Tafakari Dominika 20 Ya Mwaka A: Imani & Unyenyekevu Mwanamke Mkananayo
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi. Wapendwa familia ya Mungu, ni Dominika ya 20 Mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha kuwa, “Mpango wa Mungu wa Ukombozi ni kwa Watu Wote” Ni mpango wa Mungu tangu mwanzo kwamba wanadamu wote waupate ukombozi wa milele. Ingawa mpango huu ulianza na taifa la Israeli, taifa teule la Mungu, umewafikia sasa watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa njia ya imani, nasi sote tunapokea zawadi hii ya upendeleo kutoka kwa Mungu wetuu. Somo la 1: Ni kitabu cha Nabii Isaya 56:1, 6-7. Somo la kwanza ni kutoka mwanzoni mwa kitabu cha tatu cha Nabii Isaya (Drito Isaiah), kinachoanzia kimsingi sura ya 56-66. Sehemu hii imeandikwa baada ya taifa la Mungu kurejea Yerusalemu kutoka utumwani Babeli. Mji wa Yerusalemu na hekalu vilikuwa vimeanza kujengwa upya tena. Pamoja na kujengeka kwa mji na Hekalu, manabii Ezra na Nehemia walianza pia kazi kubwa ya kufanya majiundo mbalimbali ya kimaadili na kidini. Moja ya majiundo hayo ilikuwa ni kuwafukuza wale watu wote waliokuwa sio Wayahudi (Nehemia sura ya 13). Matokeo yake, kukatokea mgogoro na mvutano mkubwa sana wa kiutambulisho (The crisis of Identity), kwamba, ni nani sasa alistahili kuwa sehemu ya Taifa la Mungu na nani anapaswa kutengwa mara baada ya kurejea Yerusalemu.
Ni nani hasa alikuwa Mwisraeli kweli kweli? Tukumbuke, Wayahudi wengi walikwishachangamana na makabila mengine walipokuwa huko utumwani Babeli. Katika muktadha huu wa ubaguzi na hofu ya wageni, Mungu anamtuma Isaya kutoa tangazo la mapinduzi: milango ya Hekalu iko wazi kwa wote. Mungu anatangaza kuwa, hata wageni (wasio Wayahudi) watakaribishwa katika mlima wake mtakatifu mradi tu wanashika Agano lake na kutenda haki. Somo hili linatabiri sasa kuvunjwa kwa kuta zote za ubaguzi ambazo viongozi kama Nehemia walilazimika kuziweka zamani kwa ajili ya usalama wa kiimani. Waisraeli tangu mwanzo walifikiri kwamba, ahadi ya Mungu ya ukombozi iliwahusu wao tu na wala sio watu wa mataifa mengine. Wokovu ni kwa ajili ya watu wa mataifa yote, ndiyo dhima kuu ya sehemu hii ya mwisho ya kitabu cha Nabii Isaya. Utabiri huu utatimia kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa sadaka ya kifo chake msalabani, amemnunulia Mungu watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Sote tumeshirikishwa bure ahadi hii ya ukombozi.
Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 15:21-28. Katika somo la Injili Takatifu, Bwana wetu Yesu Kristo katika utume wake hakufungwa na mipaka ya kijiografia wala kijamii. Jambo hili lilimfanya aingie kila mara katika mgogoro na Mafarisayo, kama pia sehemu iliyotangulia Injili (15:1-20) hii inavyoelezea. Mwanzoni kabisa mwa sehemu hii ya Injili Takatifu tunaambiwa, “Yesu aliondoka huko akaenda kando pande za Tiro na Sidoni” Haya ni maeneo yaliyokaliwa na Wapagani au watu wa mataifa. Katika utamaduni wa Kiyahudi wa wakati huo, neno “mbwa” lilitumiwa na Wayahudi kama neno la kashfa au dhihaka dhidi ya watu hawa wa mataifa mengine (wasio Wayahudi), kwa sababu waliwaona wapagani hao kuwa ni watu wachafu kiroho, wasio na sheria za Mungu, na wanaoabudu miungu ya uongo. Kristo anavunja mipaka hii ya kijamii na kijiografia iliyokuwapo baina ya Wayahudi na watu wa mataifa. Utabiri wa Nabii Isaya unatimia sasa katika maisha na utume wa Kristo. Ingawa ni kweli wokovu ulianza kwanza na taifa la Israeli na kwamba Kristo ilimlazimu kuwashughulikia kwanza wao, bado yupo tayari kumpokea na kumsaidia kila mwenye imani thabiti katika yeye. Na hapa Mwinjili Mathayo anatupa leo mfano wa mwanamke huyu mkananayo mwenye imani thabiti katika Yesu, kuliko hata Wayahudi wenyewe.
