Tafakari Dominika 18 ya Mwaka A wa Kanisa: Upendo, Huruma na Ukarimu wa Mungu
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa familia ya Mungu, ni Dominika ya 18 mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya: “Upendo, Huruma na Ukarimu wa Mungu.” Katika safari yetu ya maisha tunakutana na njaa na kiu, dhoruba na kutindikiwa katika mambo mengi. Mwenyezi Mungu hatuachi peke yetu, anatutazama kwa upendo na anatuonea huruma. Ekaristi Takatifu ni kilelezo cha Upendo na Ukarimu huu wa Kimungu usio na mipaka. Ni Mungu, ambaye kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo anatushibisha kwa Mkate wa Mbinguni na kutuliza njaa na kiu zetu zote, katika safari yetu hapa duniani kuielekea ile karamu ya uzima wa milele mbinguni. Somo la 1: Ni kitabu cha kwanza cha Nabii Isaya 55:1-3. Somo la kwanza ni kutoka katika sehemu ya mwisho ya kitabu cha pili cha Nabii Isaya (Deutero Isaiah), kinachoanzia kimsingi ile sura ya 40-55. Mazingira ya somo hili ni nyakati za mwisho mwisho za maisha ya taifa la Israeli huko utumwani Babeli, mwaka 539 BC. Katika somo hili ningependa tutafakari mambo yafuatayo yatakayotusaidia kuelewa vyema ujumbe ambao Mama Kanisa amependa kututafakarisha katika dominika hii ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa.
Fundisho la Kwanza: Katika maisha yetu ya kila siku tunakutana na njaa na kiu mbalimbali za kiroho na kupambana kutafuta kitulizo katika mambo ya kidunia. Wakati Nabii Isaya anatoa ujumbe huu tuliousikia katika somo hili la kwanza, Wayahudi walikuwa tayari wamekaa utumwani kwa muda mrefu na walikata tamaa kabisa. Walianza kuridhika na maisha yale ya utumwani. Wengi waliozaliwa huko walihisi kusahauliwa na kutengwa na Mungu. Waliona kama Mungu wa Israeli hana nguvu na uweza kama miungu ya kipagani ya Babeli. Wakajikatia tamaa kabisa kubaki wakavu kabisa rohoni. Katika dini ya Babeli, miungu ya kipagani kama Marduk na Ishtar iliaminika kuwa ni miungu iliyoweza kudhibiti uchumi, ustawi na mafanikio. Na ili kupata kibali chao, watu walilazimika kununua dhahabu, fedha, na vifaa vya gharama kubwa ili kutengeneza au kupamba sanamu ya miungu hiyo, na hatimaye wapate baraka na mafanikio. Wayahudi, kwa kuwa nao walikua katika mahangaiko ya kukidhi njaa na kiu za maisha yao, walianza kuiga mitindo hii ya kipagani. Walijikuta wanakesha wakifanya kazi ili wapate fedha za kununua vitu vya hivi vya kifahari kwa ajili ya miungu ya Babeli. Ndio maana Nabii Isaya katika ile aya ya pili anawauliza: Kwanini kutoa fedha kwa kitu ambacho si chakula cha kweli? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Kumbe walihangaika kufanyia kazi vitu ambavyo visingewapa kamwe furaha ya kweli.
