la janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 anasema hakuna sababu ya kukata tamaa, bali huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watu ambao wamechoka kuishi katika mazingira machafu; wanaoendelea kunyonywa na kudhalilishwa; watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa kwa rushwa, ufisadi na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote! Watu wa Mungu nchini Italia wanahamu ya kutaka kuendelea kuishi, wana kiu ya haki, ustawi na maendeleo fungamani.
Kuna haja ya kuwa makini katika kipindi hiki cha mpito kutoka kwenye janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna watu wamelazimika kuikimbia nchi, wamepoteza fursa za kazi; kuna ongezeko kubwa la maskini, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Watu wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Wote hawa wanapaswa kusikilizwa na kuhudumiwa! Baba Mtakatifu Francisko anawasihi watu wa Mungu nchini Italia, kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kujikatia tamaa; tayari kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Maendeleo ya teknolojia ya kweli hayana budi kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watu, mahitaji yao msingi pamoja na mazingira! Rej. Laudato si 194. Kuna umuhimu wa kufanya wongofu wa kiutu, kiroho na kiikolojia, ili kufikia wongofu wa kiikolojia kijamii, ili hatimaye kuunda mifumo mipya ya kijamii na kiuchumi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu! Kuna haja ya kujenga utamaduni wa majadiliano, haki na amani; kwa kuzingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!
Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika mahubiri ya kufunga Maadhimisho ya Juma 49 la Wakatoliki wa Italia Kijamii, tarehe 24 Oktoba 2021 amesema, bado kuna haja ya kusimama na kusikiliza kilio cha watu wa Mungu nchini Italia, kwa kukazia umuhimu wa kutengeneza fursa za ajira, kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa pamoja na kuwahakikishia wananchi afya bora. Kuna haja ya kuzingatia ikolojia msingi kwa vile kila kitu kinahusiana na kingine; na matatizo ya leo yanahitaji mtazamo unaozingatia kila sehemu ya mgogoro wa ulimwengu. Kumbe, ikolojia ya mazingira na kiuchumi inapaswa kuangaliwa katika mapana yake. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa ni nyenzo msingi katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na ujenzi wa uchumi shirikishi.
Mfumo wa uchumi mpya unahitaji mtindo mpya wa kijamii unaofumbatwa katika: udugu wa kibinadamu, mshikamano, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, matumizi sahihi ya rasilimali na utajiri wa dunia. Vijana wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa udugu wa kinibadamu kama sehemu ya mchakato wa ufufuaji wa uchumi duniani. Masomo na vitendo vioneshe kwa dhati kwamba, uchumi mbadala inawezekana. Kamwe vijana wasikate wala kukatishwa tamaa, bali waongozwe na upendo wa Injili, chemchemi ya mageuzi yote ya kiuchumi, kwa kuingia na kuzama ndani ya madonda ya historia ya mwanadamu ili hatimaye, kufufuka tena. Vijana wajenge utamaduni wa kusikiliza kilio cha maskini kwa kuwashirikisha katika ujenzi wa mustakabali wa wengi.
Rais Sergio Mattarella wa Italia katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anakiri kwamba ni mchango mkubwa katika ujenzi wa mshikamano wa kitaifa, ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa uchumi fungamani, unaotoa kipaumbele cha pekee kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwa namna ya pekee ulinzi wa uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika mustakabali wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Italia. Kuna mwingiliano mkubwa kati ya mazingira, kazi pamoja na ustawi wa kiikolojia na kijamii. Maendeleo ya kweli hayana budi kujikita katika ukuaji wa uchumi, matumizi sahihi ya rasilimali na utajiri wa dunia hii. Maendeleo ya kweli yasaidie kuibua sera bora zaidi za kupambana na umaskini; uwiano sahihi wa mazimgira, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rasilimali jamii inapaswa kukuzwa na kuendelezwa zaidi na kwa namna ya pekee, kuna haja ya kuwekeza katika rasimali watu na wala si vitu!