Somo la Pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 11:13-15, 29-32. Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anatufundisha kwamba, ni mpango wa Mungu wa tangu awali, kwamba watu wote waokoke. Lakini Wokovu huu ulianza na taifa teule la Mungu, ili kwa njia yao mataifa mengine yote yaupate pia wokovu huo. Katika dominika iliyopita, mtume Paulo alieleza masikitiko yake makubwa sana kwa kuwa Wayahudi hawakuipokea Injili kama vile walivyotarajiwa. Wao ndio walikuwa wa kwanza kumkataa Kristo. Lakini Mwenyezi Mungu bado anadhihirisha kwamba, wale wasio Wayahudi, yaani watu wa mataifa, kwa sababu ya imani yao thabiti, watakuwa sababu pia ya wongofu wa Wayahudi ili nao tena wamrudie Mungu. Hiki ni kielelezo cha Huruma kuu ya Mungu, inayowajumuisha watu wote, na kutoa bado nafasi kila mmoja kurudi tena na kuikumbatia upya wakati wowote. Katika masomo yetu yote katika dominika hii ningependa tutafakari pamoja mafundisho yafuatayo, yanayotusaidia kuelewa ujumbe huu wa Neno la Mungu katika Dominika hii ya 20A. Fundisho la kwanza: Mwenyezi Mungu ni wa watu wote na kila mmoja ana nafasi katika mpango wa Mungu wa ukombozi. Kanisa li wazi kuwapokea watu wote. Katika somo la kwanza tumesikia Mwenyezi Mungu akinena kwa kinywa cha Nabii Isaya, akiahidi kuwapokea watu wote katika Ufalme wa nyumba yake, maadamu wanalishika Agano walilofanya naye kwa kuishi maisha maadilifu. Anasema, “Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote”. Bwana wetu Yesu Kristo hali kadhalika katika utume wake alikwenda kwa watu wa Mataifa, nao kwa sababu ya imani yao, walipata nafasi ya kuifaidi Huruma ya Mungu inayowaalika wote kwenye ukombozi. Hawa wanawakilishwa na Mwanamke huyu Mkananayo katika somo la Injili Takatifu. Mtume Paulo hali kadhalika anafurahia matunda ya wongofu wa watu wa mataifa, yeye, akiwa Mtume kwa watu wa Mataifa, aliyeamini ya kuwa Huruma ya Mungu inavuka vizingiti na mipaka yote iliyopo kati watu. Mwenyezi Mungu anafungua milango, watu wote wana nafasi katika mpango wake wa ukombozi.
