Tafuta

2026.07.29 Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu(CPS) watembelea Radio Vatican. 2026.07.29 Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu(CPS) watembelea Radio Vatican.  #SistersProject

Wamisionari wa Damu Azizi(CPS):Tunatumwa mahali popote!

“Imani iliyoko Afrika tunaiomba sana irithishwe kwa vijana,kwa watoto na familia ziwe ni vikanisa vidogo maana ndiyo msingi wa imani.Kuna neema za kutosha tujitahidi kuzichota ili tuwe kati ya wale wachache ambao walivuka kwenda nchi ya Kanaani.”Huu ni ushuhuda wa Wamisionari wa Damu Azizi(CPS),wakati wa kutembelea Studio za Radio Vatican,wakiwa katika hija yao ya mafunzo jijini Roma.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Utume wa kimisionari kama Shirika la Kimataifa kuanzia shuleni, changamoto za Watoto na zana za kiteknolojia baada ya Uviko 19 na msisitizo wa urithishwaji wa imani barani Afrika, ulikuwa mada za ushuhuda uliotolewa na Masista Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, walipotembelea Radio Vatican, wakiwa katika hija yao ya mafunzo ha masistia wa nadhiri za muda ambao wanafanya utume wao barani Ulaya. Katika kukutanika pamoja kutoka maeneo mbali mbali ya utume wamejifunza mengi na wanaendelea kujifunza. Miongoni mwao, walikuwa ni Sr Lilian Mdolwa kutoka Parokia ya Gare, Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga, Tanzania na Sr  Margaret Mary, mzaliwa wa Kenya,  Jimbo la Mombasa huko Taita Milimani na ambaye alisema  “Ninafurahi sana kuwa hapa, mmisionari wa Damu Takatifu.

Kama Wamisionari wa Damu Azizi, shughuli zenu  ni zipi?

Sr Lilian: Tunafanya utume tofauti tofauti. Ni Shirika la Kimataifa tunafanya utume wetu katika nchi mbalimbali hapa duniani. Na sisi wawili leo tuko hapa kwenye studio za Vatican baada ya kutembelea nyumba yetu Mama hapa Roma. Tunafanya Semina ya masista wa wanadhiri za muda ambao wametumwa huku mwaka mmoja uliopita. Kwa hiyo, tumejikuta tuko hapa na tunafurahi kuwa kwenye hizi studio leo. Kwa sasa hivi ninafanya utume wangu katika nchi ya Austria, ambayo ni upande wa kaskazini mwa nchi hii ya Italia. Na kule nafanya utume wangu kama mwalimu katika shule ya ya Kimataifa. Ndiyo utume ninaofanya kwa sasa, ninafanya kazi na watoto.

Kuwakaribisha watawa wa CPS katika  Radio Vatican.
Kuwakaribisha watawa wa CPS katika Radio Vatican.

Unafundisha kwa lugha gani?

Sr Lilian: Ninafundisha kwa Kiingereza na Kijerumani, kwa sababu ni shule ya Kimataifa (International School,) basi ni shule ambayo inatumia lugha zote mbili.

Sr Margaret Mary: Nami nilipata uhamisho wangu, nilikuja hapa mwezi wa nne. Nimehamishwa kutoka Kanda ya Afrika Mashariki huko Kenya, nikatumwa hapa Roma. Na hapa Roma niko kwenye nyumba mama, ambako tuko masista 10. Wanne wako katika Baraza la ushauri na Masisita ni wa Jumuiya. Tuko pamoja, tunafanya kazi pamoja. Utume wangu hasa ni jikoni na shughuli zote zinazohusiana na nyumbani.

Makaribisho ya Watawa wa CPS
Makaribisho ya Watawa wa CPS

Nirudi kwa mwalimu ambaye anafundisha kwenye Shule ya Kimataifa. Ni changamoto gani ambazo unazipata kama wewe sista kutoka sehemu ya Afrika?

Sr Lilian: Pamoja na kuwa tayari kuwa mmisionari, lakini kiukweli ukienda nchi nyingine changamoto kwanza ni utamaduni ambapo wenzetu, tuseme wana kila kitu wanachohitaji. Na mara nyingine hata mimi changamoto ninayokutana nayo kwa mfano nikikuta labda watoto wana kila kitu wanachohitaji kuwa shuleni, na kwa hiyo akiwa na kila kitu, hahitaji kitu chochote kingine na zaidi hapendi kusoma. Halafu tena ukifikiria mahali walipo wamatazama picha, wanazoziona mara nyingi ni picha zinazooneshwa kwenye media zao ambazo mara nyingi ni zile sehemu zenye matatizo, na zaidi  labda vita.

