Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Radio Cope asema hana mpango wa kung'atuka kutoka madarakani kwa sasa licha ya uvumi uliozagaa kwenye mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Radio Cope asema hana mpango wa kung'atuka kutoka madarakani kwa sasa licha ya uvumi uliozagaa kwenye mitandao ya kijamii. 

Baba Mtakatifu Francisko Asema Hana Mpango wa Kung'atuka!

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu afya yake jinsi ambavyo wauguzi kwa mara mbili wameokoa maisha yake! Machafuko ya kisiasa nchini Afghanistan, Uhusiano kati ya Vatican na China; Kifo laini na mchakato wa mageuzi unaoendelea kufanyika kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hajawahi hata siku moja, kuwazia kung’atuka kutoka madarakani! Uvumi

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amefanya mahojiano maalum na Bwana Carlos Herrera wa Radio COPE kwa lugha ya Kihispania mara baada ya kulazwa kwenye Hospitali ya Gemelli iliyoko mjini Roma kwa ajili ya kufanyia operesheni kubwa kwenye utumbo mpana. Operesheni hii ilifanywa na Prof. Sergio Alfieri. Katika mahojiano haya, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu afya yake jinsi ambavyo wauguzi kwa mara mbili wameokoa maisha yake! Machafuko ya kisiasa nchini Afghanistan, Uhusiano kati ya Vatican na China; Kifo laini na mchakato wa mageuzi unaoendelea kufanyika kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anasema, baada ya kufanyiwa operesheni kwenye utumbo mpana, hajawahi hata siku moja, kuwazia kung’atuka kutoka madarakani. Hivi karibuni, kumekuwepo na uvumi kwenye vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa anajiandaa kung’atuka kutoka madarakani! Ni jambo la kawaida pale Khalifa wa Mtakatifu Petro anapokuwa mgonjwa, mawazo ya watu wengi ni Tsunami ya “Conclave”, yaani mkutano wa Baraza la Makardinali ili kumchagua Khalifa mwingine wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wauguzi ambao kwa mara mbili wameokoa maisha yake. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1957, alipokuwa bado Seminarini akapata ugonjwa wa mapafu na kuokolewa na mtawa mmoja. Mara ya pili ni Julai 2021 baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, akalazwa kwenye Hospitali ya Gemelli. Anakula vizuri, anaendelea na matibabu baada ya operesheni na kutekeleza vyema majukumu yake ya kila siku. Baba Mtakatifu anajiandaa kushiriki katika Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko atashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa.  Baadaye, atafanya hija ya kitume nchini Slovakia, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021. Baba Mtakatifu anasema, hija yake ya kitume nchini Slovakia ni kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano hili la Kimataifa. Atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Kanisa. Daima anapenda kusoma alama za nyakati na kusema kile kinachotoka katika undani wa moyo wake! Afghanstan kwa sasa imetumbukia katika machafuko ya kisiasa ni matumaini yake kwamba, diplomasia ya Vatican chini ya Kardinali Pietro Parolin itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake, lakini pia ni wajibu wa waamini kusali, kufunga na kufanya toba ili kukimbilia: upendo, huruma na msamaha wa Mungu katika maisha ya waja wake.

