Tafakari Dominika 16 Mwaka A wa Kanisa: Huruma na Uvumilivu wa Mwenyezi Mungu
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa wanafamilia ya Mungu, ni Dominika ya 16 mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “Huruma na Uvumilivu wa Mungu.” Mwenyezi Mungu amepanda mbegu njema ya Ufalme wake ndani ya mioyo yetu ili ikue, isitawi na kuzaa matunda bora. Lakini mara kwa mara kutokana na kuwa baridi na kulala kiroho, Shetani mwovu anapanda tena mbegu mbaya ya magugu, yaani uovu ndani ya mioyo yetu. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu mwenye Huruma hatuangamizi mara. Anatupa nafasi nyingine, ili tufanye mabadiliko na kuikumbatia tena huruma yake kabla ya hukumu ya mwisho. Sisi tunaopokea huruma ya Mungu hatuna budi nasi kuwa tayari kuwapa wengine nafasi ya pili. Tusiwe wepesi kuhukumu, wala kujihukumu, bali tuamini na kutumania utendaji kazi wa Huruma ya Mungu anayeishi daima katikati yetu. Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Hekima ya Sulemani 12:13, 16-19. Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Hekima ya Sulemani. Kitabu hiki kiliandikwa mnamo mwishoni mwa karne ya 1BC, kwa Wayahudi waliokuwa huko uhamishoni katika mji wa Alexandria, Misri (diaspora Jews). Wayahudi hawa wakiwa huko uhamishoni, walikuwa wamezungukwa na imani, mila, desturi na tamaduni mpya za kipagani za Wagiriki. Maisha yao hayakuwa rahisi, waliteseka, walinyanyasika, walidhalilishwa, walibaguliwa na kudhulumiwa na mataifa yenye nguvu yaliyowazunguka kwa sababu tu ya imani yao kwa Mungu mmoja. Katika mazingira hayo walijiuliza maswali mengi. Kwa nini Mungu mwenye nguvu na enzi anawaacha waovu waendelee kustawi na kuwatesa wateule wake pasipo kuwaangamiza mara moja? Mwandishi wa kitabu hiki anajibu swali hili kwa kufafanua mfumo wa utendaji wa Mungu. Anatoa ufunuo wa tabia ya Mungu mmoja wa Israeli, hakimu mwenye haki na nguvu lakini anayetawala, kuwajali na kuwaangalia watu wote kwa huruma, upole, na uvumilivu. Tofauti na wafalme wa kidunia ambao hutumia nguvu zao kuonea, kuhukumu na kuangamiza maadui zao kwa haraka, Mungu anatenda kazi tofauti kabisa. Hukumu ya Mungu haisukumwi na hasira, hailengi katika kuangamiza au kulipiza kisasi, bali inatawaliwa na huruma na uvumilivu unaotoa nafasi ya toba na wongofu kwa mkosaji kabla ya hukumu ya mwisho. Zaburi ya 86 tuliyoimba katika wimbo wa katikati inaelezea sifa hii ya Mungu, “Kwa maana wewe u mwema, umekuwa tayari kusamehe.”
Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 13:24-43. Katika Dominika iliyopita 15A, Mwalimu wetu Bwana wetu Yesu Kristo alianza kuwafundisha wanafunzi wake juu ya Ufalme wa Mbinguni kwa mifano (parables). Baada ya kufundisha mfano wa Mpanzi, Bwana wetu Yesu Kristo anaendelea tena katika dominika hii ya 16 A kwa kutoa mifano mingine mitatu, mfano wa Magugu katikati ya Ngano, mfano wa punje ya haradali, na mfano wa chachu. Somo hili la Injili Takatifu linatusadia kuelewa kwa kina zaidi juu ya huruma na uvumilivu wa Ufalme huu wa Mungu ulio katikati yetu, kama tulivyoona pia katika somo la kwanza. Katika dominika hii ningependa tutafakari mafundisho yafuatayo yatakayotusaidia kuelewa kwa kina ujumbe ambao Mama Kanisa anatutafakarisha katika dominika hii ya 16A: Fundisho la kwanza: Mwenyezi Mungu amepanda mbegu njema ndani ya mioyo yetu, ndio Ufalme wake aliousimika kati ya watu kwa njia ya Kristo Mwanaye. Katika Mfano wa Kwanza, Bwana wetu Yesu Kristo anaufananisha Ufalme wa Mbinguni na mtu aliyepanda Mbegu katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui na kupanda magugu katikati ya shamba la ngano. Magugu yalipoonekana, wafanyakazi wakataka kwenda kuyakusanya. Lakini mwenye shamba akawakataza wasubiri mpaka wakati wa mavuno, wasije wakang’oa pamoja na ngano pia.
Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu anapanda mbegu njema katika konde, ndiyo ndani ya mioyo yetu. Ufalme wake ni utawala wake katikati yetu, utawala uliositirika katika nafsi, maisha na utume wa Mwanaye mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ndio utawala wa upendo, furaha, amani, uvumilivu, upatanisho, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Ni mbegu bora kabisa inayotarajiwa kukua, kustawi na kuzaa matunda mengi. Dominika iliyopita ilitupa wajibu wa kuwa udongo mzuri ambapo mbegu ya Neno la Mungu itaweza kuwa na mizizi imara, kukuwa taratibu na kustawi na kisha kutoa matunda mengi. Neema na baraka za kuendelea kuwa mbegu bora na udongo mzuri tunazipata kutoka kwa Kristo mwenyewe, ndani ya Kanisa, kwa njia ya kulipokea kila mara Neno hilo na kuruhusu liguse kabisa akili na mioyo yetu. Lakini pia kwa kuishi maisha ya uchaji, kupokea Sakramenti za Kanisa na kutenga muda kwa ajili ya Mungu, ili mbegu hii iweze kutuzwa, na yule mwovu Shetani asipate nafasi hata mara moja ya kuliondoka Neno hilo, ya kuuvuruga ufalme huo ndani ya mioyo yetu, ndani ya familia zetu, ndani ya jumuiya zetu, ndani ya Kanisa, ndani ya jamii yetu na katika ulimwengu mzima.
Fundisho la pili: Mwaribifu wa Ufalme wa Mungu ndani mwetu ni Ibilisi, mwovu Shetani. Hatupaswi kulala kiroho hata mara moja. Katika mfano wa kwanza Bwana wetu Yesu Kristo anasema, “Watu walipokuwa wamelala, akaja adui na akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.” Baada ya mpanzi kupanda mbegu njema, anakuja mwovu kupanda mbegu mbaya, anapanda magugu katikati ya ngano. Ndugu mpendwa, mwaribifu wa mbegu njema iliyopandwa ndani ya mioyo yetu, mwaribifu wa Ufalme wa Mungu unaopaswa kukuwa na kustawi katikati yetu ni yule mwovu shetani. Mwenyezi Mungu anapopanda mbegu njema ndani mwetu, anataka mbegu hiyo njema ikue, iwe na mizizi imara, ichanue na kustawi na kisha itoe mazao stahiki. Kama imepandwa mbegu njema ndani mwetu ni wazi matokeo yake yatakuwa mema. Hakuna mbegu ya ngano inayotarajiwa kuzaa magugu, kwa kuwa ni mbegu bora kabisa iliyopandwa na Mungu mwenyewe. Lakini sisi tunapolala kiroho, yule adui mwovu shetani anapanda kwa siri mbegu mbaya ndani mwetu. Magugu haya anayozungumzia Kristo, yalikuwa kawaida yanafanana kabisa na ngano wakati yakiwa bado madogo, kwa hivyo ni ngumu kuyatambua kwa haraka. Kumbe, nasi tunapolala kiroho, tunaoacha kusali, tunapoacha kupokea Sakramenti za Kanisa, tunaposhindwa kutimiza vyema wajibu wetu, shetani anapata nafasi ya kupanda mbegu mbaya ndani mwetu. Pia anakuja kwetu kwa njia ya hila, kupitia mafundisho ya uwongo yanayoonekana kufanana kabisa na yale ya kweli, kupitia watu, vitu, mazingira mbalimbali, anaweka uovu ndani mwetu, ndani ya familia zetu, ndani ya Kanisa, na jamii yetu. Lengo la mwovu, ni ili mwenye shamba akate tamaa na aharibu shamba zima. Ni jaribu la kuonesha nguvu ya uovu katikati ya wema wa Mungu mkuu.
