Tafuta

Papa Francisko akutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Hungaria: Mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; utunzaji wa mazingira na familia. Papa Francisko akutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Hungaria: Mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; utunzaji wa mazingira na familia. 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa: Viongozi wa Serikali

Papa amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Hungaria Katika mazungumzo yao pamoja na mambo mengine wamegusia kuhusu: utume wa Kanisa nchini Hungaria; Umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wamekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia! Viongozi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya 34 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Slovakia inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu anafanya hija hii baada ya kuhitimisha kwa Ibada ya Misa Takatifu Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) yaliyozinduliwa na Kardinali Angelo Bagnasco, Jumapili tarehe 5 Septemba 2021 huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu alipowasili nchini Hungaria, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa nchi. Katika mazungumzo yao ya faragha pamoja na mambo mengine wamegusia kuhusu dhamana na utume wa Kanisa nchini Hungaria; Umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wamekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Mkutano huu, umehudhuriwa pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican.

Akiwa njiani kuendelea Budapest, Hungaria, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya “kuchonga na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Amemtambulisha Monsinyo George Jacob Koovakad aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Mratibu mkuu wa Safari za Baba Mtakatifu kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Amemshukuru Monsinyo Guido Marini ambaye kwake hii ni safari ya mwisho kama Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Agosti 2021 amemteua Monsinyo Guido Marini (56) kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki laTortona, nchini Italia. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Guido Marini alikuwa ni Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Guido Marini alizaliwa tarehe 31 Januari 1965 huko Genoa, Kaskazini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 4 Februari 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na Kardinali Giovanni Canestri. Baba Mtakatifu ameishukuru Kampuni ya Ndege ya Italia, Alitalia ambayo imefanya safari 171 za kuwasafirisha Mapapa sehemu mbalimbali za dunia, lakini kuanzia sasa Kampuni hii inajulikana kama ITA!

Papa Viongozi wa Serikali
12 September 2021, 11:30