Nia za Baba Mtakatifu Francisko Mwezi Septemba 2021: Mazingira!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Septemba 2021 anatoa mwaliko kwa waamini kusali, ili wote waweze kuchagua kwa ujasiri maisha rahisi na endelevu kwa mazingira, huku wakifurahi pamoja na vijana ambao wamejitosa kusimama kidete kulinda mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anafurahia kuwaona vijana wakiwa na ujasiri wa kuanzisha miradi kwa ajili ya utunzaji bora wa wa mazingira na maboresho ya kijamii; kwa sababu mambo haya mawili yanategememeana. Watu wazima wanaweza kujifunza mengi kutokana kwa vijana wa kizazi kipya kwa sababu wao wako mstari wa mbele. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya tafakari kuhusu mtindo wao wa maisha na hususan katika kipindi hiki chenye migogoro ya kiafya, kijamii na kimazingira. Ni wakati wa kutafakari kuhusu mtindo wao wa ulaji na matumizi ya vitu; jinsi wanavyosafiri au jinsi wanavyotumia maji, nishati, vyombo vya plastiki pamoja na vitu vinginevyo vingi, ambavyo mara nyingi ni hatari kwa sayari ya dunia! Watu wanapaswa kuchagua kubadilika. Watu wazima wasonge mbele huku wakiwa wameambatana na vijana, kuelekea kwenye mitindo ya maisha ambayo ni rahisi zaidi na yenye kuheshimu mazingira.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujizatiti katika sala, ili wote waweze kufanya maamuzi jasiri na muhimu kwa ajili ya kudumisha maisha endelevu ya mazingira; kwa kuhamasishwa na vijana wa kizazi kipya ambao wamejitosa kwa ajili ya kutunza mazingira. Vijana hawa si wajinga anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa sababu wanajizatiti kikamilifu kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Ndiyo maana vijana wa kizazi kipya wanataka kubadili kile watakachokirithi wakazi ambapo wazee wa sasa hawatakuwepo! Kwa ufupi kabisa, Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Septemkba 2021 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kuhusu mtindo wa maisha yao, kwa kuangalia kwa kina na mapana ni jinsi gani wanavyotumia rasilimali na utajiri wa Dunia Mama, ili kuanza kujikita katika mchakato wa mabadiliko yanayokita mizizi yake katika uwajibikaji, utunzaji, heshima, urahisi pamoja nidhamu. Binadamu amechangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, hali inayowatumbukiza watu wengi katika hali ya umaskini, njaa na magonjwa.
Bayianuai ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya ikolojia. Kumbe, kuna haja ya kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa kwa kulinda asilimia 30% ya dunia kama hifadhi maalum hadi kufikia mwaka 2030, ili kuondokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na kupotea kwa bayianuai. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uchafuzi wa mazingira sanjari na upotevu wa bayianuai, hali ambayo inawaathiri watu zaidi ya bilioni 3.2 sawa na asilimia 40% ya Idadi ya watu wote duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anakaza kusema, kwa muda mrefu watu wamejihusisha na ukataji ovyo wa miti; wamechafua vyanzo vya maji sanjari na kuharibu ardhi kiasi hata cha kusahau. Mwanadamu amechangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa mazingira na matokeo yake kwa sasa yanajionesha kwenye jamii ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” anasema vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinahusishwa moja kwa moja na maisha ya mwanadamu pamoja na shughuli zake. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na nafasi ya mwanadamu ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ili kulinda na kuhifadhi Injili ya Mazingira.
Kwa upande wake Padre Frèderic Fornos, SJ., Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote inapaswa kufanyiwa kazi mara moja. Kipeo cha ikolojia kinahitaji mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha pamoja, umoja na mshikamano na udugu kibinadamu, ili kupata ikolojia fungamani na endelevu. Huu ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ujasiri wa vijana wa kizazi kipya ulete hamasa katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!