Ndugu mpendwa, hali ya Waisraeli utumwani Babeli inafanana sana na maisha ya mwanadamu wa sasa. Ingawa hatupo utumwani tena kijiografia, lakini kiroho na kisaikolojia tunapitia mazingira yale yale yaliyomfanya Nabii Isaya aandike ujumbe wa somo hili la kwanza. Waisraeli walitumia nguvu zao zote huko utumwani Babeli kufanya kazi ili kupata fedha za kununua bidhaa za kifahari na anasa kwa ajili ya miungu, lakini roho zao zilibaki tupu. Leo hii katika maisha yetu, hamu na shauku ya kila mwanadamu ni kutafuta furaha, kwa kupitia mambo mengi na kwa namna mbalimbali. Yaweza kuwa katika anasa na starehe, mali, vyeo, ufahari nk. Tunafanya kazi saa 24 (uraibu wa kazi), kwa nguvu, jitihada na moyo tukiamini utajiri utaleta furaha ya kweli. Somo hili la kwanza linatukumbusha kuwa vitu hivi vinalisha tu mwili; haviwezi kuishibisha roho ya mwanadamu ambayo iliumbwa kwa ajili ya Mungu. Waisraeli hawa walizungukwa na utamaduni wa Babeli ambapo hata baraka za miungu ya uongo zilitakiwa zinunuliwe kwa sadaka kubwa za dhahabu na fedha. Tunaishi katika ulimwengu wa kibepari (capitalism) ambapo ukiwa huna fedha hupati huduma, heshima, wala upendo. Tunaishi kwenye ulimwengu ambapo thamani ya mtu hupimwa kwa kile alicho nacho. Tutazame hata kwenye jamii na familia zetu, wenye uwezo, wenye utajiri, wana sauti, wana nguvu, wana maamuzi. Hata katika baadhi ya mazingira ya kidini leo, kuna kishawishi cha kuamini kuwa lazima tutoe fedha nyingi ili tununue miujiza au baraka za Mungu. Watu wanatoa mpaka sadaka ya kujimaliza wakiamini kuwa baraka za Mungu zinanunuliwa na kuuzwa. Nabii anasema na moyo wako, anasema na moyo wangu, “Kwa nini kutoa fedha kwa kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha?
Fundisho la Pili: Ni Mwenyezi Mungu pekee awezaye kutuliza kiu na njaa ya maisha yetu. Anatupenda, na kwa ukarimu wake anatukumbuka na kutusaidia. Taifa la Israli wakiwa katika mahangaiko hayo ya kutafuta kukidhi njaa na kiu yao wakiwa utumwa Babeli, Mwenyezi Mungu anawapelekea ujumbe wa faraja akiwaalika wajongee sasa katika karamu yenye vyakula na vinywaji tele bila malipo akisema: “Kila aonaye kiu, njooni majini, naye asiye na fedha; nunueni mle; naam, njooni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila thamani. Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema. Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono, tegeni masikio yenu, na kunijia. Sikieni, na nafsi zenu zitaishi, nami nitafanya nanyi Agano la milele, naam, rehema za Daudi zilizo imara.” Ndugu mpendwa, hakuna kitu chochote katika ulimwengu huu kinachoweza kutuliza kiu na njaa ya mioyo yetu isipokuwa Mungu pekee yake ambaye tuliumbwa kwa ajili yake. Ni yeye mwenyewe kwa wema na ukarimu wake mkuu anatualika sisi sote bure kabisa kupata chakula na maji ya uzima wa roho zetu. Licha ya kuwa mwaliko huu unaongelea vyakula na vinywaji vya kimwili lakini kimsingi unahusu zaidi chakula cha kiroho ambacho hakiwezi kununuliwa kwa fedha. Na chakula hiki ndicho akitoacho mwana wa Adamu, ndiyo Ekaristi Takatifu. Mwenyezi Mungu katika Ekaristi Takatifu anatualika tuingie katika ushirika naye katika Ufalme wake unaofananishwa na karamu nono isiyo na malipo yoyote. Kumbe, huu ni uthibitisho wa upendo wa pekee wa Mungu kwetu. Anatualika kulisikia na kulishika daima Neno lake.