Wananchi mahalia wajengewe uwezo wa demokrasia kadiri ya mazingira na tamaduni mahalia na kamwe si kutoka nje ya nchi. Kuteleza na kuanguka dhambini ni sehemu ya udhaifu wa binadamu, kusimama, kutubu na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ni mwanzo wa mchakato wa utakatifu wa maisha. Hata katika maeneo ya Vatican, Shetani, Ibilisi anapitapita akitafuta mawindo kama ambavyo Kristo Yesu anasimulia katika Maandiko Matakatifu. Waamini wamwogope Shetani, Ibilisi anayebisha hodi katika malango ya nyoyo zao. Baba Mtakatifu anasema mwezi Machi 2022 ataadhimisha Miaka tisa tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Wakati wote amekuwa akitekeleza maazimio yaliyotolewa na Baraza la Makardinali kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, jinsi ya kutekeleza maazimio haya ni mchango wake katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” uliochapishwa tarehe 24 Novemba 2013, anatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo Yesu ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wosia huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za mbeleni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Wosia huu wa kitume unachota utajiri wake kutoka katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anakazia mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani, inayotangazwa na kumwilishwa katika matendo kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana na wajibu wa waamini wote. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wanashiriki: ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo Yesu, kumbe, wote ni wafuasi wamisionari wanaopaswa kushiriki kikamilifu katika matendo ya kiibada kama nguvu ya uinjilishaji. Waamini watumie karama na vipaji mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano unaoinjilisha na kutamadunisha; kwa kuzingatia fikra na elimu makini! Baba Mtakatifu anatoa kipaumbele cha pekee kwa mahubiri kama muktadha wa kiliturujia unaotoa nafasi kwa Mama Kanisa kuongea na watoto wake kutoka katika sakafu ya maisha na nyoyo zao. Kwa njia hii, mahubiri yanapaswa kuwasha moto wa imani, matumaini na mapendo kwa wale wanaosikiliza, ili hatimaye, waweze kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao, kielelezo makini cha imani tendaji. Wakleri ambao wanashiriki kwa namna ya pekee kazi ya: kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu, wanapaswa kuandaa vyema mahubiri yao kwa kuzingatia heshima kwa ukweli wanaoutangaza na kuushuhudia; kwa kumwilisha Neno katika maisha yao, ili kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Wakleri wajitahidi kuboresha mahubiri yao kwa kutumia nyenzo mbalimbali zilizowekwa na Mama Kanisa kama vile masomo ya maisha ya kiroho na tafakari kutoka kwa Mababa wa Kanisa. Wahubiri wawe makini kusoma alama za nyakati, ili mahubiri yao, yaweze kuwasaidia waamini, daima wakichota utajiri na amana ya Neno la Mungu, kama sehemu ya mchakato makini wa uinjilishaji mpya unaotumia hata vyombo vya mawasiliano ya jamii, kuhakikisha kwamba, cheche za Neno la Mungu zinawafikia watu wengi zaidi!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, rushwa na ufisadi wa mali ya Kanisa ni kashfa ambayo imeendelea kuchafua maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu aliamua kumvua Kardinali Angelo Becciu nyadhifa zake, ili kuimarisha mchakato wa haki mjini Vatican. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa kupyaisha sheria, kanuni na taratibu sanjari na kuwateua Majaji na waendesha mashitaka wapya. Inasikitisha sana kuona watu wanakula rushwa ndani ya Kanisa! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sheria, taratibu na kanuni zilizoundwa zitasaidia kukuza na kudumisha haki, ustawi na maendeleo ya wengi. Kardinali Angelo Becciu amekuwa ni msaidizi wake wa karibu na kwamba, amemsaidia kwa mambo mengi katika maisha na utume wake na kwamba, hadi wakati huu anamwona hata hatia hadi pale kesi yake itakapokuwa imefikia hukumu kwa ukweli kufahamika na haki kutendeka!

Baba Mtakatifu Francisko, anasema, tarehe 16 Julai 2021 alichapisha Barua Binafsi: Kuhusu Liturujia “Motu Proprio “Traditionis custodes” yaani Walinzi wa Mapokeo ya Kanisa: Juu ya Matumizi ya Liturujia ya Kirumi Kabla ya Mageuzi ya Mwaka 1970. “Sheria Mpya Kuhusu Ibada ya Misa Takatifu", Maaskofu mahalia wanawajibika zaidi.” Makundi ya waamini yanayotumia “Missale Romanarum” yaani Misale ya Kirumi ya Mwaka 1962 iliyorekebishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI miaka 14 iliyopita imefanyiwa marekebisho na Baba Mtakatifu Francisko na anatoa sababu msingi zilizompelekea kuandika Barua Binafsi “Motu Proprio “Traditionis custodes” yaani Walinzi wa Mapokeo ya Kanisa: Juu ya Matumizi ya Liturujia ya Kirumi Kabla ya Mageuzi ya Mwaka 1970. Papa Francisko anasema, ni wajibu wa Askofu mahalia kuhakikisha kwamba hata makundi ya waamni yanayotumia misale hii kuyatambua na kuheshimu mabadiliko ya Kiliturujia yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kadiri ya mwanga angavu wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium”. Tangu sasa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa kufuata Misale ya Kirumi ya zamani, hayataruhusiwa tena kuadhimishwa kwenye Parokia. Utakuwa ni wajibu wa Askofu mahalia kupanga Kanisa na siku ambamo Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa. Masomo ya Ibada ya Misa Takatifu yanapaswa kuwa ni katika lugha ya watu mahalia iliyopitishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki husika. Kiongozi mkuu wa Ibada atakuwa ni yule aliyeteuliwa na kutumwa na Askofu mahalia. Maadhimisho haya yawe ni kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu katika barua yake kwa familia ya Mungu nchini Ujerumani, anawasihi Maaskofu kushikamana na kutembea kwa pamoja kama ndugu na kamwe asiwepo mtu anayetembea pweke pweke, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Roho Mtakatifu, aweze kupyaisha maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani. Sinodi ya Maaskofu Katoliki Nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hiki ni kipindi cha mabadiliko makubwa yanayoibua matatizo na changamoto mpya na zile za zamani, mwaliko kwa familia ya Mungu kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anatambua hali ngumu ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani, ndiyo maana ameamua kuwaandikia ujumbe huu, ili kuunga mkono jitihada zinazoendelea kufanyika hadi wakati huu! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kama ambavyo imeshuhudiwa wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani uliofanyika mwezi Machi 2019.

