Tafuta

Umisionari Papua New Guinea Umisionari Papua New Guinea 

Miaka 125 ya uwepo wa Kimisionari,Jimbo la Bougainville nchini Papua New Guinea

Jimbo la Bougainville linaadhimisha miaka 125 ya uwepo wa kimisionari Katoliki katika Mkoa wa Kaskazini kuanzia tarehe 14 hadi 17 Agosti 2026.Ni maadhimisho yanayotaka kuheshimu vizazi vya wamisionari,makatekista na waamini wote wa eneo hilo walioliunga mkono Kanisa wakati wa vita,migogoro na mabadiliko ya kijamii.

Na Sr. Christine Masivo, CPS, - Vatican.

Jimbo Katoliki la  Bougainville nchini Papua New Guine linaadhimisha miaka 125 ya kihistoria ya kuwasili kwa Wamisionari wa kwanza Wakatoliki, sherehe hii ni zaidi ya kumbukumbu ya zamani. Kanisa limekita mizizi na kuvumilia magumu na vita, na kukua na kuwa Jumuiya yenye nguvu ya wakazi, na  zaidi ya Wakatoliki 200,000 katika Parokia 35.

Kutoka vituo vya misheni hadi Parokia.

Kanisa Mahalia, likiwa limejikita katika ujio wa kwanza wa Wamisionari wa Shirika la Wamarist huko Pokpok mwaka 1901 na Buin mwaka 1903, limekua kutokana na kujitolea kwa wamisionari na makatekista walei. Imani hiyo ilizidi kukomaa hata wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na mgogoro wa Bougainville. Maadhimisho ya Jubilei yameanza tangu  tarehe 14 - 17 Agosti 2026 ambayo ynaibua kwa mara nyingine tena historia  ya mwanzo hadi sasa, ikiwa na mwakilishi wa Papa,  Kardinali Luis Antonio Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji ambaye ataongoza Ibada ya Misa Takatifu ya Jubilei mnamo  tarehe 16 Agosti 2026 katika Kanisa Kuu la Mama Yetu aliyepalizwa Mbinguni huko Hahela. Ziara yake pia inajumuisha kutembelea huduma ya Parokia na hospitali, kukutana na viongozi wa kikanda, na kubariki jengo jipya la jimbo hilo.

Imani ya watu wa Mungu wa Papua New Guinea
Imani ya watu wa Mungu wa Papua New Guinea   (© Fr. Zdzislaw Mlak SVD in PNG)

Kuelekea uongozi mahalia

Kwa mujibu wa  Shirika la Kipapa la Habari la Kimisionari Fides, lilibainisha kuwa Padre Christian Sieland, Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Utume wa Kimisionari (PMS) nchini Papua New Guinea, alielezea historia hii kama mwenyeji aliyekuwa na fursa ya kipekee ya kukua Papua New Guinea wakati ambapo karibu 90% ya Kanisa mahalia wakati huo, walikuwa Wamisionari." Aidha  Padre huyo alisimulia kuwa “Baba yangu alikuwa mmisionari mlei aliyeajiriwa na Shirika la Maendeleo ya ushirika la Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ujerumani (Misereor),” na alifanya kazi pamoja na “mapadre na watawa wa kike na kiume kwa zaidi ya miaka 20,” alisema.

Kwa sasa yeye ni wa eneo hilo ambaye anasimama kidete  wakati huu muhimu wa mabadiliko kutoka Kanisa  la kimisionari hadi Kanisa mahalia, Ulimwenguni. "Ninaamini maadili muhimu zaidi ambayo nimerithi ni heshima na shukrani," alisema. Wito wangu mwenyewe ulitokana na ushuhuda wa familia na wamisionari. Baada ya kujitolea na Shirika la Mapadre wa Neno la Mungu (SVD) huko Papua New Guinea kuanzia 1999 hadi 2000, urafiki wake na Wamisionari uliamsha wito wake wa upadre.