Ndugu mpendwa, tunaishi katika dunia ambayo vitu vinabadilika haraka sana. Ajira zinaweza kuisha, uchumi unaweza kushuka, mali zinaweza kupotea na hata watu tunaowapenda au kututegemea wanaweza kutuacha au kutubadilikia. Hakuna kitu chenye uhakika. Ni kwa njia ya kuingia katika ushirika wa kudumu na Kristo, ndipo tunaweza kupata usalama na uhakika wa hatma ya maisha yetu. Na Agano hili ameliweka kwa njia ya damu yake ya thamani kubwa sana, watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa wakipata zawadi na mwaliko huu bure kabisa. Tunapoingia kwenye Agano hili na Mungu, tunapata uhakika kuwa haijalishi dunia itabadilika vipi, upendo wa Mungu, ulinzi wake, na ahadi zake kwetu hazitabadilika kamwe. Huu ndio uhakika wa maisha yetu ya baadaye. Tukishaingia katika Agano na Mungu tutakuwa tayari kusikia Neno lake. Neno kusikia kwa lugha ya Kiebrania ni Shema. Katika utamaduni wa Kiyahudi na katika Maandiko Matakatifu, kusikia na kutii ni kitu kimoja. Kusikia ni kufanyia kazi maelekezo ya Mungu. Ni kutafakari ujumbe tunaousikia na kujiuliza: “Hii ina maana gani kwangu binafsi? Mungu anataka nibadili nini hapa?” Ni hatua ya kuruhusu Neno hilo liwe chakula cha nafsi zetu. Kusikia kwa namna hii, ndipo Biblia inaposema “nafsi zenu zitaishi”, yaani tutaanza kuona matokeo ya uwepo wa Mungu ndani mwetu, yaani amani ya kweli, nguvu, na ustawi katika maisha yetu ya kila siku. Ni ukarimu wa pekee tunaopokea kwa Mungu mwenyewe, kama Mzaburi anavyoimba katika wimbo wa katikati, “Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.”
Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 14:13-21. Somo la Iinjili Takatifu laeleza muujiza wa Yesu kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Kabla ya muujiza huu, Bwana wetu Yesu alikuwa amepokea habari za kusikitisha za kuuawa kwa binamu yake, Yohane Mbatizaji. Aliondoka kwa mashua kwenda mahali pa faragha nyikani ili kupumzika na kusali. Hata hivyo, umati wa watu uligundua aliko na kumfuata bado kwa miguu. Yesu haangalii maumivu au uchovu wake binafsi pale mwanadamu anapokuwa na shida; upendo, huruma na ukarimu wake daima vinachukua nafasi ya kwanza. Katika dominika hii ningependa tutafakari mafundisho yafuatayo ili yatusaidie kuelewa ujumbe ambao Mama Kanisa amependa kututafakarisha. Fundisho la kwanza: Kristo daima anatutazama, na kwa upendo wake mkuu anatuonea huruma. Anahusika na mahitaji yetu yote, ya kiroho na kimwili. Katika somo hili la Injili takatifu tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo ambaye hachoki katika kuwasaidia watu. Akiwa amejitenga faraghani kusali kama ilivyokuwa kawaida yake kusali na kuongea na Baba yake, Kristo bado anaona na anajibu mahitaji ya wale waliokuwa wakimtafuta. Tunaambiwa wengi walimfuata Yesu kwa miguu kutoka mijini kwao. Na alipowaona mkutano ule mkuu aliwahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Anajishughulisha na mahitaji yote ya mwanadamu. Anaponya magonjwa yao, maana yake anaponua mwili, anawafundisha neno la Mungu yaani anaponya roho, na mwishowe anawapa chakula yaani mahitaji ya kila siku.
