Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV akipata chakula cha mchana pamoja na maskini wa Roma. Baba Mtakatifu Leo XIV akipata chakula cha mchana pamoja na maskini wa Roma.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 18 Mwaka A wa Kanisa: Liturujia ya Neno & Ekaristi Takatifu

Ujumbe wa Neno la Mungu umejikita katika ukarimu wa Mungu kwa mwanadamu unaofumbatwa katika upendo. Yeye ni ngao na kinga ya maisha yetu, hivyo daima tumtegemee. Nasi tunapaswa kuwa walinzi, na wakarimu kwa wengine kama alivyo Mungu Baba yetu ili tuwe kama Yeye na kustahilishwa kuuona uso wake mbinguni aliko. Muujiza wa ukarimu unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu: Kuganga, Kuponya, Kusamehe na Kulisha wenye njaa!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 18 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ni siku ya 60 ya Upashanaji Habari Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa siku hii umebebwa na maneno haya; “Kulinda Sauti na Nyuso za Kibinadamu.” Baba Mtakatifu anasema kuwa katika ulimwengu wa kidigitali sauti na nyuso za kibinadamu zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa kwani ndizo alama za kipekee zinazomtambulisha kila mtu. Hivyo anasisitiza kuwa katika ulimwengu wa akili mnemba, mashine hazipaswi kuchukua nafasi ya mwanadamu kwani ni yeye pekee aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwa 1:26) na utu wake unapaswa kupewa nafasi ya kwanza kabla ya mashine. Hivyo, chochote tunachokifanya “akili unde” tutangulize kulinda na kutunza hadhi na utu wa mwanadamu. Ujumbe wa Neno la Mungu katika dominika hii umejikita katika ukarimu wa Mungu kwa mwanadamu unaofumbatwa katika upendo. Yeye ni ngao na kinga ya maisha yetu, hivyo daima tumtegemee. Nasi tunapaswa kuwa walinzi, na wakarimu kwa wengine kama alivyo Mungu Baba yetu ili tuwe kama Yeye na kustahilishwa kuuona uso wake mbinguni aliko. Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Ee Mungu, uniokoe, ee Bwana, unisaidie hima. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, ee Bwana, usikawie” (Zab. 70:1, 5). Na Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana, uwe nasi watumishi wako, utukirimie mema yako yasiyo na mwisho sisi tuombao. Uyatengeneze na kutuhifadhia mema hayo, kwa vile tunaona fahari kwamba wewe ndiwe mwumba na mfalme wetu.”

Papa Leo XIV akiangalia mitambo ya kurushia matangazo ya Radio Vatican
Papa Leo XIV akiangalia mitambo ya kurushia matangazo ya Radio Vatican   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 55:1-3). Ni mwaliko wa kuingia katika Ufalme wa Mungu unaofananishwa na karamu nono pasipo malipo. Mwaliko huu ulielekezwa kwa waisraeli wakiwa utumwa Babeli, wakipitia suluba nyingi sana, ikiwemo njaa na kiu ya kimwili na kiroho. Katika hali hiyo Mungu anawapelekea ujumbe wa faraja akiwaalika wajongee katika karamu yenye vyakula na vinywaji tele bila malipo akisema: “Kila aonaye kiu, njooni majini, naye asiye na fedha; nunueni mle; naam, njooni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila thamani. Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema. Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono, tegeni masikio yenu, na kunijia. Sikieni, na nafsi zenu zitaishi, nami nitafanya nanyi agano la milele, naam, rehema za Daudi zilizo imara.” Licha ya kuwa mwaliko huu unaongelea vyakula na vinywaji vya kimwili. Lakini unahusu zaidi chakula cha kiroho ambacho hakiwezi kununuliwa kwa fedha. Gharama yake ni Damu azizi ya Yesu, ambaye kwa upendo ilimwagika Msalabani, ikalipia gharama ya adhabu ya dhambi zetu, naye akajitoa mwenyewe kuwa chakula chetu cha kiroho, Ekaristi Takatifu; Mkate na maji ya uzima wa milele vilivyoshuka kutoka mbinguni (rej. Yn 4:10,14; 6:51). Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema. Bwana ni mwema kwa watu wote, na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, wote wamwitao kwa uaminifu” (Zab. 144:8-9, 15-18.)