Wakati wa Ziara ya Kitume ya  Papa Francisko nchini Papua New Guinea Septemba 2024
Wakati wa Ziara ya Kitume ya Papa Francisko nchini Papua New Guinea Septemba 2024   (Vatican Media)

Imani, utamaduni na upatanisho

Kanisa limepitia vizazi vya huduma ya kimisionari. Miaka ya 1990 na 2000 ilileta ongezeko kubwa la miito ya asili, na kuunda kizazi cha leo hii cha viongozi wa Kikristo wa eneo hilo. Kwa njia hiyo Papua New Guinea ni mojawapo ya mataifa yenye tamaduni nyingi zaidi duniani, yenye lugha zaidi ya 800 na jamii nyingi za kikabila na  ambazo husababisha mgawanyiko, lakini hii pia inaweza kuwa chanzo cha umoja mkubwa.” Kanisa limesaidia kujenga umoja huo kupitia kujenga shule, huduma za afya, na jumuiya za kichungaji zinazowaunganisha watu wa tabaka mbalimbali ya kikabila. "Ndani ya mabaraza ya kichungaji ya Parokia, si jambo la ajabu kuona wanachama wa jumuiya zinazopingana kihistoria wakifanya kazi pamoja kama familia moja ya Kikristo," Padre Sieland alisema.

Huduma kupitia vituo vya kichungaji

Changamoto kubwa bado zipo. Mapigano madogo, migawanyiko ya kisiasa, shutuma zinazohusiana na ushirikina, vurugu, na mifumo ya jadi ya kulipiza kisasi inaendelea kusababisha mateso katika baadhi ya jamii. "Kanisa linatafuta kushughulikia hali hizi kwa usikivu wa kichungaji na uwazi kuhusu desturi zisizoendana na imani ya Kikristo," alisema Padre Sieland. Vituo vya kichungaji hutoa mafunzo katika utatuzi wa migogoro, upatanisho wa amani, na usaidizi kwa waathiriwa wa vurugu za majumbani na shutuma za ushirikina. Wapatanishi waliofunzwa na kanisa wakati mwingine huitwa kuingia katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ya kikabila inayoendelea, na Padre Sieland alisisitiza hili, akisema kwamba kupitia kazi kama hiyo, Injili inakuwa zaidi ya ujumbe unaotangazwa kutoka kwenye mimbari, na inakuwa nguvu ya vitendo ya uponyaji na upatanisho.

Mustakabali wa Kanisa la Melanesian

Kuna utofauti mkubwa wa makabila na tamaduni, na kwa hiyo utamaduni unabaki kuwa safari inayoendelea. "Watu wetu lazima wahimizwe kuhifadhi lugha zao, urithi wa kiutamaduni, na maadili huku wakiifanya Injili kuwa yao wenyewe. Heshima na shukrani kwa yaliyopita ni muhimu ikiwa imani itaota mizizi zaidi, alisema Padre Sieland. Akimbuka Mtakatifu wa hivi karibuni wa aliyetangazwa tarehe 19 Oktoba 2025, na Papa Leo XIV alisema: “Papua New Guinea imepata baraka ya Mtakatifu wao wa kitaifa, Mtakatifu Peter To Rot, ambaye anatoa taswira yenye nguvu ya umoja huu," alisema Padre Sieland. Ingawa alitoka Rabaul, Wakatoliki nchini kote wanamwona kuwa  wao kwa sababu anakumbukwa kama Katekista, shahidi, na Mkatoliki mwaminifu. Hii inaonesha fursa nzuri tulizonazo za kujenga ushirika wa kweli.

Katekista Mtakatifu wa Papua New Guinea
Katekista Mtakatifu wa Papua New Guinea   (© Fr. Zdzislaw Mlak SVD in PNG)

Kanisa mahalia lazima lijengwe juu yao 

Baada ya miaka 125 huko Bougainville na zaidi ya karne moja ya uinjilishaji wa Kikatoliki kwingineko huko Papua New Guinea, Kanisa limesimama katika kizingiti kipya. Wamisionari wa zamani waliweka misingi, Kanisa la leo hii  hapa nchini lazima lijengwe juu yao. Changamoto ni kubwa, lakini pia matumaini. Ikiwa imani, utamaduni, upatanisho, na uongozi wa mtaa vitaendelea kukua pamoja, kizazi kijacho kinaweza kurithi si kanisa tu ambalo lilinusurika historia yake, bali kanisa linaloweza kubadilisha mustakabali.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

15 Agosti 2026, 10:20