Ndugu mpenda kama tulivyotafakari pia katika somo la kwanza, Mwenyezi Mungu hawezi kamwe kutusahau katika mahangaiko yetu ya maisha. Ndivyo tulivyoona pia katika somo hili la Injili Takatifu. Kristo anatutazama kwa upendo, anatuonea huruma. Anatazama familia zetu, anatutazama tunavyopambana kila siku katika kazi na majukumu kwa ajili ya familia zetu, anatutazama katika changamoto zetu mbalimbali za afya, za kifamilia, za kijamii, anatutazama katika nyakati ngumu za msongo wa mawazo, anatutazama katika maumivu, kudhulumiwa, anatuonea huruma. Anatazama wale waliojeruhiwa kwa namna nyingi au hata sasa wanapitia maumivu makali moyoni, anawaonea huruma. Anatazama watoto na vijana wetu walioangukia katika uraibu wa ulevi na dawa za kulevya, athari mbalimbali za utandawazi na utamaduni mpya, Kristo anatuonea huruma. Anasikiliza sala na vilio vya wote wanaosali kwa ajili yao na kwa ajili ya uponyaji wa ndani wa wengine, wale wanaofunga safari ya kiroho kumtafuta Kristo na kuomba uponyaji wake. Kristo Yesu hatuachi vile tulivyo, hatofumbia macho kamwe mahangaiko yetu, anatutazama kwa upendo. Anatupatia daima uponyaji katika Neno lake na katika sakramenti. Kwa njia ya kitubio anatutazama kwa upendo licha ya dhambi zetu, anatupatia msamaha wa dhambi, anaponya mahusiano yaliyovunjika kati yetu na yeye na kati yetu sisi kwa sisi. Kwa njia ya sakramenti ya mpako wa wagonjwa, anawagusa wale wasio weza waliomo mahospitalini na majumbani.
Fundisho la Pili: Kristo Yesu anatualika tumkabidhi hata kidogo tulicho nacho, naye kwa wema na ukarimu wake atakizidisha. Anatualika nasi pia kuwa wakarimu. Katika somo la Injili tumesikia kwamba, ilipofika jioni, wanafunzi walitaka Yesu awaage watu waende vijijini kujinunulia chakula kwa sababu mahali pale palikuwa nyikani. Yesu anawajibu: “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Wapeni ninyi chakula.” Nao wanasema, “Hatuna kitu hapa isipokuwa mikate mitano na samaki wawili” Wanafunzi waliamini kuwa uwezo wao mdogo (mikate mitano na samaki wawili) hautoshi kitu mbele ya umati mkubwa. Yesu alitaka waelewe kwamba kazi ya Mungu inahitaji ushirikiano kati ya mwanadamu na Mungu. Anawaonyesha kuwa wanapaswa kutoa kile kidogo walichonacho kwa ukarimu, na Yeye atafanya kilichobaki kupitia muujiza wake. Ndugu mpendwa, kitendo cha Yesu kutazama mbinguni na kushukuru kwa mikate mitano na samaki wawili pekee, kinatufundisha kuwa siri ya muujiza na baraka katika maisha haipo kwenye wingi wa rasilimali tulizonazo, bali ipo kwenye moyo wa shukrani na utayari wa kukithamini kile kidogo tulichokabidhiwa. Tunapoacha kulalamika kuhusu mapungufu yetu, au changamoto za kila siku na kuanza kumshukuru Mungu kwa dhati kwa ajili ya zawadi ya uhai, afya, na kazi tuliyonayo, tunafungua milango ya kimungu ambapo yeye anavibariki vyote tulivyonavyo na kuvizidisha kwa namna ya kushangaza. Shukrani inabadilisha mtazamo wetu kutoka kwenye uhaba kwenda kwenye ukwasi, ikigeuza kile kidogo tulichonacho ili kutosheleza mahitaji yetu na hata kusalia kwa ajili ya kuwasaidia wengine wanaotuzunguka. Ombi hili la Kristo “Wapeni ninyi chakula” linatukumbusha wajibu wa Kanisa hauhusu tu kulisha roho za watu kwa Neno la Mungu, bali pia unajumuisha wajibu wa msingi wa kukabili mahitaji yao ya kimwili na kijamii. Kristo anabainisha wazi kuwa, uanafunzi wa kweli hauwezi kutenganishwa na mapambano dhidi ya umaskini, njaa, na magonjwa, jambo ambalo limekuwa ndio nguzo kuu na msingi wa taasisi za kikatoliki za misaada na maendeleo duniani kote. Kupitia agizo hili, Kanisa linaendelea kutekeleza utume wake kama chombo cha huruma inayofanya kazi, likishirikiana na Kristo kuwainua wanyonge, yatima, na wagonjwa, na hivyo kushuhudia upendo wa Mungu kwa matendo yanayogusa maisha halisi ya kila siku ya mwanadamu.