Na kwa upande wa kuulizwa juu ya Afrika kwa kawaida inaonekana kama ni nchi moja, ingawa nchi za Afrika ni kubwa. Na kwa wale ambao hawajafunguka, yaani hawajatoka nje wakaona, ukikutana nao wanakuuliza, hata wazazi au mtu yeyote tu unayekutana naye akiwa interested na wewe, anakuuliza: “How is Africa?” Sasa unajiuliza mimi ninatoka Lushoto kule Gare, hata nchi yangu yenyewe sihifahamu vizuri , kwa sababu sijaenda kule kusini, kaskazini, mashariki, au  magharibi. Katika hilo unaweza kujikuta unapata kama kigugumizi cha kujibu lile swali. Lakini siku hizi nimezoea, mtu akiniuliza: “Habari ya Afrika?” Nasema: “Mimi ninajua tu pale ninapotoka nyumbani…

Ninakuja na swali jingine. Baba Mtakatifu hivi karibuni mwezi wa tano tarehe 25 alichapisha Waraka wake wa Kwanza wa Kitume wa Magnifica Humanitas)hasa hasa kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi utu wa mwanadamu. Changamoto kwa sasa ni kwenye upande wa vijana, na hasa kwa utambuzi wa kuwa  mbele na changamoto, lakini pia hata kwetu sisi Afrika ambao wako nyuma japokuwa  wanakwenda kwa kasi. Katika shule ambapo ndiyo changamoto zaidi, mnafanyaje kuwa makini kati ya ufundishaji na mitaala ya kawaida, kumwona mwanafunzi kama anaweza kweli, baada ya kutumia hizi zana zinazotolewa na mitandao ya kijamii, hasa kwenye upande wa akili unde (AI)?

Watawa wa CPS wakiwa Studio za Radio Vatican
Watawa wa CPS wakiwa Studio za Radio Vatican

Sr Lilian: Kweli hii ni changamoto. Tena ukichukulia kwamba mimi nimekuja kipindi kifupi kabla ya Corona(UVIKO 19) na tulikuwa tunafanya kazi tukiwa nyumbani au hata kama ukienda shuleni kwa sababu huku watoto hawawezi, wazazi wana fanya kazi hakuna wasaidizi tuseme madada wa kazi. Kwa hiyo mzazi anatategemea mtoto aende shuleni akakae huko mara nyingine kuanzia saa 2:00 asubuhi mpaka saa 11:00 jioni ili mzazi aweze kufanya kazi yake atoke na ndiyo  aje amchukue mtoto arudi nyumbani. Kulikuwa na wengine  wenye uwezo wa kukaa nyumbani. Unapokuwa unafundisha pale darasani wale watoto waliopo darasani, nao wa darasani ilibidi tutumie mtandao kuwafikia wale watoto.

Kwa hiyo lazima walikuwa wawe na Kompyuta, wakae online na sisi tuko shuleni. Kwa hiyo unachofundisha unatuma kazi, kama mtoto hayupo darasani inabidi utume kazi unachowakilisha na ye akisikie kule nyumbani na umuone. Katika hili basi watoto wakazoea vibaya mno kiasi  kwamba mtu anaweza akatoka chumbani  akiwa na na mavazi ya kulala, hajanywa hata chai, anajua tu saa 2:00 tuna kipindi, basi anatoka kitandani anakwenda anakaa pale kwenye Komputa unafundisha, ukimaliza kipindi anaondoka. Hii ikawa ni changamoto wakati Corona imeisha kurudi shuleni tena. Ikawa ni changamoto moja watoto hawataki tena kuja shuleni, wanataka wakae nyumbani uwafundishie wakiwa nyumbani. Lakini hiyo basi tukaweza kuitatua kwa sababu ilifika mahali, sisi shule wetu asante Mungu ni ya Kimataifa, hivyo tuna uhuru fulani kwamba shule inaweza kudhibiti vitu vingine.