Papa leo XIV akishiriki chakula cha mchana na maskini wa Roma
Papa leo XIV akishiriki chakula cha mchana na maskini wa Roma   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:35, 37-39). Ujumbe wake unalisitiza jinsi pendo la Mungu lilivyodhihirishwa kwetu katika Kristo Yesu. Nasi tukikubali kuongozwa na hilo pendo, hakuna hatari wala matatizo yawezayo kututisha na kutukatisha tamaa, “wala dhiki, wala shida, wala adha, wala njaa, wala uchi, wala hatari, wala upanga, wala mauti, wala uzima wala malaika, wala wenye mamlaka yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”. Lakini kinyume chake ni kweli, kwa wale ambao wanaukataa upendo wa Kristo na kuutupilia mbali, dhiki, shida, adha, njaa, uchi, hatari, upanga na mauti ndio chakula chao. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt.14:13-21). Ujumbe wake umegawanyika katika sehemu kuu tatu. Kwanza, inatueleza kuwa Kristo ni Masiha, mfano wa Musa ambaye kwa mkono wa Mungu aliwalisha Waisraeli jangwani. Pili, inadokeza matayarisho ya karamu ya Ekaristi takatifu, kuwa chakula ambacho Mungu aliwapa Waisraeli kwa njia ya Musa, ishara na alama ya upendo wake kwetu sisi sote. Na tatu inaonyesha upendo wa Mungu anayetualika sote kwenye karamu ya mbinguni kwa njia ya Yesu kwa ishara ya kuibariki na kuimega mikate mitano na samaki wawili na watu wote wakala wakashiba. Hivi ndivyo huruma ya Mungu inayofumbatwa katika upendo inavyojifunua kwa Yesu kuwaonea huruma watu walio kama kondoo wasio na mchungaji, kuwalisha neno lake kwa mafundisho yake, kuwaponya magonjwa yao, na kuwashibisha njaa zao.

Misa Takatifu: Liturujia ya Neno na Ekaristi Takatifu
Misa Takatifu: Liturujia ya Neno na Ekaristi Takatifu   (@Vatican Media)

Fundisho kuu hapa ni kuwa; Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, kwa pamoja vinafanya mlo kamili wa kiroho. Hivyo kupokea kimoja na kuacha kingine, madhara yake ni kuwa na utapiamlo wa kiroho. Lakini pia Yesu katika kuwalisha makutano, alifanya muujiza kwa kutumia mikate mitano na samaki wawili vilivyotolewa na mtoto mmoja. Hii inatuonyesha umuhimu wa majitoleo yetu wakati wa Sadaka ya Misa Takatifu ambapo sala na majitoleo ya vipaji mbalimbali vinageuzwa kuwa hazina yenye thamani ya kutupatia uzima wa milele baada ya maisha ya hapa duniani, kama inavyosisitiza sala ya kuombea dhabihu ikisema; “Ee Bwana, tafadhali uzitakatifuze dhabihu hizi kwa wema wako. Uikubali sadaka hii ya roho zetu, na kutufanya sisi wenyewe tuwe kwako sadaka ya milele.”Hivyo ni majitoleo yetu ndiyo yatakayofanya tustahilishwe kuingia katika uzima wa milele, kumuona Mungu aliye furaha ya kweli na ya kudumu kama anavyosisitiza Mtakatifu Agustino baada ya kuongofu akisema: “Ee Bwana, umetuumbwa kwa ajili yake, na roho zetu haziwezi kutulia mpaka zitakapotulia ndani yako”. Lakini furahi hii tunaanza kuionja kwa kuwahudumia wengine kwa upendo kwa kuwa Mungu ni Upendo. Kristo Yesu ndiye kielelezo chetu cha majitolea yetu. Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu, sisi nasi tunawajibu wa kujitoa wenyewe kuwahudumia wengine kwa maisha yetu. Haitoshi kutoa vitu tu kwa ajili ya wengine, bali pia kujitoa wenyewe katika kuwahudumia kwa vile tulivyonavyo. Basi tuombe neema za Roho Mtakatifu ili tuweze kuwa na moyo wa kuwahudumia wengine, ili tupate kustahilishwa nasi kuingia katika uzima wa milele mbinguni tukaishi pamoja na Kristo aliye shibe yetu kama anavyosali mama Kanisa katika sala baada ya komunyo akisema: “Ee Bwana, utulinde daima na popote sisi uliotutia nguvu kwa chakula cha mbinguni. Utufadhili siku zote ili tustahili ukombozi wa milele.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 18 Mwaka A wa Kanisa
29 Julai 2026, 16:17