Mkutano huu uliwajumuisha: Maaskofu, wakleri, watawa, wajumbe kutoka kwa waamini walei, wataalam na mabingwa wa mambo mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Wote hawa kwa pamoja wakajadili na hatimaye kupitisha mbinu mkakati wa kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Ujerumani. Umuhimu wa utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani ni matunda ya utafiti na upembuzi yakinifu uliofanywa na Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, DBK, inayowahusisha wawakilishi wa makundi mbali mbali ya familia ya Mungu nchini Ujerumani. Tume hii pamoja na mambo mengine, ilidadavua kwa kina na mapana kuhusu uwepo wa idadi kubwa ya waamini wenye umri mkubwa ndani ya Kanisa Katoliki, ikilinganishwa na idadi ya vijana wanaobatizwa kila mwaka. Tume hii ilipembua pia kuhusu kupungua kwa idadi ya miito ya kitawa na kipadre nchini Ujerumani, mafundisho tenge kuhusu tendo la kujamiiana au kama wanavyofahamu wengi, tendo la ndoa. Tume iligusia pia hali na mtindo wa maisha na utume wa Mapadre nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu anasema, hana sababu msingi ya kuzama tena katika tafiti hizi, bali anapenda kujielekeza zaidi kwa kuchangia hoja zake katika maisha ya kiroho zaidi, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya. Kumbe, kipaumbele cha kwanza katika majadiliano haya yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kilenge kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa nchini Ujerumani. Familia ya Mungu nchini Ujerumani iendelee kujiweka chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu kwani historia inafundisha kwamba, pale ambapo Jumuiya ya waamini ilijiangalia yenyewe na kutaka kutatua matatizo na changamoto zake kwa kutumia nguvu zake yenyewe; mbinu na akili zake, imejikuta ikikuza na kuendeleza matatizo yaliyokuwa yanapaswa kupewa ufumbuzi wa kudumu.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi la Miaka 160 tangu kuanzishwa kwa Gazeti la L’Osservatore Romano na Miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Radio Vatican, Jumatatu tarehe 24 Mei 2021 alitembelea Jumba la Mawasiliano ya Vatican. Hii ilikuwa ni fursa ya kukutana na kuzungumza na wafanyakazi mmoja baada ya mwingine sanjari na kubadilishana nao maneno “mawili, matatu”. Baba Mtakatifu alitembelea Idara ya Ufundi na Teknolojia. Hapa ni mahali ambapo kuna wataalam wa teknolojia ya mawasiliano wanapofanyia shughuli zao, ili kuhakikisha kwamba, kile kinachozalishwa na L’Osservatore Romano, Radio Vatican, Kituo cha Televisheni cha Vatican pamoja na Wavuti ya Vatican kinawafikia walengwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, vyombo vya mawasiliano ya jamii mjini Vatican vinapaswa kusoma alama za nyakati, ili kutambua mahitaji ya wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wake. Hili ni Baraza lenye wafanyakazi wengi zaidi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican na linaongozwa na mwamini mlei. Changamoto hizi zimevisaidia sana vyombo vya mawasiliano mjini Vatican kujipanga vizuri zaidi ili kukabiliana na changamoto mamboleo.