Wata wa CPS wakitembelea Radio Vatican
Wata wa CPS wakitembelea Radio Vatican

Pia hata ukiwa darasani ubao wa kufundishia sio kutumia kalamu, ni Kompyuta. Unakuwa na Kompyuta yako unaunganisha na ubao kwa hiyo unachofundisha kinatokea kule ubaoni. Kwa hiyo ikawa ni shida kurudi kwenye kuandika labda kwenye vitabu na nini… kwa sababu ukishaitoa pale ina maana mtoto unaweza kutolea nakala akachukua. Kwa hiyo ikawa ni hivyo, kumpa mtoto kazi ya nyumbani ikawa ni shida ya kurudi tena kuwaambia watoto waandike vitu kwenye madaftari yao badala ya kusubiri mwalimu awape nakala  ya kazi uliyofundisha.

Kitu kingine sasa hivi tena tunachopigana nacho, kwa sababu watoto kwenye shule yetu pia wanatumia Kompyuta kwa kila kitu hasa Sekondari hadi kidato cha Tano na Sita (especially middle school na high school). Kwa hiyo hakuna muandiko. Ukiwaambia waandike kitu kwa mkono yaani wewe mwalimu mwenyewe utakuwa unajipa adhabu kwa sababu hawana ile sanaa(art) ya kutumia mkono. Na sisi tulivyofundishwa, tulivyokuwa vyuoni ni kwamba unapomfundisha mtoto, uhakikishe anatumia milango ya fahamu(senses) nyingi ili kuweka kumbukumbu. Anavyoshika kalamu anaandika huku anasikiliza, huku anachora..., basi inamsaidia kukumbuka. Lakini sasa hii ya AI na kila kitu,kiko hapo. Kwa hiyo mtoto anakuwa mvivu wa kufikiria, ni changamoto kubwa kweli.

Kama walimu mnafikiria ni kitu gani na mnafanyaje angalau kuwarudisha hawa watoto

Kitu ambacho shule imefanya na sisi wote tunafanya sasa hivi, kwa mfano sisi shule yetu tangu tumeanza muhula, huu muhula wa mwisho ambao tumeanza tu likizo wiki iliyopita, tumeombwa na tumekubaliana wote kwamba hakuna tena kutumia Kompyuta darasani kwa muda mrefu kufundishia. Tumerudi kwenye mambo ya kutumia kalamu, na karatasi, kusoma vitabu. Hata kama unatoa  kazi ya kufanya utafiti kwa mfano, hata kwenye mtandao, inabidi iwe Kudhibiti(controlled)  utoe mada flani(specific topi) na zana ile ambayo mtoto ataitumia kufanya utafiti wake. Halafu aandike kwa maneno yake, asome anachosoma kule mtandaoni, kwa sababu ni fursa (advantage) fulani kwamba siku hizi unaweka na  unavuta, unapata habari (information)unayotaka. Ili mtoto aweze kutumia ile habari (information) anayotaka isije ikawa kama tulivyokuwa tunafanya wakati wa Corona, anaiandika kwa maneno yake mwenyewe. Na mwalimu anakuwa anadhibiti (incontrol,) Kompyuta zao ambazo zimeunganishwa na imfumo wa shule. kwa njia hiyo anapoandika unaona, na alichotoa. Kama mwalimu inabidi  adhibiti  hata kama uko hapo darasani, wanapofanya kazi kwenye Kompyuta zao, mwalimu anauwezo wa kudhibiti na kumwambia mtoto: Hapa umenukuu neno kwa neno, unatakiwa uyafikirie. Kwa hiyo tumeamua kwamba turudi kwenye kipindi cha kuandikia (analog.)Tunafanya hiyo kazi hivyo, halafu kitu kingine ni simu. Sisi shuleni kwetu kila mtoto ana kabati ya kuweka vitu na , hawaruhusiwi kutumia simu shuleni.

Watawa wa CPS ndani ya Jengo la Pio
Watawa wa CPS ndani ya Jengo la Pio

Asante sana Sista, tunakutakia kila la heri katika utume wako. Nirudi kwa Sista anayekaa Roma. Wewe tangu umefika hapa Roma, ni mambo gani ambayo yamekufurahisha hasa kwenye upande wa dini na mambo mengine ambayo labda ni changamoto ukilinganisha na sehemu ambazo umepitia katika utume?