Fundisho la tatu: Mwenyezi Mungu si mwepesi katika kuwaangamiza wale walio waovu, bali kwa huruma yake kuu anawapatia nafasi ya kufanya mabadiliko. Hatupaswi kuhukumu, Kristo mwenyewe ndiye Hakimu mwenye haki. Katika mfano wa kwanza, watumwa wale walikua wepesi sana kufikiri kuyang’oa na kuyateketeza magugu mara tu walipoyagundua kuwa yameota katikati ya ngano iliyo bora. Lakini tunaona mtazamo wa Bwana mwenye shamba ni tofauti kabisa, yeye anasema, viacheni vikue pamoja, na wakati wa kuvuna nitawaambia wavunao, yakusanyeni kwanza magugu, mkayafunge matita matita, mkayatupe motoni, bali ngano ikusanyeni ghalani. Mwenye shamba anatoa nafasi kwa vyote, mbegu bora ya ngano pamoja na magugu vikue. Kristo anatualika tutambue kuwa hukumu ya mwisho ipo, lakini bado tuna nafasi kila mara ya kufanya mabadiliko ya kweli na kuanza tena upya, haijalishi tumekua magugu muda mrefu kiasi gani. Ndugu mpendwa, katika somo la kwanza, tuliona mtazamo wa Wayahudi wakati wakiwa huko uhamishoni, walijiuliza maswali mengi sana juu ya utendaji kazi wa Mungu. Walishangaa kwa nini Mwenyezi Mungu ana huruma iliyopitiliza? Kwa nini anawaacha waovu waendelee kukuwa na kustawi hata kuliko wale wenye haki? Kwa nini Mwenyezi Mungu hatoi hukumu ya haki kwa wakati? Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma. Ukuu, nguvu, enzi na utukufu havipo katika kutuangamiza sisi mara tu tunapotenda dhambi, bali kuturehemu na kutupatia daima nafasi ya kufanya mabadiliko. Hebu tufikiri mimi na wewe kama kila tulipotenda dhambi Mwenyezi Mungu angetuadhibu na kutuangamiza sa ile ile, hakika hakuna mtu angekua amesalia. Watakatifu wengi, tumtazame Petro na Paulo na wengine wengi walipata nafasi ya kutubu, wakaongoka na wakawa watakatifu na ndiyo safari ya kila mmoja wetu. Kristo anafundisha kuwa tusiwe wepesi katika kutoa hukumu, bali tuwasaidie waregevu kwa sala na mifano bora ya maisha yetu ili waweze kuongoka na kuikumbatia huruma ya Mungu wetu. Ni kweli kiuhalisia magugu hayawezi kuwa ngano, lakini sisi wanadamu, tulio waovu na dhaifu twapata nafasi na neema ya kutubadilisha. Mwenyezi Mungu anatuacha sote tukue pamoja, wema na waovu, ili kila mmoja wetu apate nafasi ya kubadilika na kuwa ngano bora katika Ufalme wa Mungu. Hatupaswi kujikatia tamaa wala kuwakatia tamaa wengine, hatupaswi kuhukumu na kuwaona waovu kama hawana nafasi kwa Mungu. Machoni petu twaweza kuwaona wengine kuwa magugu lakini machoni pa Mungu wakaonekana mbegu bora ya ngano safi, kwa kuwa sisi sio watoa hukumu, bali anayehukumu ni Mungu mwenyewe.