Kashfa ya Nyanyaso za Kijinsia Ndani ya Kanisa: Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Kardinali Sean Patrick O'Malley, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Boston, Marekani ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Makardinali Washauri lililoundwa na Baba Mtakatifu Francisko ili kumsaidia kupata ushauri wa kufanya mageuzi ndani ya Kanisa. Ni kiongozi wa Kanisa aliyesimama kidete kupambana na nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Jamii inapaswa pia kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia zinazotumia picha za utupu! Inasikitisha kuona kwamba, hata kuna baadhi ya Serikali zinazoruhusu kuchapishwa na hata kutangazwa hizi picha za utupu!

Laudato si: Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiikolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya mafao ya watu wote duniani. Mabadiliko ya tabianchi ni janga la kimataifa anasema Baba Mtakatifu Francisko, kama ilivyo pia haki ya maji safi na salama; yanayopaswa kutunzwa vyema kwani ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kwa ajili ya wote na kwamba, haki hii inaambata utu wa mwanadamu. Kiini cha yote haya anasema Baba Mtakatifu ni kutunza utofauti unaojitokeza katika bayianuai kwani kutokana na utunzaji mbaya wa mazingira kila mwaka kunatoweka jamii za mimea na za wanyama, ambazo kamwe watoto wetu hawataziona tena.

Mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, urithi wa pamoja unaopaswa kutunzwa na wala si kuharibiwa, kwani ni amana ya binadamu wote. Utunzaji wa viumbe hai unapaswa kusindikizwa na wema na wajibu kwa ajili ya binadamu. Ndiyo maana hapa anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi na matumizi binafsi yanapaswa kuzingatia kwanza kanuni hii. Mapokeo ya Kikristo yanakazia kwa namna ya pekee mwelekeo wa kijamii zaidi kuliko masuala binafsi. Baba Mtakatifu anasema, masuala ya kisiasa na kiuchumi hayana budi kupata mwelekeo mpana zaidi badala ya kujikita katika sera zinazotaka kupata mafanikio ya muda mfupi kwa ajili ya chaguzi. Mchakato wa maamuzi makubwa kwa ajili ya mafao ya wengi hauna budi kujikita katika ukweli na uwazi pamoja na kusimama kidete kupambana na rushwa pamoja na ufisadi na mafao binafsi; mambo ambayo yana madhara makubwa katika jamii. Sera na mikakati ya kiuchumi ijikite katika kanuni maadili na masuala ya fedha yasimamiwe kwa kuzingatia ubora wa maisha ya watu. Wanaharakati mbalimbali wanapaswa kujielekeza katika utunzaji wa mazingira, utetezi wa maskini na ujenzi wa mtandao wa mshikamano unaosimikwa katika heshima na udugu. Umuhimu wa elimu na majiundo ya kweli ya mwanadamu kama moja ya changamoto kubwa katika nyakati hizi.

Hapa kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya wa mtindo wa maisha, kwani binadamu bado ana uwezo wakufanya marekebisho makubwa katika maisha yake katika mchakato wa ujenzi wa nyumba ya wote. Hapa kuna haja ya kuanza na mambo ya kawaida katika utunzaji wa mazingira kwa kutofautisha ukusanyaji wa taka, kuwa na matumizi bora ya maji, taa na viyoyozi, lakini zaidi kwa kuondokana na masuala ya uhalifu na ubinafsi, ili kujenga utamaduni wa kuwa na kiasi. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Mkutano wa 26 wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 utafanyika kuanzia tarehe 1-12 Novemba 2021 huko mjini Glasgow nchini Scotland. Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna maafa na majanga makubwa yanayotokana na ukame wa kutisha, mafuriko pamoja na majanga ya moto sehemu mbalimbali za duniani. Matokeo yake ni watu wengi kuanza kunyemelewa na baa la njaa na utapiamlo. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, tangu mwaka 2007 amekuwa na uelewa mpana zaidi kuhusu umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kutokana na kujifunza pamoja na kuangalia athari zake! Baba Mtakatifu anatarajia kuhudhuria mkutano wa COP26 huko mjini Glasgow nchini Scotland.

Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya China na Vatican: Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China, ulitiwa saini tarehe 22 Septemba 2018 kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia. Lengo la Vatican ni kuwapata wachungaji bora watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko akashuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi. Mkazo ni kuhusu shughuli za kichungaji na kitume, ili kuwawezesha waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato huu pamoja na mambo mengine unapania kukoleza: imani na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu. Uteuzi wa Maaskofu kwa ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya China ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini China na kwamba, huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa halina budi kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano unaofumbatwa katika ushuhuda wa uvumilivu kama ilivyo pia katika majadiliano ya kidini.

