Tafuta

Sr Judita akiwa katika Hospitali. Sr Judita akiwa katika Hospitali. 

Siria:Kumtumikia Mungu na watu katikati ya vita na shida

Kwa miaka minne iliyopita, Sr. Judita amekuwa akihudumu nchini Siria,ambapo yeye na shirika lake wanasimamia Hospitali ya Kikatoliki.Anazungumzia kuhusu hofu za Wakristo,kuhama kwa vijana na matumaini wanayojitahidi kuwaletea wagonjwa kila siku.Kwa hiyo Damasco,anajulikana kama mtawa anayeendesha “Hospitali ya Kifaransa.”

Na Sr. Jana Pavla Halčinová, DC

Kwa miaka 33, Sr. Judita Cáková amekuwa mmoja wa Shirika la Mabinti wa Upendo wa Mtakatifu Vinsenti wa Paulo(DC). Akiwa muuguzi aliyefuzu, amehudumu katika sehemu nyingi za dunia, ikiwa ni pamoja na kambi za wakimbizi na maeneo ya migogoro kabla ya kufika Damasco. Alikumbuka tukio moja ambalo limebaki na kumu kumbu. Watu walipouliza, "Mwanamke anayetusaidia ni nani?" mkalimani alijibu tu, "Ni mwanamke anayempenda Mungu na watu." Maneno hayo yamebaki ndani mwake tangu wakati huo. Uamuzi wake wa kujitolea katika utume wa kibinadamu unagusa sana. "Niliguswa na umaskini uliokithiri wa watu waliokimbia vita na vurugu bila chochote na walikuwa wakihitaji hata msaada wa msingi kabisa," anasema. Leo, dhamira yake imechukua sura tofauti. "Jukumu langu ni kusimamia Hospitali kwa njia ambayo itaifanya iwe endelevu kifedha huku tukibaki tumejikita katika kakarama yetu ya kuwahudumia maskini." Hospitali hiyo, inayojulikana sana Damasco kama Hospitali ya Kifaransa, ni ya Shirika wa Mabinti wa Upendo wa Mtakatifu Vinsenti wa Paulo DC. Ingawa masista wanasimamia utawala wake, wafanyakazi wake wengi ni wataalamu wa kawaida kutoka asili tofauti za kidini.

Mwanzo mgumu

Sr. Judita alipofika Siria kwa mara ya kwanza, hakuzungumza Kiarabu na ilibidi abadilishe mfumo wa afya tofauti kabisa. "Nilijua Kifaransa na Kiingereza kidogo," alikumbuka huku akitabasamu, "lakini lugha zote zilichanganyika kichwani mwangu." Polepole, alipata njia za kuwasiliana na kuzoea kazi yake katika chumba cha upasuaji. "Nilifurahia sana kusaidia katika chumba cha upasuaji wa wanawake waja wazito kwa sababu utaratibu ulikuwa sawa kabisa." Madaktari wawili waliosoma nchini Urusi walikuwa washauri muhimu sana. "walikuwa wa msaada mkubwa kwa sababu niliweza kuwauliza maswali na walinielezea kila kitu kwa uvumilivu."

Leo, Hospitali inafanya kazi chini ya hali ngumu. Ina vitanda 108, karibu wafanyakazi 250, na na takriban madaktari 130. "Jukumu langu ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanapokea mishahara yao mara kwa mara na kwamba wana mazingira mazuri ya kazi." Kudumisha utulivu wa kifedha ni changamoto ya mara kwa mara huku tukiendelea kuwa waaminifu kwa dhamira ya hospitali. "Hatuwezi kuwahudumia maskini tu kwa sababu hatuna shirika linaloweza kufadhili huduma zao zote. Kwa sababu hiyo, pia tunawakaribisha wagonjwa wanaoweza kumudu matibabu, na kuturuhusu kutoa huduma kwa wale ambao hawawezi." Hospitali inashirikiana kwa karibu na Caritas na mashirika kadhaa ya upendo nchini Syria yanayoungwa mkono na wafadhili wa kimataifa. Katika miaka iliyopita, pia ilipokea msaada mkubwa kupitia mpango wa Hospitali Huru ya Vatican, unaoongozwa na Balozi wa Kitume, Kardinali Mario Zenari. "Shukrani kwa msaada huu, watu wengi waliweza kupokea upasuaji kuokoa maisha yao, hata katika hali za dharura."