Fundisho la nne: Mwanzo wa Ufalme wa Mbinguni ni mdogo, lakini matokeo yake ya wazi kati yetu ni makubwa sana. Katika Mfano wa pili, Yesu anaufananisha Ufalme wa Mbinguni na mbegu ya haradali ambayo ni mbegu ndogo zaidi kuliko zote, lakini ilipopandwa ilikuwa mti mkubwa sana hata ndege wa angani huja na kutua hapo. Kristo anaufananisha Ufalme wa mbinguni na mbegu ya haradali kwa sababu ya sifa kuu mbili: udogo wake wa mwanzo na ukubwa wake wa mwisho baada ya kukua. Mfano huu unafundisha jinsi Ufalme wa Mungu unavyofanya kazi duniani na katika roho zetu. Ndugu mpendwa, kama ilivyo ndogo mbegu ya haradali, ndivyo Ufalme wa Mungu ulivyoanza kudhihirika kati ya watu. Ulianza katika udogo na unyenyekevu mkubwa kwa njia ya maisha na utume wa Kristo. Licha ya udogo wake, mbegu hiyo imekuwa mti mkubwa. Kanisa na Injili ya Kristo vimeendelea kukuwa na vimeenea duniani kote na kuleta mabadiliko makubwa kutoka kwa kundi lile dogo la jumuiya ya wakristo wa mwanzo. Kumbe ndivyo Ufalme huo unavyokua na kustawi pia ndani mwetu. Moyoni mwetu, Ufalme wa Mungu unaweza kuanza taratibu sana, kwa kuwa na mazoea ya kusali, hata sala fupi tu kila siku, hamu ya kusoma Neno la Mungu walau aya kadhaa kila siku, hamu ya kujitahidi daima kuepuka vishawishi mbalimbali na hila na mitego ya Shetani, na nia ya dhati ya kuacha vilema na dhambi zinazonishinda, au ambazo zimekua zikijirudia rudia kila wakati, lakini pia hamu ya kupokea Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Kitubio. Hatupaswi kukata tamaa na kuona kana kwamba jitihada zetu hazina matokeo. Tukiitunza hiyo nia ndogo kwa neema ya Mungu, itakua na kuwa imani kubwa na thabiti. Matokeo ya ufalme huu ni kwamba ndege wa angani wanakuja na kufanya viota katika matawi yake, ishara ya kwamba Ufalme wa Mungu unajumuisha na kuwakaribisha watu wa mataifa yote, tamaduni zote, na makabila yote kupata wokovu, usalama, na pumziko. Kila tunachofanya kwa ajili ya Mungu na jirani, hata kikiwa kidogo tu kama vile kutabasamu, kutoa msaada hata kama ni kidogo kwa upendo mkubwa, kusema neno la faraja kwa wanaohuzunika, kusamehe na kuomba msamaha, vina nguvu kubwa ya kukua na kuleta matokeo makubwa tusiyoyatarajia katika maisha yetu na ya wengine. Kama vile mti wa haradali unavyokuwa kimbilio la ndege, maisha yetu yanapaswa kuwa chanzo cha ulinzi, faraja, makimbilio na amani kwa watu wanaoteseka, waliovunjika moyo, au wanaotafuta msaada karibu yetu.
