Askofu Mkuu Colombo:Ziara ya Papa nchini Argentina italeta ujumbe wa amani
Na María Cecilia Mutual- Vatican.
Kanisa Katoliki nchini Argentina linasubiri kwa hamu ziara ya Papa Leo XIV nchini humo, iliyothibitishwa na Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican. Tukio hilo linalosubiriwa kwa muda mrefu linatoa fursa ya kuimarisha imani na kufufua dhamira ya jumuiya ya Wakatoliki katika uinjilishaji.
"Ni ziara ya kitume ambayo kila mtu amekuwa akiisubiri kwa hamu," Askofu Mkuu Marcelo Daniel Colombo, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Argentina na Askofu Mkuu wa Mendoza, alisema hayo akizunumiza na Vatican News. "Tunafurahi sana kumkaribisha Baba Mtakatifu nchini mwetu, tukimpokea kama shahidi wa Kristo na msafiri wa Habari Zake Njema. Tunajua anatuletea ujumbe wa matumaini; tunajua anakuja kwa jina la Kristo; na tunajua pia anatuletea furaha ya Injili."
Askofu Mkuu alikuwa akizungumza kufuatia tangazo la tarehe 5 Agosti 2026 la Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV ya kwenda Amerika Kusini, ambayo itafanyika kuanzia tarehe 6 hadi 17 Novemba 2026. Katika ziara hiyo, Papa atatembelea Buenos Aires, Córdoba na Luján kuanzia tarehe 8 hadi 11 Novemba. Argentina itakuwa nchi ya pili katika ratiba ya Ziara yake ya sita ya Kitume ya kimataifa, ikifuatia na Uruguay na Peru.
Maandalizi makini yenye mwelekeo mkubwa wa kichungaji
Maandalizi yalianza mara tu uwezekano wa ziara ya Papa ulipojitokeza. Askofu Mkuu Colombo alisema kwamba timu zimeanzishwa ili kusimamia upangaji wa vitendo wa ziara hiyo, kujifunza juu ya ziara za hivi karibuni za Papa Leo XIV na kushauriana na maafisa wa Kanisa waliohusika katika kuziandaa. "Kama sehemu ya mchakato huu, tulisoma uzoefu wa Ziara za Kitume za hivi karibuni na kushauriana na maafisa wa Kanisa walioshiriki katika kuzipanga," alielezea.
Utofauti na uhai wa Kanisa nchini Argentina
Zaidi ya mipango ya vifaa, Askofu Mkuu Colombo alisisitiza umakini mkubwa wa kichungaji wa maandalizi. "Tunachokiona kuwa muhimu ni uhai wa Kanisa litakalompokea," alisema. "Maisha ya Kanisa hilo yanawakilishwa kupitia maaskofu wake. Kwa sababu hii, ziara ya Papa ilikuwa mada kuu ya majadiliano wakati wa mkutano mkuu wa hivi karibuni wa maaskofu wa Argentina." Maaskofu walishiriki maoni na matarajio yao kulingana na hali halisi tofauti zinazokabili majimbo na mikoa ya nchi hiyo, kwa lengo la kuhakikisha kwamba ziara hiyo inaonyesha utofauti na uhai wa Kanisa nchini Argentina.
Mbebaji wa amani
Askofu Mkuu wa Mendoza alibainisha kuwa "maneno na ishara za Papa Leo kama mchungaji mwema" zimeambatana na Kanisa na waamini tangu alipoanza huduma yake. "Sasa tutakuwa naye miongoni mwetu, akishiriki ziara ya uinjilishaji na watu wa Argentina na kuleta ujumbe wake wenye nguvu wa amani, kujitolea kwa utu wa binadamu na ufufuo unaoendelea wa Kanisa," alisema. "Sinodi na utume, utume na sinodi, zimeunganishwa kwa karibu, ni mada zinazojirudia katika jumbe na mapendekezo ya Baba Mtakatifu," aliongeza.
Sherehe huko Luján, ambapo Papa Bergoglio mara nyingi alisali
Kabla ya kuondoka Argentina, Papa Leo XIV atasafiri kwenda Madhabahu ya Luján kusali mbele ya Mama Yetu wa Luján, mlinzi wa nchi hiyo. Askofu Mkuu Colombo alisema sherehe hiyo "itakuwa chanzo cha furaha na fursa ya kukutana na Mama yetu, mlinzi wa Waargentina wote".
"Kuwa na Papa huko, kama tulivyokuwa na Kardinali Bergoglio, Askofu Bergoglio na Padre Bergoglio, (yaani Papa Francisko) na kama tulivyomkaribisha Papa Yohane Paulo II, itakuwa fursa nzuri na ya ajabu kweli ya kupata uzoefu wa ziara ya Papa Leo XIV kwa umoja na katika roho ya watoto wa Mungu," Rais wa Baraza la Maaskofu wa Argentina alihitimisha.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.