Watawa Wakatoliki waongoza katika kusimulia historia zao wenyewe
Na Sr. Francine-Marie Cooper.
Pembeni mwa Kongamano la Dunia la SIGNIS, lenye mada “Mawasiliano ya Kidijitali kwa Uwiano wa Kiutamaduni na Ustawi wa Mazingira,” lililofanyika Kigali, Rwanda, Juma la kwanza la Agosti, kuanzia tarehe 3 hadi 8, 2026, Vatican News ilizungumza na Sr. Jane Wakahiu, PhD, Makamu Rais Mshiriki wa Operesheni za Programu na Mkuu wa Watawa Wakatoliki katika Mfuko wa Conrad N. Hilton.
Katika mahojiano hayo alitafakari umuhimu wa kuimarisha “uwezo wa mawasiliano wa Masista Wakatoliki kupitia mipango inayolenga, elimu na mafunzo, na kuwawezesha kuongeza matokeo ya kazi zao katika jamii zilizotengwa ulimwenguni kote.”
Uzoefu wa watawa mara nyingi kusimuliwa na wengine
Sr. Jane Wakahiu alisisitiza umuhimu wa watawa “kusimulia historia zao wenyewe, hasa katika enzi ya mawasiliano ya kidijitali.” Kwa vizazi vingi, “uzoefu wa watawa mara nyingi umesimuliwa na wengine,” lakini alisema kwamba “watawa wenyewe wako katika nafasi nzuri zaidi ya kuelezea kazi zao kihalisi miongoni mwa jamii za vijijini, miji ya ndani na watu wanaoishi pembezoni.”
Mpango wa Pentekoste
Katika kufafanua zaidi, Sr Jane, aliakisi “Mpango wa Pentekoste, unaoungwa mkono kupitia ushirikiano na Baraza la Kipapa la Mawasiliano,” kama “mfano wa jinsi ya usimulizi wa historia za kidijitali unavyoweza kukuza sauti za Watawa na jamii wanazohudumia. Kupitia historia za kila Juma zinazochapishwa kwenye Tovuti ya Habari za Vatican/Vatican News, katika lugha 10, mpango huo unatafuta kutoa sauti kwa uzoefu wa watawa kutoka sehemu, jamii na maeneo ya vita ambayo mara nyingi hayazingatiwi, wakishirikisha historia za matumaini, furaha na ustahimilivu.”
Watawa waishi kwa kutimiza utume wa Kanisa
Sr. Jane aliziita historia hizi ni “aina ya uinjilishaji,” akiwaonesha “watawa kuwa hawako katika makanisa tu, bali wapo pamoja na watu katika maisha yao ya kila siku, wakitumiakia kwa huruma, upendo, imani na matumaini,” huku wakiishi “kwa kutimiza utume wa Kanisa na karama za mashirika yao.” Aidha, Sr Jane aliendelea kusisitiza kwamba, “watu wa nje hawapaswi kuwaona watawa kama watu mashujaa tu, bali kama watu wanaosindikizana na jamii, wanaozungumza lugha zao, wanaoelewa uzoefu wao na kusaidia kurejesha matumaini na maelewano ya kiutamaduni.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.