Utamaduni wa Kifo: Sera za utoaji mimba na Kifo laini: Baba Mtakatifu anaendelea kuwakumbusha waamini kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama waamini wanaitwa na kuhamasishwa kulinda, kuitunza na kuidumisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu, hata pale watu wanapokumbana na magonjwa pamoja na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Hakuna mwenye haki ya “kufyekelea mbali zawadi ya maisha ya binadamu”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, uhai wa binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa na kwa njia hii, kuweza kutangaza na kushuhudi tunu msingi za maisha ya Kikristo katika mazingira ya kifamilia. Kila huduma ya matibabu inayotolewa kwa mgonjwa iwe ni chemchemi ya huruma na upendo kwa wagonjwa wanaoteseka. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya mwanadamu yanapaswa kuwa kweli ni chombo cha huduma kwa wagonjwa na wala si vinginevyo. Kamwe mgonjwa asionekane kuwa ni mzigo mzito, kiasi cha kuanza kuhalalisha kisheria mchakato wa kifolaini. Kwa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu, jambo hili linaweza kuonekana kuwa kama sehemu ya uhuru wa mtu binafsi; lakini ndani mwake, uhuru huu unafumbata ubinafsi unao thubutu kupima: haki, heshima na utu wa mtu kutokana na umuhimu wake. Kifolaini hakumsaidii mtu kumpunguzia maumivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, umefika wakati wa kusimama kidete kupinga utamaduni na utandawazi usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini, ni hatari kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee hata nchini Hispania badala ya sera na mikakati inayopania kuwagawa watu.

Wakimbizi na Wahamiaji: Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati, ili kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Baba Mtakatifu anazipongeza nchi ambazo zimewapokea wakimbizi na wahamiaji na kuanza kuwapatia huduma msingi za elimu, afya pamoja na fursa za ajira.

Umoja wa Jumuiya ya Ulaya: Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa nchi wanachama wa Umoja wa Jumuiya ya Ulaya kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, wanautegemeza umoja huu, ili usije kusambaratishwa na watu wenye misimamo mikali kuhusu utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko pamoja na watu wanaojitafutia umaarufu. Umoja wa Ulaya hauna budi kupyaishwa ili uweze kusonga mbele bila ya kuvurugwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu anasema, mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na waasisi wa Umoja wa Ulaya hapo tarehe 25 Machi 1957, walijiwekea sera na mikakati ya kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, lakini hasa kwa kuwekeza katika ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu. Walitaka kulinda na kudumisha uhai, udugu na haki, kama chachu muhimu sana ya mabadiliko Barani Ulaya, baada ya patashika nguo kuchanika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Jumuiya ya Ulaya itaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama itaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya. Mwaka 2022, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipohutubia Jumuiya ya Umoja wa Ulaya akionesha umuhimu wa kukuza na kudumisha utambulisho wake.

Mtazamo wa Kikristo Kuhusu Michezo: Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika medani mbalimbali za maisha ili kufikia lengo linalotarajiwa. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha kwa kuhakikisha kwamba, kila mtu anajitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaobomolea mbali kuta za tabia ya ubinafsi, uchoyo na ubaguzi na kuwakirimia watu wa Mungu ile furaha ya moyoni! Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Ujasiri, Sadaka na Udumifu ni mambo msingi katika michezo. Mama Kanisa amekuwa akiwahimiza wanamichezo kujenga na kudumisha: umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Michezo ni shule ya maisha ya mwanadamu; mahali pa kujifunza Heri za Mlimani daima waamini wakijibidiisha kutafuta taji ya utukufu wa mbinguni. Mababa wa Kanisa wamekuwa wakiwahimiza wanamichezo kushindana kwa kuzingatia: ukweli, haki, amani na utulivu wa ndani, kwani michezo ni furaha, ili kuwawezesha wanamichezo kuwa na afya njema. Baba Mtakatifu Francisko anasema si mshabiki sana wa michezo, katika ujana wake alipenda zaidi kuwa ni mlinda mlango. Lakini kadiri anavyoendelea kuishi kati ya mashabiki wa mpira wa miguu hasa nchini Italia, anaendelea kujifunza mengi, kwani elimu haina mwisho!

Papa Mahojiano Cope
01 September 2021, 15:48