Sr Margaret: Tangu nifike hapa Roma, kitu ambacho kimenifurahisha sana ni wakati tulikuja kusherehekea sherehe ya ujio wa Roho Mtakatifu, Pentecoste. Nilifurahi sana tulikuja na tukamwona Papa kwa macho. Hiyo ndiyo ilikuwa furaha yangu kubwa, tulikuja na masista wetu. Niliona imani ya Wakristo wa hapa Roma, watu ni wengi kweli lakini wengi wao wanakuja kama utalii hivi, wanakuja kuona Roma ikoje, ni mahali gani. Kwa hivyo nikilinganisha imani ya Afrika na hapa Roma, naweza kusema kule Afrika tulipokea hii imani na kuna utulivu kanisani. Lakini ukija kulinganisha na hapa, unaona kwamba kuna watu wako kanisani, lakini bado unaona wengine wanapiga picha, wengine wanaongea, hakuna ule utulivu ule wa kusali. Kwa hivyo tunakuja kuangalia majengo ama picha fulani.. Na changamoto nyingine ambayo mimi nimeipata ni lugha, bado ninajifunza Kiitaliano, bado inakuja polepole lakini ndiyo changamoto sana.

Taratibu taratibu. Kuna jambo jingine ambalo unataka kuwaeleza wasikilizaji wetu wa Radio Vatican?

Sr Margaret: Jambo ambalo ningependa kuwaeleza ni kwamba ni fursa kubwa sana ukipata nafasi ya kuja kujionea Roma, ambaye ndiyo makao makuu ya dini ya Kikatoliki duniani. Ni furaha sana utafurahia. Jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu ni ile fursa ya kutembelea majengo tofauti tofauti na makanisa tofauti ambayo imani ya Kikatoliki imekua kutoka hapo. Kwa mfano kutembelea Basilika ya Mtakatifu Petro na Mtakatifu Paulo, unaona kwamba hao ndiyo viongozi wa Kanisa letu. Hiyo ni fursa kubwa sana unaipata na inakuza imani yako ya Kikatoliki. Asanteni sana.

Sr unalo lolote la mwisho tukirudi katika imani yetu au fursa ya kuja Roma kupitia katika maeneo mbali mbali?

Sister Lilian: Kwa mambo ya kiimani kama Sista mwenzangu alivyosema, kiukweli ninalopenda kuwahusia wenzangu Waafrika kule mlipo: Furahieni dini yenu, furahieni imani yenu, endeleeni hivyo hivyo kwa sababu inaonekana sasa hivi Afrika ndiyo imani inachipuka wakati wenzetu huku imekufa. Yaani wamepoteza kitu kinachoitwa Mungu. Na ukiangalia maisha yao unaona wamemweka Mungu pembeni, wana kila kitu wanachohitaji, wanachokosa katika maisha yao ni ule utulivu na amani ya kweli. Sio vitu vitakupatia amani ya kweli, lakini ukiwa umejikita katika Mungu, na sala, hiyo imani iliyoko Afrika tunaiomba sana irithishwe kwa vijana, irirhishwe kwa watoto, na familia ziwe ni vikanisa vidogo maana ndiyo msingi wa imani. Kuna neema za kutosha tujitahidi kuzichota, ili tuwe kati ya wale wachache ambao walivuka kwenda nchi ya Kanaani, au Loti na watoto wake waliovuka kwenda nchi ya uhamiaji vizuri wakafika.

Watawa wa CPS wakiwa mbele ya Gofu la Kale la Mateso ya Wakristo Jijini Roma
Watawa wa CPS wakiwa mbele ya Gofu la Kale la Mateso ya Wakristo Jijini Roma

Ninawashukuru sana Masisita wetu, Mungu awabariki na utume mwema, kwa  ushuhuda wa Sr Lilian Mdolwa kutoka Tanzania anayefanya utume wake nchini Austria, pamoja na Sr Margaret Shinga anayefanya utume wake mjini hapa Roma. Wote wawili ni wammisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu. Shukrani kwa ushuhuda wao wa kimisionari katika nchi za kigeni. Hadi siku nyingine msikose kutusikiliza kila wakati tunapotuletea makala hizi muhimu.

Masista wa Damu Azizi ya Yesu(CPS)

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

29 Julai 2026, 13:17