Ndugu mpendwa, nasi pia ni kwa njia ya neema ya bure kabisa ya Kristo, tumeshirikishwa bila mastahili yetu ukombozi, watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Sote kwa njia ya Kristo tumefunguliwa njia ya kuuendea uzima wa milele. Na ukombozi huu tunaupata kwa njia ya Kanisa, ambalo lipo wazi kuwapokea watu wote. Kanisa Katoliki maana yake ni kwa ulimwengu wote, kila mmoja ana nafasi, Kanisa limefungua milango kuwapokea watu wote, maadamu wanashika Agano walilofanya na Mungu na kwa kujitahidi kuyaishi maisha maadilifu. Kila mmoja ana nafasi ya kuupata uzima wa milele. Lakini ni hulka yetu sisi wanadamu kuweka mipaka, Katika Kanisa, katika familia zetu, katika jumuiya zetu za kitawa, katika jamii yetu, makazini kwetu, kwenye huduma mbalimbali, ipo hulka ya kusema, “Huyu ni wetu, na huyu si wetu; au huyu anafaa na yule hafai, au tukajihesabia kuwa wenye haki na kuwa haraka kuwaona wengine wote kwamba hawastahili kabisa. Au huyu kwa kuwa ni maskini hana kitu, huyu hana umuhimu wala kipaumbele kuliko yule mwenye uwezo, ushawishi na tajiri. Dominika hii inatupa changamoto kuchunguza upya mahusiano yetu kati yetu sisi kwa sisi, na kuyajenga kwa namna ile ile Mwenyezi Mungu anavyotuchukulia sisi sote mbele zake. Kwa Mungu wote wana nafasi, wote wanakaribishwa, wote ni wa thamani, wote ni wa muhimu. Je mara ngapi ninachagua hata watu ninaohusiana nao, marafiki, vikundi, au hata kwenye vyama vya kitume? Mara ngapi tunawafungia watu milango hata wale walio na nia ya dhati ya kumtafuta Mungu, kwa sababu ya vigezo vyetu sisi vya kibinadamu kama mafarisayo na waandishi? Tukumbuke, hata kama watu tumewakatia sisi tamaa na hatuwakubali, kwa Mungu wanakubalika. Hata kama ni mimi na wewe nyakati fulani tutakataliwa, Mungu hawezi kamwe kutukataa. Anataka tujisikie kila wakati kwamba sisi tu sehemu ya familia yake, yaani Kanisa. Kumbe moyo wa Kikristo kweli haujengi ukuta, bali unajenga kila mara daraja.
Fundisho la pili: Imani ya kweli haikati tamaa, tuwe na udumifu katika kusali. Tusiwakatishe tamaa wengine wenye nia ya kumtafuta Mungu. Katika somo la Injili Takatifu tunamwona Mwanamke Mkananayo ambaye alikutana na Kristo, akampazia sauti akisema, “Unirehemu, Bwana, mwana wa Daudi” Mama huyu licha ya kuwa ni mpagani, alimtambuana kumkiri Kristo kama Masiha, Mwana wa Daudi. Tukumbuke Wayahudi hata leo hii bado hawajamkiri Yesu kuwa ni Masiya, lakini Mama huyu mpagani akaonesha imani ya juu kabisa kwa Kristo. Lakini Kristo anakaa kimya na wala hakumjibu Neno. Mitume nao wanamkatisha tamaa zaidi, wanamwambia Yesu, “Mwache aende zake, maana anapiga kelele nyuma yetu” Mama huyu hakukata tamaa wala hakuondoka kwa hasira, bali alitambua kuwa imani inadai kuvumilia na kusubiria wakati wa Mungu. Ndugu mpendwa, Mwanamke huyu Mkananayo anatuwakilisha sisi sote ambao mara kwa mara tunakutana na Kristo, katika sala tukiwa nasi na mizigo na changamoto zetu mbalimbali. Tunaomba uponyaji wa maradhi mbalimbali yanayotusibu, tunaomba ili tupate kazi au ajira, tunaomba kwa ajili ya changamoto na matatizo mbalimbali katika ndoa na familia zetu, tunaomba juu ya mipango yetu mbaimbali ya baadaye, tunaomba mabadiliko fulani katika maisha yetu. Lakini sio kila mara Kristo atatujibu kwa wakati sisi tunaotaka. Tunaweza kwa haraka kuanza kuwaza kwamba, mimi Mungu amekwisha niacha. Mungu hana mpango tena na mimi. Huenda katika mahangaiko yetu, wakatokea pia watu wa kutukatisha tamaa hata juu ya imani yetu, wengine wakatudhihaki na kuona kana kwamba tunapoteza nguvu na muda bure. Lakini yawezekana pia imani yetu ikabezwa, ukaonekana kama yule mwanamke mkananayo kwamba, unawapigia watu kelele. Mwanamke huyu mkananayo licha ya kwamba Yesu mara ya kwanza alikaa kimya, na akapokea jibu la kukatisha tamaa kutoka kwa mitume wa Yesu, hakukata tamaa, alibaki mbele ya Yesu akiendelea kuomba. Hatupaswi kamwe kukata tamaa. Kuchelewa kwa Mungu kujibu sala zetu hakumaanishi kwamba ametusahau, wala ametuacha. Imani ya kweli inatualika daima kusema, “Bwana, hata kama sielewi mipango yako juu yangu, bado ninakutumainia.”