Fundisho la Tatu: Ekaristi Takatifu ni ishara ya upendo na ukarimu huu wa Kimungu, na wito wa kwenda kuwa mashuhuda wa upendo. Muujiza huu wa kuwalisha watu elfu tano, unatueleza kimsingi mambo makuu matatu. Kwanza unatueleza kuwa Kristo ni Masiha, mfano wa Musa ambaye kwa mkono wa Mungu aliwalisha Waisraeli jangwani. Pili, inadokeza matayarisho ya karamu ya Ekaristi takatifu, kuwa chakula ambacho Mungu aliwapa Waisraeli kwa njia ya Musa, ishara na alama ya upendo wake kwetu sisi sote. Na tatu inaonyesha upendo wa Mungu anayetualika sote kwenye karamu ya mbinguni kwa njia ya Yesu kwa ishara ya kuibariki na kuimega mikate mitano na samaki wawili na watu wote wakala wakashiba. Ndugu mpendwa, Kristo katika muujiza huu, kwa kubariki mikate na kuwapa mitume ili wawagawie watu, Yesu anawaonyesha wanafunzi wake kuwa wao ndio watakaokuwa watumishi wa kuwagawia watu Chakula cha Uzima yaani Ekaristi Takatifu, na atawapa uwezo wa kufanya hivyo katika karamu ya mwisho siku ya Alhamisi kuu. Agizo hili linaendelea kutekelezwa kwa njia ya Kanisa hata atakaporudi tena, kwa ajili ya uzima wa kiroho na kimwili wa taifa la Mungu. Baada ya kula na kusaza, mitume waliyaokota masazo ya vipande vya mikate vikapu kumi na viwili vimejaa. Kitendo hiki kinatufundisha kuwa, tofauti na rasilimali za kibinadamu zinazoisha na kupungua, zisizoweza kutosheleza shauku, njaa na kiu ya mioyo yetu, baraka za Kristo kila mara zinafurika na kutosheleza hitaji la kila mtu ndani ya Kanisa lake.
Hakuna baraka tunayokosa ndani ya Kanisa letu. Neno la Mungu, Sakramenti zote tunazipata ndani ya Kanisa Katoliki. Kwa nini tukahangaike kuzitafuta na kuzinunua huku na kule? Kwa nini tutange tange wakati tumeziacha ilipo hazina yetu ya kweli ndani ya kanisa letu? Idadi hii ya vikapu 12 ina maana kubwa sana ya kiteolojia. Inawakilisha mitume kumi na mbili, kila Mtume akiwa na kapu lake, wanatumwa kwenda kuwalisha kabila kumi na mbili za Israeli, yaani kuwalisha watu wa mataifa yote. Kumbe nasi tunapopokea Ekaristi Takatifu tunaondoka na wajibu. Kila mmoja anapokea kapu lake ambalo ndani mwake zimejaa baraka za Kristo, kwa ajili ya kuwashirikisha pia na wengine. Je, maisha yetu baada ya kupokea Ekaristi Takatifu yanamshuhudia kweli Kristo tuliyempokea? Tuombe neema ya kuwa mashuhuda wa upendo na ukarimu wa Kristo.Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 8:35, 37-39. Mtume Paulo anatufundisha kwamba Pendo la Mungu lisilo na mipaka limedhihirishwa kwetu katika Kristo Yesu. Nasi tukikubali kuongozwa na hilo pendo, hakuna lolote litakaloweza kututenga na Kristo, iwe shida, au dhiki, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga. Licha ya magumu yote tutakayokutana nayo Mtume Paulo anatuhakikishia ya kuwa, “Tunashinda na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Hitimisho. Tuombe neema ya kuisikia Sauti ya Kristo Yesu na kumfuata yeye ambaye kwake upo uzima na tumaini la kweli la maisha yetu, ya sasa na ya milele.