Kuongezeka kwa kutokuwa na uhakika

Kulingana na Sr. Judita, jamii ya Syria imebadilika sana tangu kuzuka kwa vita mwaka wa 2011. "Watu wengi hufanya kazi mbili ili tu kuishi. Pia kumekuwa na uhamiaji mkubwa wa watu walioelimika—hasa Wakristo na wanachama wa jamii za wachache—kwenda Ulaya, Amerika, na Australia." Wale wanaobaki, alisema, mara nyingi ni watu ambao hawana uwezekano wa kuondoka. Mvutano wa kikanda umeongeza safu nyingine ya kutokuwa na uhakika: milipuko na mashambulizi ya roketi yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Shambulio moja linabaki wazi sana katika kumbukumbu yake. Kufuatia bomu katika Kanisa la Kiorthodox ambalo lilisababisha vifo kadhaa, wengi wa waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Ufaransa. "Tuliwatibu karibu asilimia themanini yao." Wengi wa waathiriwa walikuwa vijana. "Tulipowauliza baada ya upasuaji jinsi tunavyoweza kuwasaidia, karibu wote walitoa jibu lile lile: walitaka kuondoka nchini."

Mahali pa amani na mapokezi

Licha ya vurugu zinazoizunguka, hospitali inajitahidi kubaki mahali pa matumaini. "Muundo wetu una mazingira ya Kikristo—ya heshima, ushirikiano, na hamu ya kweli ya kuwahudumia wengine." Wafanyakazi wanahimizwa kumwona Kristo ndani ya kila mtu na kumtendea kila mgonjwa kwa heshima na huruma. "Ni moja ya sababu watu wanahisi salama hapa." Katika nchi ambapo vituo vingi vya afya vinaendeshwa na serikali, Hospitali ya Ufaransa imekuwa ishara ya uaminifu kwa familia nyingi. Muundo huo pia unaendelea kukua. Hivi majuzi, ilifungua idara mpya ya magonjwa ya moyo inayotoa huduma ya katheta ya moyo na upasuaji wa moyo wazi. "Ni muhimu kwamba kila mtu, ikiwa ni pamoja na Wakristo, apate huduma bora ya matibabu."

Dhamira yake mara nyingi huenea zaidi ya huduma ya afya. Wakati wa vipindi vya mgogoro, hospitali ilitoa malazi kwa wafanyakazi wa afya ambao walipoteza ghafla nyumba zao na kazi zao. Pia ilipanga usafiri kwa wafanyakazi kwa sababu kusafiri kupitia Damasco baada ya giza kumekuwa hatari zaidi. "Hakuna umeme. Jiji ni giza, na watu wanaogopa."

Matumaini yanayodumu

Sr. Judita alikiri kwamba hospitali inategemea sana msaada wa kimataifa. "Kila aina ya usaidizi unakaribishwa, iwe kifedha au vifaa. Tunahitaji haraka ambulensi mpya, na pia tunahitaji msaada wa kugharamia gharama za upasuaji kwa wagonjwa maskini." Lakini katikati ya vita, ugumu, na kutokuwa na uhakika, ni maisha yaliyobadilishwa ambayo yanaendelea kudumisha tumaini lake. Anamkumbuka mtoto mmoja wa kike ambaye alizaliwa kabla ya wakati akiwa na ujauzito wa miezi sita tu. "Alizaliwa siku ya Mtakatifu Mikaeli, kwa hivyo tulipendekeza jina la Miša." Leo, msichana huyo mdogo ni mtoto mwenye afya njema wa miaka miwili. "Nyakati kama hizi hutuletea furaha kubwa," Sr. Judita alisema. "Zinatukumbusha kwa nini tunaendelea."

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

03 Agosti 2026, 16:26