Tafuta

Siku ya VII ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira: Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Uwajibikaji, Ushirikiano Umoja na Udugu wa Kibinadamu! Siku ya VII ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira: Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Uwajibikaji, Ushirikiano Umoja na Udugu wa Kibinadamu! 

Ujumbe Wa Siku ya Kuombea Utunzaji wa Kazi ya Uumbaji 2021

Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira sanjari na Kipindi cha Kazi ya Uumbaji yameukuta ulimwengu ukiwa umeandamw na majanga asilia. Hii inatokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kuna mafuriko, maporomoko ya udongo na ukame wa kutisha. Bado kuna majanga ya moto yanayoendelea kuteketeza uoto wa asili, misitu na hata makazi ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Siku ya VII ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira inaadhimishwa tarehe 1 Septemba 2021 na kunogeshwa na kauli mbiu “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake” Zab 24:1. Siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015 kama sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni katika muktadha huu, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anakazia umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa kujikita katika mchakato wa uwajibikaji, ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utunzaji bora wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na huduma kwa maskini.

Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira sanjari na Kipindi cha Kazi ya Uumbaji yameukuta ulimwengu ukiwa umeandamwa kwa kiasi kikubwa na majanga asilia. Hii inatokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kuna mafuriko na maporomoko ya udongo pamoja na ukame wa kutisha. Bado kuna majanga ya moto yanayoendelea kuteketeza uoto wa asili, misitu na hata makazi ya watu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha myumbo mkubwa wa uchumi, kitaifa na kimataifa pamoja na maafa ya watu. Matukio yote yana athari kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kipindi cha watu kuwekwa karantini, kwa upande mmoja kimesaidia sana kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa pamoja na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Imekuwa ni fursa ya kujifunza kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, watu wote wanategemeana na kukamilishana katika mahitaji yao msingi. Hii imekuwa ni fursa kwa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kuendelea kujikita zaidi katika sera na mikakati ya utunzaji bora wa kazi ya uumbaji kwa sababu mazingira ni sehemu ya vinasaba vya Liturujia na Mapokeo ya Kanisa. Ushirikiano wa dhati kati ya Kanisa na Sayansi ni muhimu katika mchakato wa kulinda na kutunza ikolojia ya mazingira asilia.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili awapushe watu na janga la UVIKO-19, awapate wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa mwanga na akili ya kuweza kufufua shughuli za uzalishaji na huduma, ili kukuza uchumi. Ni muda wa kujiepusha na ulaji wa kupindukia pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali za dunia kama ilivyokuwa hapo mwanzo kabla ya janga la UVIKO-19. Anapenda kuwashauri wale wanaopinga chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kutambua maafa makubwa yaliyosababishwa na gonjwa hili na kuacha kupotosha umma kuhusu ufanisi wa chanjo dhidi ya UVIKO-19. Kimsingi, Chanjo lazima ithibitishwe kuwa salama na yenye ufanisi kwa idadi kubwa ya watu kabla ya kuidhinishwa na kuingizwa kwenye programu za chanjo sehemu mbalimbali za dunia. Kwa bahati mbaya sana, huu pia ndio msimamo wa baadhi ya watu wanaopinga ushauri wa wataalamu wa sayansi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi. Ukweli wa mambo ni huu, kuna haja kwa watu kuwajibika kimaadili, kushirikiana na kushikamana, ili kutekeleza sera na mikakati inayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa.

Uchafuzi wa mazingira ni kwenda kinyume kabisa cha kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu. Utunzaji bora wa mazingira na upendo kwa Mungu na jirani ni kielelezo makini cha imani inayomwilishwa katika matendo. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni sehemu ya ushuhuda wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; sanjari na kuzingatia ushauri wa kisayansi unaotolewa na wataalam. Sayansi makini iwasaidie waamini kuboresha imani, matumaini na mapendo. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ujirani mwema, upendo kwa Mungu na jirani ni mambo msingi yanayoonesha utakatifu wa maisha ya mwanadamu. Hii ni Liturujia ya Kanisa inayopata chimbuko lake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Maisha na utume wa Kanisa anasema, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol unakazia pamoja na mambo mengine heshima na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji, utamaduni pamoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Katika kipindi hiki kigumu chenye changamoto nyingi na pevu, Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika kukazia sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Kanisa linawahimiza waamini kuchanjwa dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Waamini wajifunze kwa dhati kabisa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote kama zawadi makini kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa kufanya hivyo, waamini wanatoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Muumbaji na Mkombozi. Mwishoni, mwa ujumbe wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol amewapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema baraka zake za kichungaji!

Patriaki Mazingira
31 August 2021, 15:07