Fundisho la Tatu: Tunapaswa daima kuwa wanyenyekevu mbele za Mungu. Katika somo la Injili, Mwanamke huyu mkananayo hakumjia Yesu kwa majivuno. Hakuja akifikiri kwamba kupokea uponyaji kutoka kwa Yesu ilikuwa ni haki yake kama walivyofikiri kila mara Waisraeli. Tunakumbuka katika simulizi ya wakoma kumi, wale tisa waliokuwa Wayahudi hawakurudi kushukuru kwa kuwa walifikiri ilikua ni haki yao, lakini msamaria alirudi, kwa unyenyekevu akitambua kuwa haikuwa haki yake, bali tendo la huruma ya Kristo. Hali kadhalika Mwanamke Mkananayo alijinyenyekeza kabisa kwa Kristo. Hata alipopewa jibu la kukatisha tamaa zaidi mara ya pili, bado alibaki mnyenyekevu na mwenye imani kuu. Hata alipopewa jibu baya tena kwa mara nyingine, aliendelea bado kuwa mnyenyekevu. Mwanamke huyu hakukasirika, hakulalamika, wala hakupandisha hasira kwa kuitwa "mbwa". Hakusema: "Mbona unanitukana? Mimi pia ni binadamu!" Badala yake, alikubali kwa unyenyekevu mkubwa kuwa yeye si Muisraeli na hana haki ya kisheria ya kudai baraka za agano la Israeli. Alijishusha kabisa mbele ya Yesu. Ndugu mpendwa, sisi nasi kuna nyakati tunakwenda mbele za Mungu kana kwamba tunajua kila kila kitu na tunastahili kupata kila kitu. Tunaomba ili Mungu atujibu kwa wakati huo huo. Lakin pia tumeona na kuvutwa na namna hizi za Injili zinazohubiriwa kwa kasi sana kwa wakati wetu wa sasa. Njoo upate hiki, njoo upate kile, na shuhuda mbalimbali zinazoendana nazo. Lakini Mungu anajua ni wakati gani atatupatia yale tunayoomba kwake. Na kigezo kimojawapo cha kupokea yale tunayoyaomba kwake ni kwa kuwa daima wanyenyekevu, kutambu ya kuwa haja zetu zote zinajulikana kwake. Tusali, tuombe, tusubiri kwa unyenyekevu wakati Kristo anapotujibu sala na dua zetu. Ni kama vile tunavyokwenda hospitalini, tunamweleza daktari matatizo yetu, kisha anatuweka katika chumba cha kusubiri majibu. Huwa tuna subira ya kukaa tukijua kabisa kwamba daktari atarudi na atatupatia majibu. Ndivyo hivyo tunapaswa kuwa na subira na unyenyekevu katika sala na maisha yetu ya kiroho. Tujifunze daima kusema, Bwana, bila wewe siwezi kitu. Hata tunapokuwa na elimu, vyeo, fedha, vipaji, mafanikio, bado tunamhitaji Mungu. Unyenyekevu huu unatusaidia kutambua kwamba neema ya Mungu ndiyo msingi wa maisha yetu.