Fundisho la tano: Ufalme wa Mungu ulio ndani mwetu huweza kuharibiwa na vitu vidogo vidogo na kwa taratibu sana. Lakini pia huweza kukua na kusambaa na kuenea taratibu na kwa ukimya kwa nguvu ya ajabu. Katika Mfano wa tatu, Bwana wetu Yesu Kristo anaufananisha Ufalme wa Mungu na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga hata ukachacha wote pia. Mpendwa, kawaida chachu ikichanganywa kwenye unga haionekani kwa macho, lakini nguvu yake inafanya kazi kimyakimya kutoka ndani na kuchachusha unga wote. Ndivyo Ufalme wa Mungu unavyokua ndani ya mioyo yetu, mara nyingi sio kwa makelele au mambo makubwa ya nje kama tulivyoona pia katika mfano wa mbegu ya haradali, bali kwa neema ya siri inayobadilisha maisha yetu taratibu toka ndani. Kumbe, kama vile chachu inavyoenea na kuathiri kila sehemu ya unga, nasi Wakristo tunaalikwa kuwa chachu duniani. Uwepo wetu, matendo yetu mema, na upendo wetu vinapaswa kuathiri na kubadilisha jamii inayotuzunguka kuelekea kwenye wema. Wakristo twapaswa kuishi maisha ya mfano na ushuhuda wa Injili, kutenda haki, kusema ukweli, kukemea maovu, kutetea wanyonge, kuhurumiana, kusameheana, kuinuana, kushikana mikono na kutembea pamoja na kuwaziana daima yaliyo mema. Kama vile chachu isivyoonekana ikichanganywa kwenye unga lakini baada ya muda mfupi inabadilisha unga mzima, dhambi ndogo au tabia mbaya ikiruhusiwa kuingia moyoni mwa mtu kama vile choyo, uongo, au tamaa inasambaa kwa siri katika fikra zake. Baada ya muda, inateka maisha yake yote na kumtenganisha kabisa na Mungu, lakini pia ina uwezo wa kuambukiza na wengine pia wakawa mbali na Mungu. Wazo moja potofu au mafundisho ya uongo yakiingizwa ndani ya jumuiya, jamii au Kanisa, yanaweza kupotosha waamini wengi hasa walio dhaifu na wachanga bado katika imani. Mtume Paulo anatulika tuitoe chachu ya kale ndani mwetu, na tuwe tayari kuwa donge jipya (1Kor 5:6-7). Ni neema ya Kristo mfufuka ndiyo inayotufanya upya ndani mwetu.
Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 8:26-27. Fundisho la sita: Roho Mtakatifu anatusaidia katika udhaifu wetu. Tunaposhindwa kuwa mbegu bora, anatusaidia kurejesha upya uhusiano mwema na Mungu wetu mwenye Huruma na uvumilivu. Kama tulivyoona katika somo la Injili Takatifu kuwa mara kwa mara tunalala kiroho na kuruhusu magugu yakue katikati ya ngano bora. Mtume Paulo anasema, “Roho hutusaidia katika udhaifu wetu”. Mwenyezi Mungu hatuachi tuangamie; anatupa msaada wa Roho wake ili kutunyanyua pale tunapoishiwa nguvu. Sala ndiyo chachu iliyo ndani ya mioyo yetu, inayotuunganisha daima na Mungu na kutupa nguvu ya kudumu katika Ufalme wake. Somo la pili linaonesha sasa chachu hiyo ikitenda kazi ambapo Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Hata pale tusipojua jinsi ya kusali au namna ya kupambana na dhambi, Roho Mtakatifu anafanya kazi kwa siri ndani ya mioyo yetu ili kututakasa na kutukuza kiroho. Lakini wakati fulani sala zetu na juhudi zetu zinaweza kuonekana ndogo na hafifu kama mbegu ya haradali kwa sababu ya ubinadamu wetu. Lakini, Roho Mtakatifu anapozichukua sala hizo na kuziwasilisha kwa Baba, anazipa thamani kubwa na kuziwezesha kuzaa matunda makubwa ya neema maishani mwetu. Hitimisho: Katika Dominika hii, tuombe neema ya kutotumia vibaya sifa hii ya Mungu, ya huruma, wema na uvumilivu. Tumwombe Mungu atujalie nguvu ya kuupokea Ufalme wa Mungu, na kuishi kadiri ya mapenzi yake ili tuupate uzima wa milele baada ya maisha haya ya hapa duniani.