Fundisho la nne: Kristo anatazama daima imani yetu na wala sio historia yetu. Nasi tusiwe wepesi kuwahukumu watu kwa sababu ya historia yao. Kristo alivunja mipaka ya kijiografia na kijamii vile kama Mwenyezi Mungu alivyonena kwa kinywa cha Nabii Isaya. Mwanamke huyu alikuwa Mkanaani, mtu wa mataifa ambaye kwa mtazamo wa kijamii ya wakati huo alikua nje ya watu waliokuwa kwenye mpango wa Mungu wa ukombozi yaani taifa la Israeli pekee. Kristo anaonekana kama kumkatisha tamaa kwa kila alichokiomba, lakini lengo lake hasa lilikua ni kumjaribu mwanamke huyu imani yake, na kuwaonesha pia wanafunzi wake kwamba, kilichohitajika kwa mwanamke yule kuhurumiwa na Kristo ni imani yake thabiti na wala sio historia yake. Mitume walikuwa bado wana mtazamo wa kibaguzi wa Kiyahudi na walitaka mwanamke huyo afukuzwe. Yesu alitaka waone kuwa Mpagani huyu ana imani kubwa kuliko Wayahudi wenyewe. Ndugu mpendwa nasi pia mara nyingi tunaweza kuwa wepesi kuwahukumu watu kutokana na historia yao, badala ya kuangalia daima kile ambacho Mungu kwa nafasi nyingine tena anaweza kufanya ndani mwake. Ni kweli mtu aweza kuwa alikua mwovu, au aliyekosea sana zamani, lakini neema ya Mungu inayofanya kazi kila wakati na kwa namna ya ajabu ndani mwetu ikatenda mabadiliko makubwa. Zipo shuhuda za watu waliohukumiwa vibaya na jamii, kutokana na historia zao lakini Mungu akawaunda wakawa vyombo vyake vipya kabisa. Watu tunaoweza kuwaona kana kwamba hawana imani, hao huenda ndiyo wana imani kubwa na thabiti kuliko hata sisi. Tusiwe wepesi kufungwa katika kisanduku cha historia ya watu, na tukaona kana kwamba hakuna jema lolote linaweza kutoka kwao.
Fundisho la Tano: Tunapaswa kuwa na imani yenye nguvu hata wakati wa ukimya wa Mungu. Somo hili la Injili Takatifu linatufundisha kwamba, Mwanamke huyu si kwamba aliomba tu. Jambo kubwa ni kwamba aliendelea kuamini wakati hali haikuonekana kubadilika. Hii ndiyo imani tunayoiomba katika dominika hii. Je, nini mtazamo wangu katika ukimya wa Mungu? Ndugu mpendwa, ni rahisi sana kumwamini Mungu wakati mambo yetu yote yanapokwenda shwari, wakati tunapopata vyote tunavyohitaji, wakati afya iko njema, wakati familia, jumuiya, ndoa zina amani, wakati biashara imechanua na kustawi, wakati kazi zetu za kila ziku zinavyokwenda vizuri na matokeo yake tunapoyaona. Hapa imani huwa imara sana. Lakini mambo yanapokwenda kinyume huwa ni rahisi sana kurudi nyuma na kutikisika kabisa kiimani. Wengine kuishia hata kuikana kabisa imani. Dominika hii inatukumbusha kuwa imaini thabiti inadhihirika pale tunapopata ujasiri kusema, “Bwana, sioni njia lakini bado ninakuamini wewe.” Kumbe, imani si kumwamini Mungu kwa sababu kila kitu kiko sawa, bali ni kumwamini Mungu hata wakati kila kitu hakiko sawa. Kristo anamsifu Mama yule kwa kuwa na imani thabiti naye anamponya binti yake tangu saa ile. Hitimisho: Katika dominika hii tuombe neema ya kutambuwa thamani ya ukombozi ambao Mwenyezi Munu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo ametaka sisi sote tushirikishwe. Tuwe tayari nasi sote kama Mtume Paulo kutumika kuwa vyombo vya huruma ya Mungu ili kuwasaidia watu wengi zaidi na zaidi kumjua Mungu na mpango wake kwa ulimwengu mzima ili sote tustahilishwe kuupata uzima wa milele.